2018-04-12 15:50:00

Kristo Mfufuka ameondoa hofu na mashaka, sasa ni ushuhuda tu!


Katika kanuni za kimaumbile habari ya mmoja aliyethibitishwa kufa na hata kuzikwa kwamba amefufuka huzusha tafrani na mara nyingi haipokeleki kirahisi. Vyombo vya habari hutupatia taarifa mbalimbali za mmoja aliyekufa na kuonekana tena lakini mara zote huusianishwa na ushirikina. Hawa wanaoonekana wapo hai tena hupokelewa kama wale waliochukuliwa misukule katika namna ya ushirikina na hata kukubalika kwao katika jamii bado huwa ni kwa polepole na kwa mashaka. Hili linaweza kuonekana kwa ilivyokuwa habari ya ufufuko wa Kristo. Habari hii haikupokeleka au kuelewaka kirahisi sana. Kwa mitume na wafuasi wake wanakuta kaburi lake lipo wazi. Lazima watajiuliza amekwenda wapi? Je! Ameibiwa? Lakini matukio yanayofuta ya kuwatokea wafuasi wake kwa nafasi mbalimbali yalilenga katika kuthibitisha kuwa hakuibiwa bali yu hai. Lakini, huo uhai wake hatuwezi kuufananisha na wa misukule? Tofauti yake ni nini? Na huo uhai wake una maana gani katika safari yetu ya kiroho na katika maisha ya Kanisa kwa ujumla wake?

Injili ya Dominika hii inamwonesha Kristo anayewatokea wafuasi wake. Kilichotokea katika mkutano huo ni hofu na mashaka: “Alisimama katikati yao akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho”. Wafuasi hawa walikuwa wakisikiliza simulizi la wenzao kwa jinsi alivyowatokea na kumtambua katika kuumega mkate. Lakini hofu na mshituko wao ulionesha kuwa bado walikuwa wametawaliwa na mawazo ya kibinadamu ambayo kama tulivyoanza kuelezea mwanzoni, yalishindwa kuelezea ukweli wa tukio la ufufuko. Linalofuata baada ya hapo ndilo muhimu linaloudadavua umuhimu wa tukio la ufufuko katika imani yetu. Kwanza anawaonesha madonda yake: “Tazamaeni mikono yangu na miguu yangu… nishikenishikeni; mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa navyo”. Alianza kwa kuwathibitishia kuwa ni Yeye kabisa, «live bila chenga»; ni Yeye ambaye alisulibiwa kwa uthibitisho wa madonda yake na hivyo kumuunganisha Kristo mfufuka na Yeye waliyemtambua wakati wa maisha yake ya hadharani.

Hatua hiyo isingetosha kufafanua zaidi kwani hata misukule nayo huwa ni mtu yule yule ambaye tulimfahamu, ambaye anakuwa anaonekana amekufa kumbe katika hali ya kimazingara hufichwa kwa makusudi ya kishirikina. Ndipo hapo tunapomuona Kristo anaelezea namna ambavyo ufufuko wake ulikwishaelezewa tangu mwanzo katika maandiko matakatifu kama mpango wa Mungu wa kutukomboa sisi wanadamu: “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu”. Tukio hilo halikutokea kwa nasibu tu au bila kuwa na mpango. Ufufuko wa Kristo ni mpango wa mwenyezi Mungu wa kumrudishia mwanadamu hadhi yake ambayo aliipoteza kwa sababu ya dhambi. Yeye alikufa ili kuzifuta dhambi zetu na akafufuka ishara ya uhai mpya ndani mwetu. Hivyo ufufuko wa Kristo ni muhimu kwa uhai na maisha ya jumuiya nzima ya Kanisa ambayo inajitambulisha kama jumuiya inayompeleka mwanadamu katika wokovu.

