2018-04-06 06:30:00

Sherehe ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!


Utangulizi: “Dominika inayofuatia dominika ya Pasaka ninataka iadhimishwe Sherehe ya Huruma ya Mungu. Mwanangu, utangazie ulimwengu wote juu ya Huruma yangu isiyo na kikomo. Katika siku hiyo nitafungulia milango yote ya Huruma yangu na roho itakayopokea Maungamo na Ekaristi Takatifu siku hiyo itapata maondoleo ya dhambi pamoja na adhabu zake zote.”  Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News hayo ni maneno ya Yesu mwenyewe kwa Mtakatifu Sr. Faustina Kowalska kama yanavyopatikana katika shajara yake kuhusu Dominika ya Huruma ya Mungu ambayo kanisa linaiadhimisha siku ya leo. Ni dominika inayotukumbusha, kama anavyofundisha Papa Francisko, kuwa Huruma ndilo jina lingine la Mungu - “Bwana amejaa Huruma na Neema” (Zab. 103:8). Na katika kipindi hiki cha Pasaka tunapomshangilia Kristo Mfufuka tunaalikwa kuiona Huruma ya Mungu katikati ya fumbo la ukombozi wa Mwanadamu. Tumshukuru Mungu wa Huruma na tuendelee kuiitikia katika maisha yetu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Mdo. 4:32-35). Kitabu cha Matendo ya Mitume ni kitabu kinachoelezea namna ukristo ulivyoanza baada ya ufufuko wa Kristo. Na kama jina lake lilivyo, kinaelezea walichofanya mitume katika kuukuza na kuuimarisha kwa njia ya mahubiri harakati zote za uchungaji walizofanya wakiitikia agizo la Kristo mwenyewe “nendeni ulimwenguni kote mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu” (Mt. 20:18-20). Katika mwanzo huo, somo la leo linaonesha kuzaliwa kwa Jumuiya ya kwanza ya waamini. Jumuiya ya kwanza ya waamini inazaliwa kama mwitikio wa ongezeko la waamini. Pamoja na ongezeko hilo na bila shaka kutoka maeneo na hali tofauti tofauti, waliunganishwa Kristo, wakawa “moyo mmoja na roho moja”, wakiishi kijumuiya na kwa manufaa ya wanajumuiya wote. Nguvu ya imani kwa Kristo Mfufuka ni nguvu inayoweza kuwaweka watu pamoja. Na kwa umoja huu Mitume waliendelea kumhubiri Kristo kwa nguvu, na neema ikatawala kwa wote.

Somo la pili (1Yoh. 5:1-6). Waraka huu Yohane aliuandika kwa jumuiya ya Makanisa ya Asia Ndogo. Huko walikuwa wameibuka watu walioanza kuwapotosha wengine kwa mafundisho yao na Yohane anawaandikia kurekebisha hali hiyo. Katika sehemu ambayo ni somo letu la pili leo, Yohane anasisitiza juu ya mambo matatu: Mosi, panapaswa kuwa na uhusiano kati ya imani ambayo mtu anayo na maisha ambayo mtu huyo anayaishi. Hivi kwamba imani ya yule anayemwamwini Kristo ijioneshe katika uadilifu wa maisha yake.

Pili, namna (mojawapo) ya kuionesha imani na upendo kwa Kristo ni kuzishika amri za Mungu. Kusema kuwa mtu anamwamini Mungu na anampenda Kristo ilhali hazishiki amri zake ni kasoro.  Tatu, anawaalika kuushinda ulimwengu kutokana na nguvu ya imani waliyonayo. Ni vigumu kuushinda ulimwengu kwa kutumia namna za kiulimwengu. Imani aliyonayo mkristo inampa nguvu ya ndani ambayo ni nguvu ya kimungu, nguvu inayomwezesha mtu kuwa thabiti dhidi ya miyumbo inayoletwa na malimwengu.

