2018-04-07 12:20:00

Askofu mkuu Filipo Iannone ateuliwa kuwa Rais wa Sheria za Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Francesco Coccopalmerio la kung’atuka kutoka madarakani kadiri ya sheria za Kanisa, baada ya kutimiza umri wa kustaafu. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu mkuu Filipo Iannone kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Tafsiri ya Sheria kanuni za Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Filipo Iannone alizaliwa tarehe 13 Desemba 1957 huko Napoli, Kusini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi na kitawa, tarehe 26 Juni 1982 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Tarehe 12 Aprili 2001 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Napoli na hatimaye, kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 26 Mei 2001 na Kardinali Michele Giordano. Tarehe 19 Juni 2009 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sora-Aquino-Pontecorvo na kusimikwa rasmi tatehe 20 Septemba 2009. Tarehe 31 Januari 2012, Papa Mstaafu Benedikto XVI akamteuliwa kuwa Askofu msaidizi Jimbo kuu la Roma. Tarehe 11 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Kipapa la Tafsiri za Sheria za Kanisa. Na tarehe 7 Aprili 2018 akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Tafsiri ya Sheria kanuni za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.