2018-04-10 10:19:00

Watawa wanawake ni mashuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa


Mama Callista Gingrich, Balozi wa Marekani mjini Vatican anasema, watawa wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia wamekuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, majanga asilia na maafa mbali mbali. Hivi karibuni, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Jasiri kwa mwaka 2018, iliyoadhimishwa hapo tarehe 23 Machi 2018, Serikali ya Marekani imewatunuku wanawake kumi ambao wamejipambanua kwa ujasiri na ushupavu wao katika kuragibisha: haki, amani, utu na heshima ya binadamu na hata wakati mwingine, wakihatarisha usalama wa maisha yao!

Kati ya watawa waliotunukiwa ni Sr. Maria Elena Berini, mwenye umri wa miaka 73, mtawa aliyezaliwa nchini Italia, lakini kwa muda wa miaka arobaini amekuwa akisadaka maisha yake kwa kuwahudumia watu walioathirika kwa vita, huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Ni mtawa aliyebaki nchini humo hata pale Mashirika ya Misaada ya Kimataifa yalipoamua kuwaondoa wafanyakazi wao kwa kuhofia usalama wa maisha yao, lakini kwa ujasiri na ushuhuda wa imani, Sr. Maria Elena Berini, akabaki kati pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Aliwahi kupigwa risasi mguuni, akawaficha watawa wengine msituni, lakini akabaki kwenye Konventi, kuwahudumia wagonjwa na maskini waliokuwa wanateseka! Ni mtawa ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, kiasi kwamba, amekuwa kweli ni shuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Kuna watawa kama Sr. Maria Elena Berini wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wanaoathirika na vita huko Sudan ya Kusini, Siria na sehemu mbali mbali za dunia; mahali ambapo hata pengine, Serikali zimeshindwa kuwafikia wananchi wao, lakini watawa hawa wapo kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Mwaka 2017 Sr. Carol Tahhan kutoka Siria alitunukiwa zawadi ya ushupavu na ujasiri kwa kutoa huduma kwa watu walioathirika na vita nchini Siria! Akafanikiwa kuwajengea vijana matumaini kwa kuwafundisha kazi za mikono na hivyo kuwapatia ajira, wanawake waliokuwa wamekata tamaa ya maisha! Ni shuhuda wa uekumene wa huduma usiobagua wala kuchagua mtu kwa misingi ya dini, dhehebu au chama chake cha kisiasa! Sr. Carol Tahhan anaona ile sura na mfano wa Mungu kwa watu wote wanaoteseka. Watawa wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo sehemu mbali mbali za dunia. Kipindi hiki cha Pasaka ni wakati muafaka wa kutambua na kusherehekea ujasiri wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa!

Hawa ni mashuhuda wa Injili ya upendo ambao mara nyingi anasema Balozi Callista Gingrich kazi na utume wao hauonekani. Ni kutokana na changamoto hii, Ubalozi wa Marekani mjini Vatican kwa kushirikiana na Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Italia, Jumatano, tarehe 11 Aprili 2018 wanafanya Kongamano la Kimataifa kuhusu: Utume wa Watawa Wakatoliki katika maeneo tete na hatarishi sehemu mbali mbali za dunia! Kongamano hili linahudhuriwa pia na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Huu ni mwanzo wa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Marekani na Vatican katika kuenzi mchango unaotolewa na watawa katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.