2018-04-11 15:44:00

Waamini shindeni woga ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka!


Jumapili iliyopita tulitafakari juu ya huruma ya Mungu au huruma takatifu. Jumapili hii ya leo tunaitwa kushiriki imani pamoja na wengine. Yesu ataka wafuasi wake kuwa mashahidi na mashuhuda. Ushuhuda: upande mmoja wanatakiwa kuona tukio, kupata ufahamu wa kitu kwa ushuhuda binafsi na siyo kusikia tu. Kwa upande mwingine: yahusisha uwezo wa kuweza kuelezea tukio hilo mbele ya wengine.

Mwaliko wa kuwa mashuhuda maana yake ni kwamba tunaitwa kwanza kuona tukio hilo halafu kushirikisha tukio hilo kwa wengine. Bahati mbaya wakristo wengi wanaishia nusu nusu katika ujuzi huu. Wengi hukazia kumfahamu Kristo, lakini hawako tayari au hawafikii kiwango cha kushirikisha ufahamu huo kwa wengine kwa ushuhuda wa maisha yao. Tunakumbushwa kuwa imani hufananishwa na mshumaa uwakao – jinsi ile mshumaa huo unavyowasha mishumaa mingine, ni kiasi hicho hicho mwanga huenea. Vinginevyo mshumaa huisha na moto na mwanga wake hupotea. Baba yake Martin Bubber yule mwanafalsafa Myahudi (falsafa ya mazungumzano) aliombwa aelezee ufasaha wa mwalimu wake. Huyu baba alikuwa kilema. Lakini ajabu ni kwamba alipoombwa kufanya hivyo alisimama na kuanza kuelezea kwa kuruka ruka na kucheza kama alivykuwa akifanya mwalimu wake huyo wakati akiwa darasani. Tangu siku hiyo akapona na ugonjwa wake wa kulemaa.

Ndugu zangu, tunapoongea habari ya Yesu Kristo, tunafanya mambo mawili makuu. Moja tunawasaidia wengine kumfahamu na wakati huo huo nasi wenyewe tunapata kumfahamu zaidi. Ndivyo ilivyo katika Injili ya leo. Katika Injili ya  Lk. 24:36 – tunawasikia wafuasi wawili – walirejea Yerusalemu kuwaelezea wengine baada ya kumfahamu Yesu. Lakini kabla ya hapo, katika harakati za kushirikishana imani – Yesu anatokea katikati yao. Nao wanapowaeleza wenzao kile walichokiona – nao wale wengine wakapata kuamini.

Yesu anafanya nini kwao wanaompata? Kwanza, anawapatia amani yake katika mioyo yao iliyofadhaika. Halafu anajaribu kuwaonesha kwamba yule Yesu aliyekufa kifo cha aibu msalabani ndiye aliye mbele yao. Zaidi ya hilo hata anakula chakula ili kudhihirisha anachosema. Halafu anaangazia akili zao ili kuelewa Maandiko na jinsi yanavyomwelezea. Tena anawatuma wakawe mashuhuda wake – Lk. 24,48. Ndivyo alivyofanya mbele ya mitume wake, na ndivyo anavyotokea kati yetu leo hii. Angalia jinsi Yesu anavyowajibika mbele yao na kwa ajili yao. Anawapa amani. Anawaimarisha imani yao na kuwaondolea wasiwasi wao. Anafungua akili zao na kuwaelezea Maandiko Matakatifu. Anawapatia ushuhuda wake. Mitume wanachofanya ni kufungua macho yao kuona, mioyo yao kupokea amani na akili zao kupokea mafundisho yake. Na anapowaambia nendeni, wanakuwa tayari kufanya hivyo.

Ni kwa jinsi gani tunamshuhudia Kristo? Pengine ushuhuda wetu kwa Kristo unakuwa mgumu kwa vile wengi wetu hatuupati vyema ujumbe huu wa Kristo. Pengine njia zinazotumika siyo nzuri katika kuufikisha ujumbe huu. Kadiri ya Yesu – njia ni rahisi – angalia wafuasi wawili wa Emmaus – wanaongea juu ya kile kilichotokea na wanaongea kukutana kwao na Kristo. Ni kuwashirikisha ni kwa nini sisi ni wakristo. Pengine shida yetu, kama asemavyo padre mmoja ni kuwa tunatumia muda mwingi kuongea juu ya Mungu badala ya kuongea na Mungu. Mwandishi mmoja kwa jina Peter Marshal anasema ‘mkristo si mtu anayejaribu kufanya kitu, ni mtu aliyepokea kitu tayari, ni mtu ambaye tayari kitu kimeshatokea kwake na kwa hiyo hawezi kukaa kimya’. Naye Mtume Petro anasema katika 1 Pt. 3;15 – kuwa - mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu, lakini kwa upole na kwa hofu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.