2018-04-05 13:16:00

Injili ya huruma ya Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa


Katika jumapili ya leo, kanisa lutuagiza kusherehekea huruma ya Mungu – kutangaza kwa uwazi huruma ya Mungu ikikumbuka magumu na majaribu yaliyo mbele ya mwanadamu. Matayarisho katika kungoja jumapili hii huanza kwa Novena siku ya Ijumaa Kuu ambayo huhitimishwa jumapili hii ya leo. Sikukuu hii ilitangazwa rasmi hapo Mei 2000 kwa agizo la Baba Mtakatifu Yohane Paulo II. Ibada kwa huruma takatifu ya Mungu ni sehemu ya maisha ya kiroho ya kanisa. Ibada ambayo Mtakatifu Faustina Kowalska aliyetangazwa mtakatifu tarehe 30/04/2000 aliishi kwa uwazi katika maisha yake na kwa makusudi mazima Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliweka sikukuu hii kutukumbusha huruma ya Mungu inavyotawala katika maisha na utume wa kanisa na ulimwengu. Katika kitabu chake “ Kumbukumbu ya Huruma ya Mungu katika roho yangu” chaonesha jinsi Mungu alivyo mwaminisha utumewa kutangaza tena kwa ulimwengu ujumbe wa Injili wa huruma yake kwa wote na zaidi sana kwa wenye mahitaji zaidi.

Kiini cha ibada hiyo ni kumwamini na kumsadiki Bwana wetu Yesu Kristo. Ili kuishi kila siku na roho ya huruma kwa jirani kwa sala, maneno na matendo. Huruma ya Mungu au huruma takatifu yatuwajibisha tunapofanya mambo ya Mungu – kuwajibishwa na upendo wa Mungu. Ni swala la kufa au kupona, si shauri la mimi kutaka au kuwazia au kuamua kufanya au la. Huu ni ushuhuda amini wa matokeo ya upendo wa Mungu kama tunavyoshuhudia katika ufufuko wake Bwana. Kwa hakika si rahisi kupinga uwepo wa Kristo na matendo yake katika historia. Kwamba alizaliwa – angalia Mt. 1:1-17, ukoo wa Yesu – Lk. 3:23-38, aliishi kati ya watu,  Lk. 1:39 – anamtembelea Elizabeti na Lk. 4:14 – anaanza kuhubiri katika Galilaya. Kwamba alikuwa na wafuasi na mitume – LK. 6:12-16. Kwamba alifanya miujiza – ufufuo wa Lazaro – Yoh. 11, kwamba aliteswa – angalia mazingira ya hukumu yake, watu wangapi walihusishwa – Pilato, Herode, Kayafa, Anasi, kuachiliwa kwa Baraba n.k, ni watu ambao waliishi na walishiriki katika siasa ya wakati ule. Historia ya kweli. Kuhusu kuwa alifufuka maelezo yake yaonekana kuwa magumu ila matokeo ya ufufuko wake yameonekana na wengi na ushuhuda wake ni wa kweli.

Zaidi sana tunasoma katika Yoh. 20;29 – wengine watamsadiki Yesu bila kumwona kwa ushuhuda wa mitume tu – Yoh. 17;20, Mdo. 1:8. Maisha ya mtakatifu Faustina ni ushuhuda wa karibu mno kuthibitisha hilo. Kwa kifupi, maandiko matakatifu ni ushuhuda wa uwepo wa upendo wa Mungu kwetu sisi, upendo uliothibitishwa na uwepo wa Kristo kati yetu.  Kinachoonekana kwa ujumla ni kuwa kifo na ufufuko wake Kristo kimekuwa ni sababu ya imani ya watu wote – Mk. 15:39, makaburi yakafunuka – Mt. 27:52-53 na hata kwa kufa kwake sisi tumepata roho wake Mungu – Yoh. 19:30.

