2018-04-05 07:52:00

Vijana wa Bara la Afrika wanapembua mchakato wa Sinodi ya Vijana!


Baba Mtakatifu Francisko aliongoza adhimisho la Ekaristi Takatifu siku ya Jumapili ya matawi tarehe 25 Machi 2018 katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambako ulishiriki umati mkubwa wa watu, miongoni mwao vijana 300 waliokuwa katika utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana hapo mwezi Oktoba mwaka huu 2018. Mwishoni mwa adhimisho la Ekaristi takatifu, vijana 12 walimkabidhi Baba Mtakatifu Hati ya Utangulizi wa  majadiliano yao, yaliongozwa na kauli mbiu ‘’Vijana, Imani na mang’amuzi ya miito’’. Hati hii itakuwa ni sehemu ya mkusanyiko wa kutengeneza hati ya kutendea kazi (Instrumentum laboris) kwa ajili ya majadiliano wakati wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Miongoni mwa wahudhuriaji wa mkutano huo wa vijana uliofanyika mjini Roma walikuwemo wakatoliki na wasiowakatoliki kutoka nyanja mbalimbali za jamii na kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Walialikwa pia vijana kutoka seminari na nyumba za malezi ya kitawa wakishiriki katika mkutano huo. Walelewa hao walipata fursa ya kusikilizana na kujadiliana na vijana wenzao kutafakari juu ya masuala mbalimbali yanayowakumba vijana katika ulimwengu wa leo; imani, mitazamo, shughuli za maendeleo, uzoefu, hofu, changamoto na furaha za vijana wa leo. Kwa namna ya pekee, walelewa walionja mubashara kutoka katika vinywa vya vijana wenzao mitazamo mbalimbali ya vijana hao kuhusu Kanisa na uinjilishaji kwa ujumla. Haikuwa ngumu kwa walelewa kugundua ari ya vijana kutamani kushirikiana na Kanisa kama mdau muhimu na mwenzi wa safari katika kutimiza ndoto na matarajio yao ya baadae, bila kuacha nyuma tamanio la vijana wengi kujitambua na kutambuliwa kama watoto wa Mungu wenye hadhi inayopaswa kuheshimiwa na watu wote.

Itakumbukwa kwamba, mkutano huo wa vijana kwa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu ulitanguliwa na mkutano wa waseminaristi na mapadre wanafunzi kutoka katika taasisi na vyuo vikuu vya Kipapa vilivyoko mjini Roma mnamo tarehe 16 Machi 2018, ambako Baba Mtakatifu Francisko akijibu maswali waliyouliza alikazia sana suala la mang’amuzi endelevu ya wito mtakatifu yakiongozwa na sala, tafakuri na kujikabidhi katika maongozi ya Roho Mtakatifu. Walelewa walioshiriki katika mkutano huu, wakibidiishwa na ujumbe wa baba mtakatifu, hawakusita kuwashirikisha vijana wenzao uzoefu wa maisha yao binafsi mintarafu mchakato wa mang’amuzi ya mito katika muktadha wa maisha ya wakfu wanayoyaelekea.

Ushiriki wa waseminaristi, watawa na mapadre katika mkutano tangulizi wa sinodi ya maaskofu ulichochea chachu ya ushuhuda wa maisha ya kimungu katika miito mitakatifu. Vijana wengi walitambua kwa namna ya pekee uzuri na umaana wa maisha ya wakfu, wakishuhudia kwa macho yao wenyewe furaha waliyonayo vijana wenzao wanafuasa malezi ya kitawa na kipadre. Walelewa walikuwa kwa vijana wengi ishara na ukumbusho wa uwepo wa Mungu miongoni mwao. Vile vile walionesha mfano wa uvumilivu, ustahimilivu, upole, utulivu, masikilizano, furaha na uchangamfu, tunu ambazo ziliamsha kiu kubwa kwa vijana kutamani kufahamu zaidi na zaidi juu ya maisha ya wakfu.