Injili (Yoh. 20:19-31); ni injili inayoendele kutoa ushuhuda wa ufufuko wa Yesu. Ushuhuda ambao mwanzo ulitolewa na akinamama kwa kukuta kaburi wazi. Hii iliashiria kuwa Kristo hakubaki amefungwa na nguvu za mauti kaburini bali amefufuka kama alivyosema. Injili ya leo inatupatia ushuhuda mwingine, Yesu anawatokea mitume. Anaingia katika chumba ambacho walikuwa wamejifungia kwa hofu ya wayahudi anawaimarisha na kuwaondoa hofu, na tena anaondoa mashaka ya Tomas asiyeamini naye anamkiri Kristo mfufuka kuwa ni Bwana na Mungu. Ni hapa pia ambapo Kristo anaianzisha Sakramenti ya Kitubio iliyo pia Sakramenti ya Huruma ya Mungu. Anapowaambia mitume “wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” anawakabidhi utume ambao naye aliupokea kutoka kwa Baba, yaani “kutafuta na kuokoa kilichopotea (Lk. 19:10).

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunapoiangalia historia ya ukombozi wa mwanadamu na historia nzima ya mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu tunaona kuwa ni historia inayoifunua Huruma kubwa sana aliyonayo Mungu. Tena kuwekwa kwa sherehe hii dominika ya pili ya Pasaka ni ufunuo mwingine unaolithibitisha, kwa sababu sherehe hii huanza kwa novena siku ya Ijumaa Kuu, siku ambayo Kristo alijitoa sadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu na ni siku iliyo kilele cha Kristo kutwaa mwili na kuja ulimwenguni, “alikuja ili afe Msalabani”.

Tunaweza kusema kuwa Huruma hii ya Mungu ambayo imejifunua katika historia nzima tangu mwanzo ni huruma ambayo pia mwanadamu hakuwa ameipa kipaumbele hadi hapo Kristo alipoamua kujifunua tena alipomtokea Mt. Faustina, Mtawa Mpoland na kumpa maono juu ya kuieneza ibada ya Huruma ya Mungu.  Kutoka katika shajara ambayo Mt. Faustina alikuwa akiandika matokeo yote ya Yesu kwake tumepata kuifahamu ibada ya Huruma ya Mungu kwa njia mbalimbali: Nji ya Picha ya Yesu wa Huruma inayomwonesha Yesu akibariki na miale miwili ikitoka katika ubavu wake uliochomwa na chini imeandikwa Yesu Nakutumainia, ikimwalika mwanadamu kuitumainia daima Huruma kuu ya Mungu katika maisha yake. Njia ya Rosari ya Huruma inayomwalika mwanadamu kutakafakari Mateso makali ya Yesu aliyoyapata kwa ajili ya kumkomboa Mwanadamu na kumwalika kumtolea Baba kwa ajili ya dunia nzima. Njia ya Saa ya Huruma, yaani kujizamisha katika Huruma ya Mungu saa ya huruma kuu, saa 9 alasiri ambapo Kristo alidhihirisha upeo wa Huruma yake na kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Njia ya Sherehe ya Huruma ya Mungu tunayoadhimsha leo ambapo Kristo alitaka picha yake Ibarikiwe kwa ibada na waamini wapokee Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi wapate maondoleo ya dhambi na adhabu zake.

Katika sherehe ya leo tunayaona tena mahangaiko ya Yesu kama alivyojifunua kwa Mtakatifu Faustina “kwa nini watu wanapotea wakati huruma yangu ipo?”. Ni mwaliko wa kutambua kuwa Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko udhaifu wa Mwanadamu. Na yeyote anayeikimbilia kwa toba ya kweli na moyo wa kujibandua kutoa maisha ya upotovu daima ataikuta wazi milango ya Huruma na ataikuwa wazi mikono ya Baba mwenye Huruma tayari kumpokea na kumkaribisha ndani kama katika mfano wa Mwana Mpotevu (Lk. 15). Huruma inaita huruma, na mwitikio kwa huruma ni huruma. Tunapojifunza huruma hii kuu ya Mungu, tunaalikwa nasi kuwa vyombo vya huruma. Mwaka wa huruma tuliouadhimisha miaka miwili iliyopita umetuachia mwaliko huu “iweni wenye huruma kama Baba”. Nami katika maisha yangu binafsi, ninapoona uwingi wa huruma ambayo Mungu amenionea na akanijalia neema ninazohitaji nami pia nijifunze kuwa huruma kwa wenzangu.

Yesu Nakutumainia!

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS.
All the contents on this site are copyrighted ©.