2018-04-09 08:36:00

Injili ya Ufufuko inatangazwa katika Golgota ya ukosefu wa haki jamii


Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika Ujumbe wake wa Pasaka ya Mwaka 2018 ambayo kwa Makanisa ya Mashariki imeadhimishwa, Jumapili tarehe 8 Aprili anasema, Injili ya ufufuko wa Kristo inatangazwa kwa walimwengu wanaoogelea katika ukosefu wa misingi ya haki jamii; heshima na haki msingi za binadamu vinadhalilishwa. Dunia imegeuka kuwa ni Mlima wa Kalvari ambapo kuna mamilioni ya wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka kwa kukosa hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, lakini waathirika wakuu ni watoto. Anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya Fumbo la Msalaba na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Mama Kanisa anatangaza Injili ya matumaini na unyenyekevu dhidi ya baadhi ya watu ambao wamejigeuza na kutaka kuabudiwa kama miungu watu. Hii ni Injili ya mshikamano na upendo dhidi ubinafsi, raha na starehe kupita kiasi! Ni Injili inayosimikwa katika utu na heshima ya binadamu dhidi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, yanayotishia utu, usalama na maisha ya binadamu wengi! Patriaki Bartholomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, Fumbo la Pasaka ni ushindi dhidi ya utamaduni wa kifo; ni kiini cha imani, liturujia, kanuni maadili na utamaduni wa familia ya Mungu katika Kanisa la Kiorthodox linalolishwa na kurutubishwa kwa imani inayobubujika kutoka katika Ufufuko wa Kristo Yesu. Huu ni ushuhuda wa imani katika maisha ya uzima wa milele, ambapo, waamini wataweza kupata utimilifu wa maisha yao!

Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, kila Jumapili, ni kumbu kumbu endelevu ya ushindi wa Kristo dhidi ya kifo na hivyo, ni chemchemi ya furaha ya maisha mapya katika Kristo Mfufuka na njia ya kuelekea katika Ufalme wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka! Huu ni mwaliko kwa waamini kujizatiti zaidi katika kupambana na ukosefu wa haki jamii, kwa kutenda mema kwa maskini na wahitaji zaidi, daima wakijibidisha kuishi kadiri ya kweli za Kiinjili, pamoja na kanuni maadili yanayobubujika katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha ufunuo wa upendo na maisha mapya kutoka kwa Kristo Yesu.

Maisha ya Liturujia ya Kanisa la Kiorthodox yanafumbatwa katika uelewa wa wokovu wa wote, uhuru kamili wa watoto wa Mungu pamoja na mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Ushindi wa Kristo Mfufuka uwe ni chachu ya maisha mapya kwa walimwengu pamoja na kukuza jitihada za kulinda mazingira ambayo kimsingi ni sehemu ya kazi ya uumbaji! Kristo Mfufuka, amewatakasa waja wake na kuwakirimia uhuru wa wana wa Mungu kwa njia ya upendo wake usiokuwa na kifani! Injili ya ufufuko ni Habari Njema kwa watu wote kwani Kristo Yesu amevunjilia mbali nguvu ya dhambi, kifo na mauti, changamoyo kwa waamini kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki jamii, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kwa kutambua kwamba, baada ya Ijumaa kuu, kuna Pasaka ya Bwana na kwamba, mateso hayana neno la mwisho katika mustakabali wa maisha ya binadamu! Njia ya Msalaba ni hija ya maisha ya kiroho kuelekea katika ushindi na ufufuko kutoka kwa wafu! Mwenyezi Mungu amewakomboa walimwengu kwa njia ya Fumbo la Msalaba linaloonesha huruma, upendo, msamaha na upatanisho wa kweli kati ya Mungu na mwanadamu!

Fumbo la Msalaba ling’oe ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na madaraka! Injili ya Pasaka iwanyenyekeshe wale wote wanaojikweza na kutaka kuabudiwa kama miungu watu; irejeshe tena utu na heshima ya binadamu dhidi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayotishia maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Kashfa ya Fumbo la Msalaba isaidie kuunganisha mbingu na dunia na kuamsha tena ari na shauku ya kutaka kuambata maisha ya uzima wa milele. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka kwa wafu! Patriaki Bartholomeo wa kwanza anahitimisha Ujumbe wake wa Pasaka ya Mwaka 2018 kwa kuwataka waamini kumwomba Kristo Yesu: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, aangaze akili na nyoyo zao, aongoze hatua za miguu yao katika matendo mema pamoja na kuwaimarisha waja wake kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo hadi miisho ya dunia, kwa sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.