2018-04-12 07:00:00

Papa Francisko: Utakatifu: mwanga na alama katika maisha ya Mwalimu


Baba Mtakatifu Francisko ametoa Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) umezinduliwa, Jumatatu, tarehe 9 Aprili 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Wosia huu wa kitume umegawanyika katika sura kuu tano: Sura ya kwanza ni Wito wa utakatifu; Sura ya Pili ni Adui wa utakatifu; Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu, Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo na Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi! Vatican News inapenda kukushirikisha kwa muhtasari sura ya tatu na ya nne!

Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuambata Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu yanayoweza kuwasaidia kufikia utakatifu wa maisha. Umaskini wa roho ni kielelezo cha utakatifu; Upole ni sehemu ya Matunda ya Roho Mtakatifu. Mwamini kwa kufikiri na kutenda katika upole anaonesha cheche za utakatifu wa maisha. Waamini wajifunze kuhuzunika na kuomboleza na jirani zao; kwa kuwa na njaa na kiu ya haki; kwa kuona na  kutenda katika huruma; kwa kuwa na moyo safi; kwa kupandikiza na kukuza mbegu ya upatanishi na amani!

Baba Mtakatifu anasema, Heri za Mlimani zinawasaidia waamini kufuata nyayo za Kristo Yesu Bwana na Mwalimu wao! Waamini wakumbuke kwamba, siku ya mwisho watahukumiwa kadiri walivyowatendea kwa upendo jirani zao walio wadogo, ambao Kristo Yesu anajifafanisha nao! Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Bwana na Mwalimu wao! Waamini waendelee kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kutekeleza kwa dhati matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama ambavyo wamehimizwa wakati wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Matendo ya huruma ni kiini cha Injili ya Kristo inayolenga kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maskini ni amana na hazina ya Kanisa, kwani wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anawalika waamini kufuata nyayo za Kristo kwa njia ya sala na ibada; kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na upendo unaomwilishwa katika huruma! Waamini wajiepushe na tamaa ya kupenda malimwengu, raha na anasa za dunia hii, waguswe na mahangaiko pamoja na mateso ya jirani zao kwa kujibu kilio chao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama njia makini ya kuendelea kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha ya watu! Ushuhuda wa watakatifu umefumbatwa katika Heri za Mlimani na Matendo ya Huruma; chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha ya Kikristo!

Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu katika sura hii anapenda kukazia zaidi: udumifu, uvumilivu na unyenyekevu wa moyo kama alama za utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo dhidi ya tabia matumizi ya nguvu, ubinafsi na uchoyo pamoja na hali ya mtu kujiridhisha binafsi katika ufahari wake. Wakristo wawe wanyenyekevu kwa kujikita katika ukweli na uwazi; utu wema pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya ulimi!

Waamini wafurahie pia mafanikio ya jirani zao, wawasahihishe kwa upole na udugu pale wanapolegea katika dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa na huu ni ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo. Kuna waamini wanaoendelea kusimamia haki, amani na maridhiano katika jamii kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Hawa wanahesabika kuwa ni vyombo vya amani! Maisha ya Kikristo ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, furaha ya kweli inafumbatwa katika upendo!

Wakristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na utulivu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha umoja na upendo wa kidugu. Waamini waoneshe uhuru na upendo wa ndani kabisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya upya wa maisha yao! Familia ya Mungu ioneshe ujasiri wa kutoka kifua mbele kama ilivyokuwa kwa watakatifu wa nyakati mbali mbali ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utakatifu ni hija inayofumbatwa pia katika maisha ya kijumuiya na Mama Kanisa anayo mifano kede kede ya Jumuiya za watakatifu. Hawa ndio akina Paul Miki na wenzake au Wamonaki waliouwawa hivi karibuni huko Algeria. Hawa ni watakatifu ambao wameishi kwa pamoja huku wakiadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kujenga umoja na udugu. Hawa ni kama Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali pa kurutubisha upendo, umoja na udugu; kwa kusaidiana na kutakatifuzana katika maisha, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, utakatifu unafumbatwa katika maisha ya sala kama sehemu ya mchakato wa kutaka kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kumbe, sala endelevu ni chachu ya utakatifu wa maisha! Ukimya na tafakuri  ni nyenzo zinazojenga uhusiano mwema na Kristo! Lakini, sala ya kweli inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yanayofumbatwa katika upendo. Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha kwani hiki ni kiini na utambulisho wa Kanisa. Waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Sakramenti za Kanisa, ili waweze kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.