Maisha ya wakfu yaliwachagiza vijana kutambua kamba mambo kama muziki, sanaa, vichekesho na kadhalika; ambayo mara nyingi huonekana kuwa ni ya kiulimwengu zaidi, hayakinzani na maisha ya wakfu ikiwa yanafanyika kwa namna, wakati na nafasi inayofaa. Ilikuwa uthibitisho halisi, burudani kali iliyotolewa na Sr. Cristina Scuccia sistercristina@facebook.com katika viwanja vya Ikulu ya zamani ya Castel Gandolfo. Yeye ni Mtawa wa shirika la Waorsolini wa Familia Takatifu, ambaye ni licha ya kuuishi utume wake kama mtawa yeye pia ni mwimbaji mashuhuri wa muziki wa kizazi kipya nchini Italia.

Kwa vijana wengi, licha ya mshangao; kusikia shuhuda hai za moja kwa moja za kufuasa maisha ya kutoa, kujitoa na kujitolea bila kujibakisha kwa ajili ufalme wa Mungu, iliendelea kuwa changamoto na motisha ya mfano wa maisha yaliyosheheni maana. Katika ulimwengu uliogubikwa na mawingu mengi ya itikadi na falsafa hasi, vijana wameendelea kuguswa kwa namna ya pekee katika majadiliano na vijana wa rika lao wanaoitikia miito mitakatifu. Licha ya kwamba kwa vijana wengi maisha katika utii, ufukara na useja ni mtihani, waseminaristi na watawa wamekuwa mfano na tumaini kwamba hakuna lisilowezekana kwa Mungu, mintarafu maadili na nidhamu ya maisha ya wakfu ikiwa ni pamoja na sadaka inayoambatana na maisha hayo. ‘waridi licha ya kunukia na kuvutia, linayo pia miba’. Juma zima la majadiliano ya vijana lilikuwa fursa nzuri kwa waseminari na watawa, kujifunda na kung’amua mambo muhimu husika na utume wa vijana. Miongoni mwa mambo hayo ni; nguvu ya majadiliano, mchango wa mitandao ya jamii kwa vijana katika uinjilishaji, Kiu ya vijana kuelewa vizuri mafundisho ya Kanisa na Umuhimu wa kiongozi wa roho.

Nguvu ya majadiliano; kiujumla vijana walimimina sifa kedekede kwa Baba Mtakatifu Francisko na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kwa fursa hii ya mkutano andalizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Kama alivyosisitiza Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika hotuba yake ya utangulizi, akielezea sinodi ya maaskofu mwaka huu 2018 alisema kuwa ka mkutano huu tangulizi ‘maaskofu watawazungumzia vijana na zaidi watazungumza na vijana’. Vijana wengi hawapendi kuwa wapokezi tu wa maamuzi kutoka juu, wanapenda kuwa sehemu hai ya maamuzi yatolewayo juu yao katika namna inayofaa. Mara nyingi wamechukuliwa kuwa ni vyanzo vya makosa na uharibifu na hivi kunyimwa ushiriki hai. Majadiliano kati ya vijana na walezi wao, kwa namna ya pekee wachungaji wao, yana nafasi kubwa katika ufanisi wa utume wa Kanisa. Vijana wakipewa nafasi katika majadiliano na kusikilizwa wako tayari kuonesha vipawa vyao na usanifu wao. Mkutano tangulizi wa vijana juu ya sinidi ya maaskofu juu ya vijana utakuwa ni ushahidi wa wazi wa umuhimu wa majadiliano kati ya Kanisa na makundi mbalimbali ndani yake, kwa namna ya pekee vijana. Aidha mkutano umekuwa ni nafasi nzuri ya kukuza majadiliano na watu wa imani nyingine na vile vile wale wasioamini. Yote hiyo imekuwa ni chachu ya kujitathmini vyema na kukuza weledi wa majadiliano ya kidini na kiekumene!

Mchango wa mitandao ya kijamii; mitandao ya kijamii ni uwanja usioepukika katika mchakato mzima wa utume wa vijana leo hii. Ulimwengu wa kidigitali unao vijana kama wadau na wateja muhimu. Ni jambo lisilofikirika kutafakari juu ya mitandao ya kijamii leo hii bila vijana. Kwa hiyo, Kanisa linao ulazima wa kuwekeza na kuelekeza jitihada za kutosha kutumia mitandao ya kijamii katika uinjilishaji, hususan kwa vijana. Kwa kutumia sikanu zao vijana wanao urahisi mkubwa wa kujipatia taarifa kokote waliko na katika muda wowote. Vijana wanaweza pia kutumia mitandao ya kijamii kushirikishana habari njema wakiwa mkondoni tu kupitia makundi sogozi katika facebook, whatsup, instagram, tweeter na Youtube pasi na kutumia nguvu nyingi! 

