2018-04-09 08:56:00

Fumbo la Pasaka ni fursa ya kushuhudia mshikamano wa upendo na udugu


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika ujumbe wake wa Pasaka ya Mwaka 2018 anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki katika safari ya imani, matumaini na mapendo pamoja na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Kadiri ya Caritas Internationalis “dhana ya wahamiaji” inachukua mwelekeo mpana zaidi kwani hawa wanaweza kuwa ni wakimbizi, watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Caritas Internationalis katika kampeni zake inatumia neno “wakimbizi” katika ujumla wake, ikiwalenga wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Inawezekana hawa wakawa ni watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe, kutokana na sababu mbali mbali kama vile: vita, majanga asilia, kinzani na migogoro mbali mbali. Hawa wanaweza pia kuwa ni watu wanaotafuta kazi na maisha bora zaidi ugenini; watoto au watu wazima wanaojikuta wakiwa ugenini bila au pamoja na familia zao. Pengine ni watu waliotumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na utumwa mamboleo! Kristo Yesu katika maisha yake hapa duniani, hata kabla ya kuzaliwa alifunga safari kutoka Nazareth hadi Bethlehemu; akiwa mtoto mchanga, akapelekwa uhamishoni Misri kama mkimbizi. Kwa muda wa miaka mitatu, akasafiri sehemu mbali mbali za Galilaya, akitangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu na hatima ya safari yake ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu kama ilivyoandikwa.

Fumbo la Pasaka linaloadhimishwa na Kanisa katika kipindi hiki ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuondoa “vizingiti vya mawe” vinavyosonga nyoyo zao na kusumbua mwono na mwelekeo wao wa maisha, tayari kushiriki katika safari. “Share the journey”.  Baba Mtakatifu Francisko, mwezi Septemba 2017 alizindua Kampeni ya Kimataifa ya Ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi inayoratibiwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis inayoongozwa na kauli mbiu “Share the journey” yaani “Shiriki safari”. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha wema na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali ya misaada ya Kanisa Katoliki sanjari na vyama vya kiraia vinavyojielekeza katika huduma ya upendo kwa wahamiaji na wakimbizi. Hii ni kampeni ya umoja na mshikamano na wale wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi pamoja na wenyeji wanaowaendea kwa unyenyekevu, ili waweze kuonja wema na ukarimu wao; kwa kuwaelewa na kuthamini tamaduni, lugha na desturi zao njema.

Kardinali Luis Antonio Tagle, anasema, baada ya Ufufuko, Kristo Yesu aliwatokea wanafunzi wa Emau waliokuwa wamegubikwa na mashaka pamoja na majonzi makubwa kufuatia: mateso na kifo cha Kristo Yesu, Msalabani. Wanafunzi wa Emau hawakumtambua Yesu hadi pale alipobariki na kuumega mkate, hapo ndipo macho yao yalipofunguka na kumtambua Kristo Yesu kati yao! Je, ni mara ngapi waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wamemtambua Kristo Mfufuka kati ya wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi? Pengine, waamini wameendelea kujifungia katika makaburi yao kwa hofu na mashaka pamoja na uelewa finyu kuhusu mateso na mahangaiko ya wakimbizi hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia?

Pasaka ni wakati wa kurejea tena na tena katika misingi ya imani, matumaini na mapendo; ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuganga na kuponya; kujenga na kuimarisha upendo na mshikamano; kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya wengine kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu mwenyewe katika maisha na utume wake kiasi hata cha kusadaka maisha, ili kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni! Waamini wanaalikwa kumwona na kumtambua Kristo Yesu, kati ya wakimbizi na wahamiaji. Caritas Internationalis linasema, kuanzia tarehe 17-24 Juni 2018 kutafanyika kampeni ya kimataifa kwa vitendo ili kushiriki safari kwa kushirikiana na Caritas Internationalis pamoja na Mashirika mbali mbali ya Misaada ya Kanisa Katoliki, ili kutoa mwaliko wa chakula kwa wahamiaji kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau kwa Yesu, kama tendo linalo kumbusha umoja wa familia ya Mungu na kwamba, wote wanategemeana na kukamilishana.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Caritas Internationalis anahitimisha ujumbe wake wa Pasaka kwa kuonesha matumaini kwamba, matendo haya yanayoweza kuonekana kuwa ni madogo lakini ni muhimu sana katika mchakato wa uelewa na ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano unaong’oa vizingiti vinavyotaka kukwamisha safari ya upendo na mshikamano kwa wahamiaji na wakimbizi, ili kwa pamoja kuweza kuwasha moto wa upendo wa Mungu hapa duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.