2018-04-10 15:42:00

Papa: Wosia wa kitume: Furahini na kushangalia, wito wa utakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) uliozinduliwa rasmi Jumatatu, tarehe 9 Aprili 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu anakazia kuhusu mwaliko wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli.

Kristo Yesu anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu kila mtu kadiri ya hali na wito wake; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4).

Askofu mkuu Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, akiwasilisha Wosia huu mbele ya waandishi wa Habari mjini Vatican amekazia umuhimu wa utakatifu wa maisha kama changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo, kwani utakatifu kama anavyosema Papa Francisko ni chemchemi ya furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Utakatifu ni hija ya mapambano dhidi ya dhambi kwa kuendelea kupyaisha ile neema ya utakaso ambayo waamini wameipokea katika Sakramenti ya Ubatizo! Utakatifu unawawezesha waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wanaitwa kuwa watakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na ni kiini na utimilifu wa utakatifu wenyewe. Utakatifu ni changamoto inayopaswa kupaliliwa kila kukicha na kamwe haitoshi kuwa Mkristo na mwamini kuanza kubweteka, bali daima ajitahidi kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanapozungumzia kuhusu Fumbo la Kanisa wanakazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Wanasema waamini kwa kuimarika na misaada mingi ya wokovu namna hii na ya ajabu, waamini wote wa kila hali na hadhi wanaitwa na Kristo Yesu kila mmoja kwa njia yake, kwenye ukamilifu wa utakatifu kama Mwenyezi Mungu alivyo mtakatifu! Baba Mtakatifu Francisko anakazia pamoja na mambo mengine, mapambano ya maisha ya kiroho, kukesha na kusali pamoja na kufanya mang’amuzi ya maisha.

Askofu mkuu Angelo De Donatis anasema, utakatifu unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku kwa kujikita katika huduma ya upendo hata kama mwamini anaelemewa kwa kiasi kikubwa na dhambi pamoja na udhaifu wa moyo! Lakini neema ya Mungu inaweza kuleta mabadiliko ya kweli kwani watakatifu ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu! Ni watu waliopambana na ubinafsi pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu, leo hii ni marafiki wapendwa wa Mungu, wandani katika hija ya imani, matumaini na mapendo. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu inayowajalia waamini kusikiliza Neno la Mungu, kushiriki Sakramenti za Kanisa; kusimika maisha yao katika kanuni maadili na utu wema pamoja na kuonja shuhuda za watakatifu mbali mbali.

Changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ni utakatifu wa Jumuiya ya waamini, dhamana na utume ambao unapaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu: kwa kukubali mahusiano na mafungamano mapya yanayoletwa na Kristo Yesu; kwa kuondokana na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko; kwa kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikiana na wengine; kwa kumwilisha imani katika matendo; vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wajitahidi kuwa wamisionari katika hali na mazingira yao! Waamini wajifunze kuteseka na kufurahi pamoja na jirani zao ili kujenga umoja, udugu na mshikamano wa dhati!

Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu kwa kuishi kiaminifu kweli za Kiinjili! Mambo yote haya ni kielelezo cha mapambano ya maisha ya kiroho, yanayohitaji kufanyiwa mang’amuzi ya kina, ili kusonga mbele katika hija ya utakatifu wa maisha! Ni mwaliko wa kukumbatia neema ya Mungu, ili aweze kuwakoa waja wake kutoka katika vishawishi na mitego ya shetani na Ibilisi. Waamini wawe wepesi kusoma alama za nyakati, kuchunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu na kukimbilia huruma na upendo wake, pale wanapoelemewa na dhambi pamoja na udhaifu wa moyo!

Kwa upande wake Paola Bignardi, mwamini mlei na Rais mstaafu wa Chama cha Vijana Wakatoliki nchini Italia anakaza kusema, Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” ni mwaliko kwa waamini wa kawaida kuhakikisha kwamba, wanamwilisha Injili ya upendo na huruma katika maisha yao ya kila siku! Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji! Wajizatiti katika kutekeleza Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa waja wake!

Wasimame kidete kulinda, kudumisha na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Wawe ni vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu! Wawe na ujasiri wa kuthubu kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwani ni jambo linalowezekana kabisa! Kwa hakika utakatifu wa maisha ni chemchemi ya furaha ya kweli.

Bwana Gianni Valente, Mwandishi wa habari, anasema changamoto kubwa inayotolewa na Mama Kanisa mintarafu hatua mbali mbali za ufunuo kadiri ya Maandiko Matakatifu ni kuendelea kuwa na matumaini, kwani Mwenyezi Mungu anaendelea kuwatunza binadamu kwa kutoa uzima wa milele kwa wote wanaotafuta wokovu, wakidumu katika kutenda mema. Huu ni mwaliko wa kutumia vyema neema ya Mungu katika kujitafutia utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika unyenyekevu wa moyo!

Ukanimungu na baadhi ya watu kutaka kujifanya miungu watu ili waweze kuabudiwa ni kati ya vikwazo vikubwa katika ulimwengu mamboleo. Hawa ni watu wanaojiamini kupita kiasi, kwa kudhani kwamba, wanazo funguo za maisha ya uzima wa milele. Kuna baadhi ya waamini wanadhani kwamba, wao wamekwisha kuokoka na kuwa watakatifu kwa vile tu: ni Wakristo, Wakleri au Watawa na kusahau kwamba, utakatifu ni mapambano ya maisha katika hali ya unyenyekevu kwa kuambata: huruma na neema ya Mungu! Kumbe, utakatifu ni mwaliko kwa watu wote pasi na ubaguzi, ni changamoto ya kujikita katika ukamilifu kama Mwenyezi Mungu alivyomkalifu na mtakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.