2018-04-06 09:16:00

Shukrani sana Askofu mkuu Lebulu! Shikamaneni na Askofu mkuu Amani


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Yesu Kristo ni uso wa huruma ya Baba wa milele na kwamba, Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ya Mungu ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa njia ya maisha na utume wake, Kristo Yesu amewafunulia walimwengu huruma ya Mungu. Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati zote. Huruma ya Mungu ni daraja linalomuunganisha Mungu na binadamu na kuufungulia moyo wa binadamu mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya dhambi na mapungufu yanayo mwandama mwanadamu!

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo, aliamua kuipatia Jumapili hii, umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa ili kutoa nafasi kwa watu wa Mungu kutafakari huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujichotea nguvu na neema zinazobubujika kutoka katika huruma ya Mungu kwa njia ya  maadhimisho ya Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho inayowakirimia waamini: upya wa maisha, amani, utulivu wa ndani na furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao!

Huruma ya Mungu katika mwanga wa Pasaka ni kielelezo cha ufahamu ambao unaweza kuchukua mtindo mbali mbali katika maisha ya mwanadamu yaani: kwa kutumia milango ya fahamu, kwa kufundishwa, lakini kubwa zaidi ni kwa njia ya mang’amuzi ya huruma ya Mungu inayofungua akili na nyoyo za watu ili kuweza kufahamu kwa kina na mapana zaidi Fumbo la maisha ya Mungu na maisha ya mtu binafsi. Huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba: vita, chuki, uhasama na ubaya wa moyo ni mambo ambayo hayana msingi kabisa na kwamba, waathirika wakubwa ni wale watu wanaofungwa katika hali kama hizi, kwani ni mambo yanayowapokonya utu wao.

Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anaendelea kusema Baba Mtakatifu Francisko, inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kwa furaha.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu kwa mwaka 2018 yanachukua sura ya pekee sana Jimbo kuu la Arusha, Tanzania kwani Askofu mkuu mteule Isaac Amani Massawe anasimikwa rasmi kuwa kiongozi na mchungaji mkuu wa Jimbo kuu la Arusha.

Askofu Mkuu Ruwaichi anapenda kuchukua fursa hii kumpongeza Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu aliyezaliwa kunako tarehe 13 Juni 1943 huko Kisangara, Jimbo Katoliki la Same, Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikuhani, tarehe 11 Desemba 1968 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 12 Februari 1979 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Same na kuwekwa wakfu tarehe 24 Mei 1979. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Arusha kunako tarehe 28 Novemba 1998 na tarehe 16 Machi 1999 akateuliwwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha.

Katika maisha yake kama Padre amelitumikia Kanisa kwa miaka 49 na kama Askofu takribani miaka 39. Tarehe 27 Desemba 2017, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani. Askofu mkuu Ruwaichi anakiri kwamba, hiki ni kipindi kirefu chenye changamoto na madai makubwa. Ni kipindi ambacho Askofu mkuu Josaphat Louis Lebulu amekiishi kwa ukarimu na uthubutu mkubwa, alikuhudumia kwanza kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Same na baadaye kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha. Kwa nyakati mbali mbali ameshika nyajibu mbali mbali katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani AMECEA.

Askofu mkuu Ruwaichi anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi kubwa ya Askofu mkuu Lebulu aliyelihudumia Kanisa kwa ukarimu, weledi, bidii, juhudi na maarifa, daima akionesha furaha katika maisha na wito wake! Anapenda kumpongeza kwa utendaji wake mzuri wa kazi, kwa ustahilimivu wake katika magumu. Familia ya Mungu nchini Tanzania inamtakia kheri na baraka katika awamu ya pili ya maisha na utume wake kama askofu mstaafu. Ataendelea kuwa Askofu katika Kanisa. Ni matumaini ya watu wa Mungu nchini Tanzania kwamba, ataendelea kulitajirisha Kanisa la Mungu: kwa mafundisho; kwa uthabiti, kwa sala na sadaka yake ya maisha pamoja na utayari wa kuendelea kushirikiana na kushikamana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Kanisa mahalia katika ujumla wake.

Askofu mkuu Ruwaichi anamtakia kheri na baraka Askofu mkuu mteule Isaac Amani Massawe anapoanza ngwe mpya ya maisha, ufuasi na utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha. Ataendelea kutekeleza dhamana na utume wa Kristo Yesu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kumbe, ni wajibu wa familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha kujitosa ili kuendelea kulidumisha Kanisa la Kristo Yesu. Askofu mkuu mteule Isaac Amani Massawe, alizaliwa tarehe 10 Juni 1951 huko Mango, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 29 Juni 1975. Tarehe 21 Novemba 2007 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi na kuwekwa wakfu tarehe 22 Februari 2008 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akisaidiana na Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha pamoja na Hayati Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi. Hivi karibuni, aliteuliwa pia kuwa ni Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Mbulu.

Kwa ufupi, Askofu mkuu mteule Isaac Amani Massawe alisoma shule ya msingi Mango, Kibosho; Seminari ndogo ya St. James, Moshi; Falsafa kati ya mwaka 1970 – 1972, Seminari kuu ya Ntungamo, Jimbo Katoliki Bukoba. Alijipatia masomo ya Taalimungu Seminari kuu ya  Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora kati ya mwaka 1972 – 1975 na hatimaye, kupadrishwa mwezi Juni 1975. Kama Padre aliwahi kuwa Paroko usu, mwalimu na mlezi wa Seminari ndogo ya St. James, Moshi. Kati ya Mwaka 1986 hadi mwaka 1989 alikuwa masomoni, Chuo kikuu cha Walsh, nchini Marekani; kati ya mwaka 1990 hadi mwaka 2003, mlezi wa watawa na baadaye akateuliwa kuwa ni Paroko wa Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi.

Askofu mkuu Ruwaichi aanamtakia kheri na baraka Askofu mkuu Massawe katika kuwalea: waamini walei, watawa na wakleri wa Jimbo kuu la Arusha. Mwaliko na himizo kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha ni kumshukuru Mungu kwa kumpata Askofu mkuu mpya katika kipindi cha muda mfupi. Kanisa linawaomba kushirikiana naye katika kuendeleza gurudumu la maisha, utume, ustawi, mafao na maendeleo ya wananchi wengi Jimboni Arusha na kwamba, hakuna muda wa kupoteza. Mwenyezi Mungu atatukuzwa na kupendezwa endapo watashikamana na mchungaji wao ili waweze kuwa kundi moja chini ya Mchungaji mmoja, Kristo Yesu! Askofu mkuu Isaac Amani Massawe amechagua maneno haya "Kuwajibika na kushirikiana katika Kristo" kuwa ni sehemu ya nembo yake ya Kiaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.