2018-04-09 14:50:00

Sinodi ya Amazonia: Njia mpya ya Kanisa kwa ajili ya ekolojia endelevu


Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 iongozwe na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia endelevu”. Baba Mtakatifu amewateuwa pia wajumbe washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia watakaoshirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi hii. Kati yao ni Kardinali Claudio Hummes, Rais wa Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM); Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Idadi ya viongozi 18 wa Kanisa kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, Maaskofu kutoka Amerika ya Kusini inakamilishwa na uteuzi wa Sr.  Maria Irene Lopez Dos Santos, Mwakilishi wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Amerika ya Kusini na Caribbean, CLAR. Huyu ni mtawa pekee wa kike aliyetuliwa kuwakilisha sauti ya wanawake Ukanda wa Amazonia.

Maandalizi ya nyaraka mbali mbali yatapata chimbuko lake katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia na kwamba, waamini walei ndio wanaoguswa na kuathirika zaidi kutokana na changamoto za kimissionari, kijamii na kiutu huko Amazonia, kumbe, wanategemewa sana na Mama Kanisa kwamba, watashirikisha uzoefu na mang’amuzi yao kutoka katika medani mbali mbali za maisha, ili kuweza kufanikisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia.

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita katika masuala ya haki, amani na mshikamano; utume na huduma ya upendo, ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inatamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia, ili Kanisa liweze kupata sura mpya ya watu wa Amazonia kwa kuwa na: wakleri pamoja na watawa wake! Hii ni changamoto inayohitaji ari, ujasiri na moyo wa kuthubutu, kwani kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na ukoloni mamboleo, unaofumbatwa katika nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayotishia: ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Amazonia. Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia inapania pamoja na mambo mengine; kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na kitume kwenye Ukanda wa Amazonia. Kwa kukabiliana kwa dhati kabisa na uhaba mkubwa wa mihimili ya uinjilishaji wa kina, hali inayowafanya waamini wa Amazonia kukosa huduma makini na endelevu za kichungaji, kiasi hata cha kujisikia kwamba, wametelekezwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anawapongeza wamisionari wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Amazonia, dhamana ambayo wanaitekeleza kama ushuhuda kwa Injili ya furaha na matumaini. Kristo Yesu alijimwilisha katika tamaduni za Kiyahudi, chachu mpya ya utambulisho wa mtu. Utamadunisho ni mchakato unaolitajirisha Kanisa na kwamba, Kanisa linataka kuwajengea watu uwezo wa kupambana na changamoto za maisha, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na sura ya Amazonia inayofumbatwa na uwepo wa watu mahalia.

Hiki ndicho kiini cha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia itakayoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2019 kwa kuongozwa kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia endelevu”. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii, kimaumbile na mang’amuzi ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa linapenda kukazia Injili ya upendo na mshikamano unaowashirikisha wananchi mahalia katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati yake.

Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha pekee katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, sera na mikakati isiyozingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini; kwa kujikita katika mchakato mzima wa uinjilishaji kwa kufunda mihimili mikuu ya uinjilishaji na utamadunisho ili kweli Injili iweze kugusa, kuganga na kutakasa maisha ya watu mahalia, ili nao waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini na huruma ya Mungu kwa waja wake!

Amazonia inashuhudia utajiri mkubwa wa kibayolojia, kitamaduni, maisha ya kiroho na hekima itakayowawezesha watu wengi zaidi, kusimama kidete, kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwani hapa, ni mahali patakatifu: chemchemi ya uhai, ambapo panawawezesha watu kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani! Uwepo wa wananchi wa Amazonia kuliko wakati mwingine wowote ule katika historia yao, uko hatarini, kwani, kwa sasa wanatishiwa zaidi na nguvu za kiuchumi: zinazotafuta kuchimba mafuta, gesi asilia na madini. Kuna sera na mikakati ya kilimo cha mashamba makubwa zisizotoa kipaumbele cha kwanza: kwa utu na heshima ya binadamu, kiasi kwamba,  watu wananyanyaswa na kudhulumiwa sana. Rasilimali na utajiri asilia uliomo ndani ya misitu hii hauna tija wala mafao makubwa kwa wananchi asilia na matokeo yake, vijana wa kizazi kipya wanakimbia ili kutafuta maisha bora zaidi ugenini.

Umefika wakati wa kuzingatia na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: mahitaji halisi ya wananchi wa Amazonia badala ya utajiri wa eneo hili, kuyanufaisha mataifa tajiri na makampuni makubwa makubwa ya kigeni! Mwanadamu akumbuke kwamba, amepewa dhamana ya kulinda na kutunza mazingira na  Mwenyezi Mungu na wala si mmiliki wa kazi ya uumbaji. Kumbe, mtindo wa maisha na hekima ya watu mahalia iwasaidie watu wa Mataifa kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Amazonia. Ili kuweza kufikia sera na mikakati ya maendeleo endelevu kuna haja kwa Serikali na taasisi kuwaheshimu na kuwathamini wananchi mahalia; kwa kujenga na kudumisha majadiliano na watu mahalia sanjari na kuzingatia: tamaduni, lugha, mapokeo, haki na amana ya maisha ya kiroho.

Kanisa linataka kuwashirikisha Wananchi mahalia kwenye majadiliano yanayogusa kwa karibu zaidi maisha yao, ili kuondokana na tabia ya ubaguzi pamoja na wananchi hao kutengwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna “cheche za matumaini” zinazozijengea uwezo Jumuiya mahalia ili kusimama kidete: kulinda na kutunza misitu na faida ya mazao yake, inawanufaisha wananchi mahalia kwa kuboresha hali ya maisha yao, kwa kuwapatia wananchi huduma bora zaidi ya elimu na afya ili kupambana vyema na mazingira yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.