Tafiti kadha wa kadha zimeonesha kuwa vijana hutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii. Kumbe haitasaidia kukaa mbali na mitandao ya kijamii kwa kuogopa athari zake hasi. Ni wakati muafaka kwa Kanisa kama taasisi na kama familia ya Mungu, kukutana na vijana huko huko waliko. Ni ukweli usiopingika kwamba mitandao ya kijamii inazo athari nyingi, hatahivyo, kama asemavyo Papa Francisko kwamba, katika ulimwengu mamboleo haisaidii kuwakataza tu vijana kutumia vifaa vya mawasiliano (Amoris Laetitiae n. 275). Yafaa kuchunguza vyema, kujifunza na kuona namna ya kufaa kutumia mitandao ya kijamii kama fursa kwa uinjilishaji.

Chachu ya mafundisho ya Kanisa; vijana wanaonesha shahuku kubwa ya kuyafahamu mafundisho ya Kanisa hasa hasa kuhusu maadili ya kikristo na gunduzi mpya za kisayansi. Masuala kuhusu ndoa za jinsia moja, ushoga, akili bandia, roboti, matumizi ya vikinga uzazi na kadhalika, yamezua mijadala mirefu miongoni mwa vijana, mintarafu mafundisho ya Kanisa. Kumbe ni shime kubwa kwa wale wanaojiandaaa kuwa wachungaji na waalimu wa mafundisho ya Kanisa kujitoma katika kuyafahamu vizuri mafundisho ya Kanisa na kubuni sanaa na lugha rahisi ya kuyaeleza katika namna ambayo vijana wenzao watafauru kuelewa kwa urahisi.

Sambamba na hilo walelewa katika miito mitakatifu wamenusa na kujichangamotisha juu ya umuhimu wa kuyafahamu vizuri Maandiko matakatifu, Mapokeo ya Kanisa na Maandishi ya mamlaka funzi kwani vijana wengi wanahitaji msaada wa karibu kuyafahamu, kuyaelewa na kuyafuata. Harambee walelewa!! Taifa la Mungu lisiangamie kwa kukosa maarifa (Hosea 4,6). Tamanio la vijana kuwa na mashuhuda wazuri wa imani na maadili lilitawala majadiliano. Vijana wanaguswa na mifano mizuri ya maisha ya uadilifu hasa kutoka kwa vijana wa rika lao, wenye changamoto kama zao lakini wanaojituma kukazana kushikiria yaliyo kweli na kuyasimamia. Vijana wengi walikiri kutambua kwamba wale wanafuasa miito mitakatifu si ‘superman’ wenye nguvu za ajabu kushinda vishawishi vyote, bali ni binadamu kama wao wanaojitahidi kuweka tumaini lao katika maongozi ya Mungu ili kuifanya kazi ya Mungu vema.

Umuhimu wa kiongozi wa maisha ya kiroho; Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kutano huo, Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia nafasi ya wazee na walezi katika mchakato wa kung’amua wito kwa vijana, alisisitiza vijana kuwa na wenzi wa safari ya mang’amuzi. Aliwataka vijana kupyaisha mahusiano yao na wazee lakini hasa na wazee wenye busara kwa njia ya mazungumzo nao. Desturi ya kuwa na mlezi wa kiroho katika maisha ya wakfu ilionekana kuwa mwanga pia kwa maisha na mang’amuzi kwa kijana yeyote. Hitaji la kuwa na mtu jirani wa kuelekeza, kukosoa na kuonesha njia ya kufuata liliendelea kudhihirika kuwa ni la vijana wote, tena si tu katika muktadha wa dini bali hata maisha ya kawaida ya kila siku. Mkutano baina ya walelewa katika miito mitakatifu ya upadre na utawa na vijana wengine wanaoishi au kutafakari miito yao mingine, ulikuwa darasa tosha la utajirishanaji wa mawazo na uzoefu kati ya pande hizo mbili.

Na,

Frt. Karoli Joseph AMANI  wa Jimbo kuu Katoliki Tabora

Chuo Kikuu Cha Kipapa Urbaniana, Roma.
All the contents on this site are copyrighted ©.