2018-04-10 15:03:00

Papa Francisko: Wamisionari mwinueni Kristo Yesu, nguvu ya umoja!


Baada ya Ufufuko wa Kristo Yesu, Jumuiya ya kwanza ya Wakristo wakiwa wameungana na Mitume walitoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwamba, kwa hakika Kristo Yesu alikuwa amefufuka kwa wafu, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Huu ukawa ni mwanzo wa upyaisho wa maisha binafsi na maisha ya Kijumuiya, kama ilivyokuwa kwa Wamisionari wa huruma ya Mungu mara baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni huduma na utume mwenye mwelekeo kwa watu binafsi, ili waweze kuzaliwa tena kutoka juu na huduma kwa Jumuiya ili iweze kuishi furaha ya kweli kwa kumwilisha Amri ya upendo katika maisha yake!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne, tarehe 10 Aprili 2018 wakati alipokuwa anaadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Wamisionari wa huruma ya Mungu. Amewataka Wamisionari wa huruma ya Mungu kufahamu maana ya kuzaliwa kutoka juu, kwa maji na Roho Mtakatifu.

Hapa kinachozungumziwa ni neema na huruma ya Mungu kwa wale wanaojisikia kuwa kweli ni wanyenyekevu mbele ya Mungu; watu wanaojitambua kwamba, ni wagonjwa na wanamhitaji Kristo Yesu. Hawa ni wale wanaotambua na kukiri imani yao katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawataka Wamisionari wa huruma ya Mungu kuwa wanyenyekevu, watu wa kawaida, tayari kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda na kuwaongoza.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wamisionari wa huruma ya Mungu wanatumwa kutekeleza dhamana na wajibu wao katika Jumuiya, wakiwa na uwezo wa kumwinua Kristo Yesu, katika jangwa la dunia kama chemchemi ya wokovu! Msalaba wa Yesu uwe ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani; mchakato wa upyaisho wa maisha ya kijumuiya kama inavyopaswa kuwa hata kwa ulimwengu katika ujumla wake. Fumbo la Pasaka ni nguvu inayojenga umoja wa Kanisa na kwa njia ya Kanisa binadamu wote.

Ni nguvu ambayo imeshuhudiwa tangu Yerusalemu, kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo kuwa na moyo mmoja na roho moja! Umoja huu uliwawezesha kushirikiana na kushikamana, kielelezo na ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka. Kwa njia hii, Kanisa likafanikiwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote na wala hapakuwa na mtu hata mmoja aliyetengwa! Hii ndiyo dhamana na wajibu wa Wamisionari wa huruma ya Mungu, mashuhuda wa huruma ya Mungu ambayo inazima kiu ya watu wengi duniani na kwamba, umoja una nguvu kubwa kushinda kinzani na migogoro. Bila huruma ya Mungu kanuni hii haina nguvu na kamwe haiwezi kumwilishwa katika maisha na historia. Baba Mtakatifu ameonesha shukrani na furaha yake kwa Wamisionari wa huruma ya Mungu ambao ameridhia kwamba, waendelee kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ili kutekeleza dhamana hii kwa uaminifu zaidi, wanapaswa kuzaliwa kutoka juu, tayari kumwinua Kristo Yesu, ili Jumuiya ya waamini iweze kuwa kweli ni alama na chombo cha umoja kati ya walimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.