Tendo la ufufuko wa Yesu siyo tendo la ushujaa. Baada ya ufufuko, Yesu anawatakia amani na kuwatuma waende. Katika Ebr. 3:1 tunasoma neno hili – kwa hiyo ndugu watakatifu wenye kuushiriki mwito wa mbinguni mtafakarini sana mtume na kuhani mkuu wa maungano yetu, Yesu aliyetumwa kwe ulimwengu. Ufufuko wahitimisha utume wake sasa. Naye aweza kuwapeleka mitume wake, wale aliowachagua yeye ili wapate kuendeleza kazi hiyo ya upendo wa Mungu kwetu. Pia karibu sana na roho ya ufufuko ni maneno ya Yesu, pokeeni roho mtakatifu. Yoh. 16:7 – lakini mimi nawaambia iliyo kweli, yawafaa ninyi mimi niondoke kwa maana mimi nisipoondoka huyo msaidizi hatakuja kwenu bali mimi nikienda zangu nitampeleka kwenu.

Katika hotuba yake siku ya Pentekoste, Mtakatifu Petro anaonesha wazi kuufahamu mpango huu wa Mungu. Anaunganisha vizuri kabisa ufufuko wa Bwana na kupeleka roho mtakatifu. Anasema akiwa ametukuzwa na Baba, Yesu alipokea roho aliyeahidiwa kutoka kwa Baba halafu akamtuma roho huyo kwetu – Mdo. 2:33.

Hakika ni mapenzi yake Baba kuwa ametupatia ukombozi na kwa njia hii kwetu ni fumbo kuu la upendo. Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanatupenda upeo kiasi cha kujitoa kwetu. Fumbo hili la upendo ni kwa ajili yetu. Ufufuko wa Kristo ni ufunguo wa mlango unaoruhusu ujio huu wa neema na upendo wa Mungu kwetu. Kama tukikubali maisha yake ina maana pia twakubali  upendo wake ndiyo maana ya ufufuko kwetu. Hii ndiyo maana  ya Pasaka. Mungu anamweka Yesu awe hakimu wa ulimwengu, wa wazima na wafu. Ametukuzwa juu mbinguni na kazi ya kuwakomboa watu inaendelea ndiyo sababu tuko hapa – hilo tukio lingeishia pale msalabani au kaburini hakika tusingekuwa tunafanya kumbukumbu hii au sherehe hii leo hii. Hivyo ni lazima tuendeleze fumbo hili. Mt. Petro anasema kila aaminiye anao msamaha wa dhambi na uzima wa milele – tukiamini na kuishi hivyo tutaokoka. Matumaini yanatuhimiza tuwe watakatifu – 1Pt. 1:3.

Sisi tunaalikwa kuujua ufufuko na kuushuhudia vizuri kama mitume. Ufahamu ni wokovu. Mfano huu ututafakarishe – mchungaji mmoja alifika mjini akitaka kwenda posta. Kwa bahati mbaya hakuijua vizuri barabara ya kufika posta. Kwa muda mrefu akawa anazunguka zunguka eneo hilo lakini bila mafanikio. Hakuwa na unyenyekevu wa kuomba msaada. Kijana mmoja alikuwa anamwona na baada ya muda akamfuata na kumwuliza anachokitafuta. Yule mchungaji akamwambia kuwa alitaka kufika ofisi ya posta. Naye bila kusita yule kijana akamwambia mzee ofisi ya posta ile pale mbele ya  macho yako. Baada ya kumaliza shughuli zake pale ofisini, yule mchungaji akamshukuru kijana na pia kumpa mwaliko kuwa jioni ya siku hiyo katika viwanja vya kanisa lake atatoa mahubiri mazuri sana juu ya namna ya kufika mbinguni. Kijana alimshukuru kwa mwaliko lakini akamwambia wazi kuwa hatafika. Mchungaji akashangaa kweli kweli na kumwuliza kijana kulikoni.  Yule kijana akamwambia kuwa itakuwaje uweze kufundisha njia ya kufika mbinguni ilihali hujui njia ya kufika posta. Mfano huu ututafakarishe sana juu ya ufahamu wetu wa ufufuko na ushuhuda wa huo ufufuko ili tuweze kuishi vizuri hiyo huruma ya Mungu kama alivyofanya Mtakatifu Faustina.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.