2018-04-05 11:10:00

Kitimu timu cha Tomaso mwenye imani haba kama kiatu cha raba!


Msafara mzima wa historia ya mahusiano ya upendo kati ya Mungu na binadamu unahitimika katika Ufufuko wa Yesu. Yaani safari nzima ya maisha ya Yesu hapa duniani inagota kwenye ufufuko wake na ndiyo tungesema ufufuko ndiyo mwisho wa reli. Hapo msafiri ukishuka kutoka kwenye treni unaingia katika ulimwengu mpana zaidi wa safari. Ni sawa na kusema: “mwisho wa uwanja ni mwanzo wa nje”. Mwanzo huu wa safari mpya usio na mipaka wa maisha ya ufufuko unatajwa waziwazi siku ya pilikapilika za Maria Magdalena: “Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado.” (Yoh. 20:1). Maria Magdalena mwenye kupagawa na upendo kwa Yesu anaamka asubuhi na mapema kwenda kaburini peke yake siyo kwa ajili ya kupaka manukato maiti, bali kwa ajili ya kwenda tu kumwona mpendwa wa moyo wake, potelea mbali awe mzima au la, yeye anatamani tu kuuona mwili wake na kumkumbatia. Tena hasemi kwamba anakwenda kuhani msiba yaani anaenda kumwona marehemu (maiti) la hasha, bali anasema: “Bwana wangu”. Halafu tena juu ya jioni ya siku hiyo hiyo ya kwanza inasemwa: “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati…”

Kwa hiyo, Siku hii ya kwanza au siku ya nane, ni mwanzo mpya usio na kikomo yaani umilele. Mungu alifunga kazi ya kuumba ulimwengu siku ya sita na ya saba akafika mwisho. Akapumzika. Kumbe siku ya saba ni mwisho wa maisha ya binadamu na siku ya nane ni mwanzo mpya wa maisha ya binadamu, na ni wa ulimwengu wa umilele wa Mungu usio na mipaka. Kumbe katika namba hiyo nane, ulimwengu wa kibinadamu umeingizwa katika ulimwengu wa kimungu. Hapo kama ndiyo mwisho wa safari ya treni la zamani (na rubani wa kubabaisha), basi Mungu amejenga reli ya kisasa (tunaanza safari mpya) na rubani wake ni Yesu aliyekalia usukani. Kwa hiyo kutoka namba nane sasa tunarudishiwa hadhi yetu na tunapaishwa juu zaidi. Ndugu zangu pale tutakapotambua hilo fumbo lililo katika namba nane, yaani ya fumbo la umilele wetu, yaani fumbo la maisha ya kimungu katika maisha ya kibinadamu, hapo ndipo tunaweza kujua maana ya kufufuka na kumgusa mfufuka. Ama kweli katika ufufuko wa Yesu “tutaisoma namba nane!”

Ili kuujua utamu ulioko katika treni mpya na kumgusa Yesu rubani wake mpya katika safari ya hapa ulimwenguni na ya kutupeleka kwenye kituo kikuu-mbinguni, nakualika kutanguzana na mtume Tomaso. Yeye hakuwapo jioni ile ya kwanza (namba nane) Yesu alipotokea: “Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu”. Yaonekana baada ya Yesu kuteswa, kuuawa na kuzikwa, Tomaso alienda kuvinjari na kupeta barabarani bila kuwaogopa Wayahudi. Labda alitaka kutikisa kiberiti na kusikiliza watu wanasemaje juu ya yaliyompata Yesu.  Kumbe, asijue kuwa jioni hiyo Yesu alifanya mambo mawili: Mosi alipotokea tu, akawaamkia mitume wake: “Amani iwe kwenu.” Kwa salamu hii ni dhahiri kwamba, Yesu aliwatuliza wanafunzi wake kutokana na yote yaliyomsibu. Kama vile angesema: “Najua mmebanwa, mguswa na mmetikisika na kuyumba sana na mliyoyaona, kama nilivyokwisha kusema kabla ya kuteswa kwangu kwamba ‘Usiku wa leo wote mtakwazika kwa sababu yangu. –skandalishesesthe.” (Mk 14:27). Lakini kuanzia sasa tulizeni boli, tangu sasa ni kicheke kwenda mbele tu! Poeni na muwe na amani, safari inaanza upya na mnitumainie mimi.” Kisha kitendo cha pili Yesu anawavuvia na kuwaambia: “Pokeeni Roho mtakatifu”. Hapa ikumbukwe kuwa alipokuwa Msalabani aliitoa roho yake: “Akainama kichwa akaitoa roho yake.” Yaani anawapa nguvu mpya.

Pili, anawaagiza kazi: “Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa.” Hii ndiyo hali inayotakiwa katika kuanza safari mpya: kwanza inabidi kutulia (kuwa na amani) na kumwaminia rubani anayetutia nguvu mpya (Roho Makatifu). Pili kuna kazi mpya ya kuliacha treni la zamani na kuingia jipya, yaani kusamehe yote kwani sasa “ya kale hayako tena, tugange yaliyoko na yajayo.” Kumbe ufufuko ni ushindi juu ya woga wa maisha na endapo tupo bado tumejifungia chumbani kwenye treni la zamani, sababu ya woga Yesu anaingia na kutupa matumaini mapya na kuturudishia furaha yetu tena. Hapo tunakuwa mashahidi wa ufufuko, mashahidi wa upendo wa Mungu uliojionesha katika Yesu aliyeshinda mauti.

