2018-04-11 14:52:00

Papa Francisko kuzindua Mwezi wa Rozari Takatifu, "Divino Amore"


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake!Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya jirani wenye shida na mahangaiko mbali mbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa Rozari Takatifu katika maisha na utume wa waamini sanjari na kutaka kukuza na kudumisha Ibada hii kama kikolezo cha njia za utakatifu wa maisha, hapo tarehe Mosi, Mei, 2018, atatembelea Madhabahu ya “Divino Amore” yaliyoko Jimbo kuu la Roma, majira ya saa 11:00 ili kufungua Mwezi wa Rozari Takatifu! Atashiriki na waamini kusali Rozari Takatifu, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari!

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 5 Mei 2018 atashiriki katika mkutano wa sala na Jumuiya ya Ukatekumeni Mpya, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Jimbo kuu la Roma. Chama hiki cha kitume kimekuwa na mafanikio makubwa kiasi kwamba, hata idadi ya waamini wanaoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa imeongezeka maradufu. Kwa njia ya ushuhuda wa imani, waamini wameweza kukabiliana na changamoto za maisha; wamesaidiwa kuimarisha miito yao ndani ya Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu waliyokabidhiwa na Mama Kanisa. Anasema, Jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko wa kimisionari. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume huu inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia nguvu ya kuwa kweli ni wamisionari wanaotoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Waamini walei wanahamasishwa kuwa kweli ni wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; ushuhuda wenye mvuto na mashiko; chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Waamini walei wawe mstari wa mbele katika kutangaza na kushuhudia Injili; wawe wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ili kuruhusu mbegu ya Neno la Mungu iweze kuingia na kuzama katika akili na nyoyo zao! Hapa kinachohitajika ni ushuhuda na wala si wongofu wa shuruti! Kanisa linaweza kukua na kukomaa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si kwa njia ya shuruti kama ambavyo aliwahi kusema, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika huduma makini kwa maskini wa kiroho na kimwili.

Katika safari ya maisha ya kiroho, kuna nyakati ambazo waamini wanaweza kupata mtikisiko katika maisha na imani yao, lakini wakimtegemea Mwenyezi Mungu wanaweza kuibuka kidedea na kuwa na ujasiri wa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Pale waamini wanapokabiliwa na changamoto za maisha na imani, wawe na ujasiri wa kuomba msaada na ushauri kutoka kwa jirani zao. Wakristo ndio waliopewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo na wala si malaika, kwani wao dhamana na wajibu wao ni kumsifu, kumtukuza na kumwabudu Mwenyezi Mungu! Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanachama wa chama cha kitume cha Ukatekumeni mpya kuwasaidia na kuwaendeleza watoto wao katika  maisha ya kiroho na utu wema, kwani wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa la Kristo! Wajitahidi kuwafunda ili hatimaye, waweze kuwa ni wakristo watakatifu na raia wema zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.