2018-04-04 07:50:00

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Kanisa kuanza kuadhimishwa mwaka 2018


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni kuridhia tamko lililotolewa na Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa kwamba, kuanzia sasa  Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Kanisa itakuwa inaadhimishwa Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste, taarifa ya Baraza inakaza kusema, maadhimisho haya yanaanza rasmi mwaka 2018.  Mabadiliko haya yanapaswa kuingizwa kwenye Kalenda za maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kufanyiwa kazi tangu sasa! Ibada hii kwa Bikira Maria, itawasaidia waamini kukumbuka kwamba,  maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba linaloadhimishwa katika Ekaristi Takatifu, Kanisa linapomtolea pia sifa na heshima Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi!

Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa, hivi karibuni limetoa ufafanuzi kuonesha kwamba, mahali pale ambapo, Sherehe ya Pentekoste inaendelea kuadhimishwa na waamini Jumatatu au Jumanne kama kumbu kumbu ya hiyari, itaendelea kama ilivyooneshwa kwenye Misale ya Kirumi. Lakini kadiri ya taratibu, kanuni na sheria za Kanisa pale ambapo zinakataza kumbu kumbu ya hiyari wakati wa Kipindi cha Majilio kuanzia tarehe 16 Desemba; Wakati wa Sherehe za Noeli hadi tarehe 2 Januari na Wakati wa Oktava ya Pasaka. Lakini, kutokana na sababu za kichungaji kumbu kumbu ya hiyari inaweza pia kuadhimishwa.

Pamoja na maelezo yote haya, lakini, Kumbu kumbu ya Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Maelezo kamili ya vitabu vya Ibada vinavyopaswa kutumiwa tayari yalikwisha pelekwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia: sanjari na masomo yaliyowekwa kwani haya yanatoa mwanga wa Fumbo la Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Kwa kuzingatia kwamba, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Kanisa ina muunganiko wa pekee na Sherehe ya Pentekoste kama ilivyo Kumbu kumbu ya Sherehe ya Moyo Safi wa Bikira Maria inavyoshibana sana na Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kumbe, pale ambapo kunakuwepo na mwingiliano na kumbu kumbu za watakatifu wa Kanisa, Sherehe ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kabisa! Ufafanuzi huu, umetolewa na na Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa tarehe 24 Machi 2018.

Itakumbukwa kwamba, mabadiliko haya yanapaswa kuonekana kwenye Kalenda ya Liturujia kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na kwenye Vitabu vya Sala za Kanisa. Tafsiri ya machapisho ya maadhimisho haya inapaswa kufanywa na Mabaraza ya Maaskofu na hatimaye, kupitishwa na Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa. Katika maeneo ambayo Ibada hii inaadhimishwa kwa heshima kubwa, wataendelea na utaratibu wa. Kwa hakika Mapokeo ya maadhimisho ya Fumbo la maisha ya Kristo ambayo kamwe hayawezi kumtenga Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa. Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Wakristo ambao wamezaliwa kwake kwa njia ya fadhila ya upendo na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kama wanavyofundisha Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na Mtakatifu Leo Mkuu. Umama wa Kristo na Kanisa ulihitimishwa pale chini ya Msalaba, Bikira Maria alipopokea upendo wa dhati kutoka kwa Mwanaye mpendwa na Yohane kwa niaba ya wengine wote, wakawa ni wafuasi na mitume wa upendo kwa ajili ya Mama yake.

Bikira Maria aliendelea kuandamana na Kanisa katika sala wakati Mitume wakisubiria ujio wa Roho Mtakatifu. Kwa nyakati mbali mbali, waamini wamekuwa wakimheshimu na kumfanyia Ibada Bikira Maria kama: Mama wa Mitume, Mama wa waamini wa wale wote wanaozaliwa upya katika Kristo Yesu na Mama wa Kanisa kama wanavyofundisha Papa Benedikto XV pamoja na Papa Leo wa XIII. Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 21 Novemba 1964, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipokuwa wanahitimisha Kikao cha tatu cha Mkutano huo, alitamka kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa; yaani: ni Mama wa Wakristo wote na wachungaji wanaomkimbilia kama Mama.

Kumbe, Bikira Maria, Mama wa Kanisa anapaswa kuheshimiwa na Wakristo wote. Katika maadhimisho ya Mwaka Upatanisho, mnamo mwaka 1975, kuliadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Litania ya Bikira Maria wa Loreto ikaongeza heshima hii katika Litania. Majimbo mbali mbali wakaona kwamba, inafaa na kuomba Kiti Kitakatifu kuruhusu maadhimisho haya yaingizwe katika kalenda ya majimbo yao! Kutokana na kukua na hatimaye, kukomaa kwa Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia tamko lililotolewa na Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa kwamba, kuanzia sasa  Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Kanisa itakuwa inaadhimishwa Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste ya kila mwaka! Tamko hili limetiwa mkwaju na Kardinali Robert Sarah na Askofu mkuu Arthur Roche, Mwenyekiti na Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa, tarehe 11 Februari 2018, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.
All the contents on this site are copyrighted ©.