Tomaso aliporudi toka huko alikoenda, wenzake wakamsimulia yaliyojiri alipokosekana. Yeye hakuwaamini kabisa na anawaambia waziwazi: “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.” (Yn 20:25). Hapa ndugu huyu hataki tu kuisoma namba bali hata kuigusa. Basi ile namba nane inajirudia anapofika Yesu mara ya pili: “Basi baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo ndani tena na Tomaso pamoja nao.” au katika ofisiyo maneno hayo yanaimbwa hivi katika antifona: “Baada ya siku nane, akaja Yesu na milango imefungwa akawaambia; amani iwe kwenu aleluya, aleluya.” Hivi baada ya siku ya nane (oktava) baada ya safari mpya kuanza, yaani katika wiki la ulimwengu wa umilele.

Hapa Tomaso anatuwakilisha sisi tulio tayari katika safari hii ya umilele. Yesu anafika na kukidhi tamanio la Tomaso na anavyotafuta jinsi ya kumwelewa na kumgusa huyo mfufuka anakuwaje. Anamwita na kumwambia: “Tomaso, lete hapa kidole chako, itazame mikono yangu; ulete hapa mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yn 20:17). Yesu anataka aguswe licha ya kuonwa. Kule kufanikiwa kumwona Yesu na kumgusa ndiko kunakompelekea Tomaso kuungama waziwazi imani yake iliyojaa upendo: “Bwana wangu na Mungu wangu!”(Yn 20:28). Namna hii pia aliungama Natanaeli alipoitwa na Yesu: “Wewe ni mwana wa Mungu, wewe ni mfalme wa Wayahudi” (Yn 1:49). Lakini, Tomaso anaenda mbele zaidi anapoongeza tendo la kumilikisha na kusema: “Bwana wangu, na Mungu wangu.”

 Kumbe, hapa Tomaso “Amesoma sawasa namba ya treni jipya.” Sasa siyo tena suala la imani tu ya kidhahania, au ya kiakili, bali ni imani ya kujimilikisha kabisa. Kwamba kwa ufufuko ule Tomaso amejimilikisha Yesu na amekuwa Bwana wake na Mungu wake. Hapa sasa kuna mahusiano mapya na wa kibinafsi na Yesu. Kwa hiyo mahusiano na Yesu mfufuka hayapo kama ya mtu kuliona treni jipya na kulishangaa, bali hata kuligusa na kulisafiria. Yaani siyo tu suala la kumwona Yesu mfufuka na kumstaajabia, bali kumgusa yaani kuwa na mahusiano naye. Kumgusa, kumpenda na kumuishi.

Ndugu yangu yule tu anayeweza kusema kama Tomaso “Bwana wangu na Mungu wangu!” hapo ujumbe wa Pasaka umeshamfikia. Anayeelewa kuwa Yesu ni Bwana na Mungu basi huyo amefufuka katika maisha kweli. Huyo macho yake yamefunguka na anaweza kutambua kitu gani kinafumbatwa katika uwepo wake kama binadamu halisi aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Hadi hapo ndipo Yesu kama rubani mpya katika safari ndani ya treni jipya, anamtania Tomaso: Yaani “Wewe kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.” (Yn 20:29). Ndugu zangu kwa wasioona treni la kisasa linavyoleta raha na linavyotitirika na kufyatua mwendo, hawawezi kuamini hadi walione na kuligusa ndiyo wataridhika. Kwa vyovyote katika Tomaso tunaweza kujikuta tunatamani kumwona Yesu na kumgusa. Sisi hatumwoni Yesu kama mitume na waliomwona na wakashuhudia matendo aliyoyafanya na wakatuandikia, bali sisi tunasoma tu yale waliyotuandikia. Tomaso anatuwakilisha sisi ambao tumemsikia tu Yesu bila kumwona wala kumgusa. Kwamba ni imani peke yake inaweza kutushirikisha katika uhalisia wa umungu. Sanasana kwetu Wakatoliki tumebahatika, tunaweza kumwona na kumgusa Yesu katika Ekaristi Takatifu tunayoipokea.

Ndugu zangu, mwanzo wa safari hii mpya ya umilele, tunaaswa kuwa na imani ya ufufuko wa Yesu. Hapo tu ndipo tunaweza kushiriki maisha ya kweli, maisha ya Mungu na tutatambua na kuuishi ukweli. Uelewa wetu wa mambo utakuwa mpya na hakika tutakuwa watu wapya tuliobadilika na kufufuka pamoja na Kristu. Vinginevyo tutaendelea kubaki ndani ya treni la zamani hata kama limeshafika mwisho wa reli. Hii ndiyo hatima ya habari njema ya leo: “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina lake.” Leo pia Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ikamwilishwa zaidi na Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu muhtasari wa historia nzima ya ukombozi, inayomwambata mwanadamu katika medani mbali mbali za maisha yake!

Heri na baraka kwa Siku kuu ya Pasaka.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.