2018-04-05 09:47:00

Wamisionari wa huruma ya Mungu wako mjini Vatican kujinoa zaidi!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa makini kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Hii ni tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na utu wema sanjari na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Kimsingi hili ndilo lililokuwa lengo kuu la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa.

Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba,  Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Hapa Mapadre wahubiri wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanaandaa mahubiri yao vyema na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayojikita katika: ukarimu, ushuhuda wa maisha, msukumo wa kichungaji, uwazi na utayari wa kutoa huduma ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Mapadre sasa wanaweza kuwaondolea watu dhambi ya utoaji mimba.

Uso wa huruma “Misericordia vultus” na “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” ni nyaraka zinazoweza kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini ukuu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto anasema Baba Mtakatifu ni kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kwa njia hii, Kanisa litaendelea kuwa kweli ni shuhuda wa huruma ya Mungu na utambulisho wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi kwa waamini kurejea katika mambo msingi ya imani, maisha ya kiroho, sala, tafakari na hija. Ijumaa ya huruma ya Mungu, imekuwa ni siku ya pekee ya kuweza kuonja shida, magumu na changamoto ya watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kielelezo cha Kanisa linalosikiliza kilio cha watu na kuwajibu kwa wakati muafaka!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” amewathibitisha Wamisionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuwaondolea waamini vikwazo na vizingiti vilivyokuwa vinawazuia kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya wongofu wa ndani, toba, msamaha na upatanisho. Mapadre kwa nguvu ya Sakramenti waliyoipokea sasa wameongezewa madaraka ya kuweza hata kusamehe dhambi ya utoaji mimba ambayo hapo awali ilikuwa imeachwa rasmi kwa Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lengo ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki.

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya limeandaa mkutano wa Wamisionari wa huruma ya Mungu, watakaoshiriki katika Ibada ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 8 Aprili 2018, saa 4:30 kwa saa za Ulaya, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hili ni kundi linaloundwa na wamisionari 550 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, na Padre Wojciech Adam Koscielniak, ndiye mmisionari pekee kutoka katika Kanisa la Tanzania. Wamisionari hawa wanakutana na Baba Mtakatifu, ikiwa imegota miaka miwili tangu alipoanzisha utume huu maalum kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. 

Kumbe, kuanzia tarehe 8-11 Aprili 2018 utakuwa ni muda wa katekesi, shuhuda na maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho. Kilele cha mkutano huu ni hapo tarehe 10 Aprili 2018 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Papa Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wawezeshaji wakuu katika mkutano wa wamisionari wa huruma ya Mungu ni viongozi wakuu kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Maaskofu wakuu walioalikwa kutoa mada mbali mbali. Kati ya mada hizi ni “Upatanisho: Ni Sakramenti ya huruma ya Mungu! Dhambi na huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Padre: Wamisionari wa huruma ya Mungu kadiri ya mtazamo wa Papa Francisko pamoja na Ushauri wa kichungaji kuhusu Sakramenti ya Upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.