2018-04-07 10:27:00

Papa Francisko: wito wa utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Takatifu kwa maana Kristo, Mwana wa Mungu anayetangazwa pamoja na Baba na Roho Mtakatifu kwamba ni peke yake mtakatifu, amelipenda Kanisa kama Bibiarusi wake, akajitoa mwenyewe kwa ajili yake ili alitakatifuze, akaliunganisha naye kama mwili wake, akalijazia kipaji cha Roho Mtakatifu, kwa utukufu wa Mungu! Kumbe, watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa kuwa ni watakatifu! Haya ndiyo mapenzi ya Mungu. Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote!

Waamini wanahimizwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe na matunda ya Roho Mtakatifu ili wafanywe watakatifu. Kutokana na udhaifu wa binadamu, waamini wanahitaji mara kwa mara kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kudadavua kuhusu Fumbo la Kanisa kwa kusema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo!

Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu! Wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Waraka huu mpya unazinduliwa rasmi, Jumatatu, tarehe 9 Aprili 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha!

Watakatifu walikuwa na mapungufu na dhambi zao binafsi, lakini wakathubutu kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Utakatifu ni hija ya maisha mbele ya Mwenyezi Mungu inayofumbatwa katika ujasiri, matumaini na uthubutu kwa kuamini kwamba, neema ya Mungu inaweza kuwaongoza kufikia hatima yake, yaani kuonana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujizatiti katika utakatifu wa maisha, hata wanapokuwa wagonjwa kitandani hawawezi kitu! Wanapokuwa kazini wakichakarika kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa uaminifu, uadilifu huku wakiwajibika barabara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Watakatifu ni mashuhuda na wandani wa matumaini na unyenyekevu wa moyo! Hawa ndio akina Mama Theresa wa Calcutta, Yohane Paulo II, Yohane XXIII na wengine wengi waliotangazwa na Papa Francisko katika kipindi cha miaka mitano ya utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Bila kuwasahau wenyeheri kama Paulo VI, aliyeonesha unyenyekevu na uvumilivu mkubwa katika maisha na utume wake. Utakatifu kadiri ya Papa Francisko ni mchakato wa kuwa marafiki wa Mungu na jirani kwa kujitosa bila ya kujibakiza hata kidogo!

Baba Mtakatifu Francisko kwa barua yake binafsi, “Motu Proprio” “Maiorem hac dilectionem” yaani “Kuhusu sadaka ya maisha” amefungua njia ya kutangazwa wenyeheri waamini ambao hali wakisukumwa na upendo, wamesadaka maisha yao kwa ajili ya jirani zao kwa kukubali na kupokea kifo kabla ya wakati kama njia ya kumfuasa Kristo Yesu kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. (Rej. 1Yoh. 3:16).

Kama inavyoeleweka kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki kwamba, mwamini anaweza kutangazwa kuwa Mwenyeheri kwa njia ya kifo dini, kielelezo cha pekee katika kumfuasa Kristo, lakini, ikumbukwe kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake ni upendo kwa Mungu na jirani. Kifodini kadiri ya ufahamu wa Kanisa ni kupokea kwa hiyari kifo kama kielelezo cha upendo kwa Kristo! Ni kupokea kifo kutokana na chuki za kiimani, au fadhila nyinginezo za Kikristo. Kifodini ni kielelezo cha unyenyekevu kwa mwamini anayesamehe kama njia ya kumuiga Kristo Yesu, ambaye alipokuwa pale juu Msalabani aliwaombea watesi wake msamaha kutoka kwa Baba yake wa mbinguni!

Njia ya pili inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri ni katika mchakato wa kumwilisha fadhila za kishujaa zinazotekelezwa kwa haraka, bila kusita na kwa moyo mkunjufu, kiasi cha kuonekana kuwa ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si tu nguvu za kibinadamu. Huu ni mwelekeo unaomwezesha mwamini kufikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili. Fadhila zinazozungumziwa hapa ni zile fadhila tatu za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo bila kusahau fadhila kuu nne yaani: Busara, Haki, Nguvu na Kiasi. Fadhila zote hizi zinafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika Mashauri ya Kiinjili, au Nadhiri kama zinavyojulikana na wengi: Ufukara, Utii, Usafi kamili na Unyenyekevu.

