2018-04-11 14:09:00

Ubatizo ni msingi wa maisha ya Kikristo na lango la uzima katika Roho


Yesu Mfufuka aliwatuma wanafunzi wake akisema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”. (Mt. 28:19-20). Kipindi cha Pasaka, yaani siku 50 za kushangilia Fumbo la Pasaka ni muda muafaka wa kutafakari kuhusu maisha ya Kikristo yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Mfufuka. Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo na lango la kuingilia uzima katika Roho na hivyo kumruhusu Kristo Yesu kufanya makazi katika maisha ya waja wake, na wao kuzama katika Fumbo la maisha yake!

Huu ni utangulizi wa Katekesi kuhusu Sakramenti ya Ubatizo, uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 11 Aprili 2018 baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu Ibada ya Misa Takatifu. Ubatizo ni neno la Kigiriki “Baptizein” maana yake “kutumbukizwa” au “kuzamishwa” ndani ya maji, alama ya maziko ya mkatekumeni katika mauti ya Kristo Yesu ambamo anafufuka pamoja naye, huku akiwa ni kiumbe kipya. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwamini anazamishwa: kiroho na kimwili ili kuweza kupokea msamaha wa dhambi na hatimaye, kuuwezesha mwanga wa kimungu kung’ara katika maisha yake.

Kwa njia ya Roho Mtakatifu, katika Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anazamishwa katika Fumbo la kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ili kuuvua utu wa kale uliochakaa kama “jani la mgomba” kutokana na dhambi inayomtenganisha mtu na Mwenyezi Mungu na hivyo kuweza kuibuka tena kama mtu mpya, aliyeumbwa upya na Kristo Yesu, ambaye kwa njia yake, watoto wote wa Adamu wanaalikwa kuishi maisha mapya. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kukumbuka siku yao ya Ubatizo na kuisherehekea kama mwanzo wa maisha mapya katika Kristo Yesu. Hii ni siku ya kumshukuru Mungu, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Kristo Yesu ameweza kuingia katika maisha ya waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kristo Yesu, aliwaagiza wafunzi wake kwenda kuwafanya mataifa yote kuwa ni wanafunzi wake kwa kuwabatiza na wale watakao amini watazamishwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Haya ni maji yaliyobarikiwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima. Ubatizo unamwezesha mwamini kuzaliwa kutoka juu kwa njia ya Roho Mtakatifu na kwamba, Mwenyezi Mungu amependa kuwaokoa waja wake si kwa sababu ya matendo yao ya haki waliyotenda, bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa na kuzaliwa mara ya pili na hivyo kufanywa upya na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema, Ubatizo ni alama muhimu sana ya maisha mapya, yanayowawezesha waamini kutembea katika upya wa maisha. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wamebatizwa katika kifo cha Kristo, na kuzikwa pamoja na Kristo, ili kufufuka pamoja naye kwa njia ya utukufu wa Baba, ili kuenenda katika upya wa uzima. Kwa njia ya Ubatizo, Wakristo wanafanywa kuwa ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na kufanywa kuwa ni washiriki wa utume wake. Upya wa uzima kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo unabubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye ni mzabibu wa kweli na waamini ni matawi yake na wale wanaokaa ndani yake huzaa sana.

Haya ni maisha yanayounganishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivyo kuwafanya kuwa Mwili mmoja, kwa kuimarishwa katika Ukristo kwa njia ya mafuta matakatifu sanjari na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu. Sakramenti ya Ubatizo inawawezesha waamini kuungana na Kristo Yesu na hivyo kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kila mtu kadiri ya hali yake, ili kuleta mageuzi ulimwenguni. Baba Mtakatifu anakazia pia umuhimu wa safari ya ukatekumeni inayowapatia watu wazima nafasi ya kufahamu mambo msingi ya imani.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, tangu mwanzo kabisa wa Kanisa, watoto wamekuwa wakipewa Sakramenti ya Ubatizo ndani ya Kanisa, kwani Kanisa lina amini na kufundisha kwamba, Roho Mtakatifu atasaidia kukuza na kuimarisha fadhila za Kikristo. Hakuna mtu mwenye haki ya kubatizwa, kwani Ubatizo ni zawadi kwa watu wote; zawadi ambayo inaweza kuzaa matunda katika udongo mzuri. Katika Mkesha wa Sherehe ya Pasaka, waamini wanapata tena fursa ya kurudia ahadi zao za Ubatizo, ili kuendelea “Kukrisitishwa”, yaani kufanywa kadiri ya Kristo Yesu na hivyo kuwa ni Kristo mwingine! Kamwe, Wakristo wasisahau kusherehekea Siku yao ya Ubatizo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.