2018-04-12 15:24:00

Papa Francisko asikitishwa sana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na vitendo vya nyanyaso za kijinsia vilivyofanywa na baadhi ya viongozi wa Kanisa nchini Chile. Anasikitika kusema kwamba, amejikuta akitumbukia katika ombwe kubwa kiasi cha kushindwa kufanya upembuzi yakinifu baada ya kukosa taarifa kamili kuhusu ukweli wa nyanyaso za kijinsia zilizotendwa nchini Chile. Baba Mtakatifu anaomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika maamuzi haya na kuwaalika Maaskofu wa Chile kuja mjini Vatican, ili waweze kujadili kwa pamoja taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Askofu mkuu Charles Jude Scicluna. Taarifa kutoka katika Baraza la Maaskofu Katoliki Chile katika barua ambayo Baba Mtakatifu amewaandikia Maaskofu wa Chile anaonesha kusikitishwa sana baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi kutoka kwa Askofu mkuu Charles Jude Scicluna aliyekuwa amekabidhiwa kuchunguza shutuma hizi.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni mara baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Chile iliyokuwa ikiongozwa na kauli mbiu “Amani yangu nawapeni” alisema, kwa ujumla, hija yake ilikuwa na mafanikio makubwa licha ya maandamano na vurugu zilizojitokeza kabla na wakati wa hija yake ya kitume, kiasi cha Makanisa kadhaa kuchomwa moto! Baba Mtakatifu alisikitika kusema, kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Chile zimechafua maisha na utume wa Kanisa na kwamba, alichukua fursa ya hija yake ya kitume, kuomba msamaha kwa wale wote waliotikiswa na kuguswa na kashfa hii!

Kashfa hii ilichafua ukurasa wa hija ya Baba Mtakatifu nchini Chile alipoonekana kana kwamba, alikuwa anamtetea Askofu Juan de la Cruz Barros Madrid, wa Jimbo Katoliki Osorno nchini Chile, kwa kutaka ushahidi ili aweze kumwajibisha Askofu wa Osorno dhidi ya shutuma zilizokuwa zinamwandama! Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia utete wa tatizo hili kimaadili “Delicta graviora”, aliamua kumtuma Askofu mkuu Charles J. Scicluna, wa Jimbo kuu la Malta na Monsinyo Jordi Bertomeu, Afisa wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwenda nchini Chile ili kusikiliza shutuma na kukusanya ushahidi, ili hatimaye, kesi hii iweze kujadiliwa kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na maamuzi kuchukuliwa kwa kuzingatia ukweli, uwazi na haki kwa wale wote wanaohusika!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, baada ya kusoma taarifa ya uchunguzi wa kashfa ya nyanyaso sasa anaweza kusema kwa uhakika kwamba, ushuhuda uliotolewa unaonesha mateso makali ambayo watu wamekumbana nayo, kiasi cha kuamsha ndani mwake uchungu mkubwa na aibu katika maisha na utume wa Kanisa!Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wa Chile waliokuwa wanakutana kwenye mkutano wao wa 115 kwa unyenyekevu kuomba ushirikiano wao, ili kujadili kwa pamoja na hatimaye, kufanya maamuzi ya muda mrefu, kati na ya haraka, ili kurejesha tena imani na matumaini kwa Kanisa nchini Chile, kwa kurekebisha kashfa hii pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka kwa waathirika. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuomba msamaha kwa kukosa vigezo muhimu katika kuamua katika ukweli na uwazi kuhusu kashfa za nyanyaso zilizojitokeza nchini Chile. Anawaomba msamaha wale wote wanaojisikia pia kukosewa haki kutokana na msimamo wake wa awali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.