Njia ya tatu inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa Mwenyeheri, ambayo waamini wengi hawaifahamu sana, lakini imefafanuliwa katika Sheria, Kanuni na Tararibu za Kanisa katika Sheria za Mwaka 1917 inayojulikana kama kutangazwa Mwenyeheri kwa kutumia kanuni ya “Equipollente” ambayo kimsingi inatumika kwa nadra sana katika Kanisa kwa ajili ya kesi maalum. Hizi ni njia ambazo Mama Kanisa anazitumia kwa ajili ya kuwatangaza waamini wake kuwa wenyeheri na watakatifu, lakini kadiri ya historia inavyozidi kusonga mbele, njia hizi zinazonekana kana kwamba, zinawatenga baadhi ya waamini ambao wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa njia ya ushuhuda wa upendo wenye mvuto na mashiko! Yesu mwenyewe anasema, hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. (Rej. Yoh. 15:13).

Njia ya nne inayotolewa sasa na Baba Mtakatifu Francisko ni sadaka ya maisha ambayo pengine inafumbata baadhi ya mambo msingi yaliyokwisha kufafanuliwa katika hatua tatu zilizotangulia, inataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa ushuhuda wa Kikristo unaofumbatwa katika upendo, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwamini kama njia ya kutafuta ukamilifu wa maisha na hatimaye, utakatifu. Sadaka ya maisha inafumbwata kwa namna ya pekee katika fadhila ya : Imani, Matumaini, Busara pamoja na nguvu.

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake binafsi anazungumzia kifo kinachodumu kwa muda mfupi kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa upendo wa Kikristo. Kanisa litaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watumishi wa Mungu kutangazwa kuwa wenyeheri kwa njia ya: kifodini, ushuhuda wa fadhila za kishujaa; ushuhuda wa upendo wa hali ya juu kabisa unaofumbata kifo. Dhana hii ni matunda ya tafakari ya kina iliyotolewa na Papa Benedikto XV aliyekazia ushuhuda wa upendo kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake.

Kunako mwaka 2014, Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu kwa himizo na ushauri wa Baba Mtakatifu Francisko, wakaanza kuivalia njuga changamoto hii kwa kuwapatia kazi wataalam wa: Sayansi ya Biblia, Taalimungu; Tasaufi, Sheria na Historia ya Kanisa na kujadiliwa kunako mwaka 2016 na kufikia uamuzi kwamba, sadaka ya maisha ni kieleleazo cha ushuhuda wa hali ya juu kabisa wa kumfuasa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baada ya upembuzi yanakifu, Baba Mtakatifu ameridhia hoja hii na hivyo kuiandikia barua binafsi “Maiorem hac dilectionem” inayokazia kwa namna ya pekee kuhusu sadaka ya maisha ni njia halali ambayo kwayo mtumishi wa Mungu anaweza kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri.

Huu ni ushuhuda wa upendo unaofumbata sadaka ya maisha kwa kupokea kifo katika kipindi kifupi! Baadaye, kutahitajika muujiza ili kuendelea mbele na mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu, kadiri ya Sheria zinazoongoza hatua hizi kuanzia katika ngazi ya kijimbo hadi zinapofika mjini Vatican. Mkazo umewekwa kwenye Mwongozo “Sanctorum Mater” yaani “Kuhusu Mambo ya Utakatifu” uliochapishwa kunako tarehe 17 Mei 2007 ili kurahisisha Sheria zilizokuwa zimepitishwa kunako mwaka 1983 na sasa Baba Mtakatifu Francisko amerahisisha zaidi na baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano, inaanza kutumika rasmi ndani ya Kanisa.

Kwa barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko, Mafundisho kuhusu Utakatifu wa maisha ya Wakristo wanaoweza kutangazwa kadiri ya Mapokeo ya kuwa Watakatifu, mwelekeo huu pia umerutubishwa zaidi kwa kutoa mwanya kwa watumishi wa Mungu ambao wamemshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya sadaka ya maisha kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo, watatangazwa ili kupanua wigo wa ujenzi wa watu wa Mungu, ambamo ndani ya watakatifu na wenyeheri, Kanisa linaoiona Sura ya Kristo na uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika historia na mifano bora ya kuigwa katika mchakato mzima wa kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini!

Na Padre  Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.