Katika Injili hiyo Kristo anawaagiza wafuasi wake kuwa mashahidi wa habari hii njema na muujiza huu mkubwa: “Nanyi mtakuwa mashahidi wa mambo haya”. Hitimisho hilo linatuunganisha na ujasiri wa mtume Petro tunaouona katika somo la kwanza. Petro anawaambia watu jinsi ambavyo walikataa uhai na kuchagua kifo hadi kusababisha kifo cha Kristo: “Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; Mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake”. Hapa kwa ufupi kabisa anauweka wazi utume wa Kanisa ambayo ni jumuiya ya ufufuko: ni kuutangaza ushindi wa uhai dhidi ya kifo; nuru dhidi ya giza. Mlimuua yule mkuu wa uzima lakini Mungu amemfufua katika wafu. Kifo au giza vinajidhihirisha katika maisha ya dhambi, yaani pale mwanadamu anapokataa uwepo wa Mungu kati yake.

Ufufuko wa Kristo unathibitisha ushindi wa mpango wa Mungu dhidi ya dhambi. Wajibu wa Kanisa katika kushuhudia ushindi huu unahitajika kutelezwa kwa namna ya pekee katika ulimwengu wetu wa leo. Kanisa, ambalo hujumuisha jumuiya ya wabatizwa linaalikwa kutoa ushuhuda wa upya wa maisha kama changamoto kwa jamii ya leo, ushuhuda ambao utalenga katika kufanya mabadiliko na kuwa suluhisho kwa changamoto mbalimbali kijamii. Ushuhuda huo unapaswa kuhakisi yale ambaye tumeelekezwa na Kristo mfufuka wakati wa maisha yake ya hadharani. Utume wa Kristo wakati wa maisha ya hadharani ulijikita katika kumwelekeza mwanadamu namna ya kuurejeza uhusiano wake na Mungu. Mafundisho, miujiza na hata uponyaji ulimfanya mwanadamu kuonja tena uwepo wa mkono wa Mungu wenye nguvu, na wenye kuokoa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo, anatupatia changamoto ya kufuata wito wa utakatifu wa maisha. Ni waraka ambao unatambua uwepo wa cheche za utakatifu katika kila nafsi ya mwanadamu. Ushuhuda wetu kama wanakanisa unapaswa kuwaelekeza wote katika katika njia hiyo. Kanisa lijaribu kuepuka kuonesha kuwa utakatifu ni wa wateluliwa wachache. Utakatifu ni zawadi inayotolewa na Mungu kwa ajili ya watu wote. Ipo hatari ya kuwaona waasi, wapinzani na walioanguka kama wasio na nafasi katika wokovu. Mtume Petro anatupatia mfano. Pamoja na kuwakumbusha watu wa uyahudi uovu wao kwa kuukataa uzima na kukipokea kifo anawaalika akisema: “Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda… tubuni basi mrejee ili dhambi zenu zifutwe”.

Mtume Yohane anaongezea kwamba tufanye toba na kuzishika amri zake. Hapo upendo wa Mungu utakuwa umekamilika kweli kweli. Ni mahusia ambayo yanatutaka sisi tulio mashahidi wa ufufuko kuweka Neno la Mungu kama kielelezo cha maisha yetu ya wokovu. Mungu abaki kuwa chemchemi ambayo kwayo tunachota maana ya uwepo wetu. Ni kisima chenye hekima zote na majawabu yote kwa maisha ya mwanadamu. Toba ya dhambi inaambatana na maisha mapya. Maisha hayo yanaonekana kwa uwepo wa upendo mkamilifu wa Mungu. Kwa maneno mengine toba ni chachu ya kusonga mbele katika safari ya kuelekea ukamilifu. Kila tufanyapo tendo la toba upendo wa Mungu uzidi kukua ndani mwetu. Upendo huo unaonekana kukua kwa namna sisi tunavyozishika amri zake.

Sisi tulio katika imani hii ya Kristo mfufuka tunayo hakika ya ufufuko wake na tumefafanuliwa kila mara maana yake na tija yake katika maisha yetu kiimani. Hivyo ushuhuda wetu katika ulimwengu wetu wa leo unapaswa kuonekana kwa nguvu nyingi na ujasiri mkubwa. Kristo mfufuka amejionesha kwetu kwa ishara mbalimbali za kiimani na hivyo hatuna hofu, woga wala mashaka kama wafuasi wa kwanza wa Kristo. Muhimu kwetu ni kujifunua mioyo yetu na kumpatia nafasi Kristo mfufuka akutane na nafsi zetu, aondoe giza la dhambi, atuondoe katika kifo na uvuli wa mauti na hatimaye tutembee katika mwanga na uhai wa wana wa Mungu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.