2018-04-04 11:01:00

Jumapili ya Huruma ya Mungu, mwanzo wa maisha mapya katika huruma!


Mpendwa msikilizaji wa Vatican News! Mtume Petro anatualika katika antifona ya mwanzo ya Dominika hii akituambia: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”. Tuuunganishe mwaliko huu na adhimisho la Huruma ya Mungu ambalo tunaalikwa katika dominika hii ya pili ya Pasaka ambayo inahitimisha siku nane au Oktava ya Sherehe ya Pasaka. Maziwa yasiyoghoshiwa ni maziwa halisi ya mama ambayo hayajachanganywa na kitu chochote. Hii ni lishe muhimu kwa mtoto mchanga kwa ajili ya kumjengea kinga za asili na ambazo zinaranda na vinasaba vyake kutokana na ukaribu wa mama na mtoto wake. Inakuwa ni bahati mbaya kwa mtoto mchanga kukosa maziwa ya mamaye kwa sababu fulani kwani pia pamoja na kumpatia lishe na mengineyo ya kuumkuza, kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama yake humuunganisha kwa karibu na mzazi wake.

Tangu zamani Kanisa pia inaiita dominika hii kwa jina la “in albis” ambayo iliunganishwa na ukamilifu wa ibada kwa wale waliobatizwa wakati wa mkesha wa Pasaka. Kila mkristo mpya alivishwa nguo nyeupe kuashiria mwanzo mpya na kupata hadhi mpya ya kuwa mwana wa Mungu. Nguo hiyo inapaswa kuvaliwa kwa juma zima hadi dominika ya leo ambapo nguo hiyo inatolewa. Hapa wanapewa sasa hadhi ya kuanza maisha mapya ndani ya Kanisa na kwa msingi huo maisha hayo yalipaswa kustawishwa na kanisa lenyewe kwa njia ya Sakramenti zake. Ndiyo maana wanaalikwa kuyatamani maziwa yasiyochakachuliwa, maziwa halisi kusudi kwa hayo wapate “kuukuliwa wokovu”. Ni mwaliko wa kubaki katika mafundisho na misingi ya kanisa kwa makusudi ya kuufikia wokovu.

Dhana hiyo inaunganika vizuri na Huruma ya Mungu ambayo tunaalikwa kuiadhimisha leo. Kimsingi fumbo zima la Pasaka linaiadhimisha huruma ya Mungu. Adhimisho la huruma ya Mungu lina asili yake tangu wakati wa adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huruma ya Mungu inatuangaza kulielewa vema Fumbo la Pasaka kwani huzifungua akili zetu ili kulielewa vema fumbo la Mungu na uwepo wetu hapa duniani. Hivyo kutusukuma kuwa mashuhuda wa Pasaka katika maisha yetu. Hivyo huruma hiyo ya Mungu ambayo Mtakatifu Faustina Kowalska aliiona kama miale ya rangi nyekundu ikiwakilisha damu ya Kristo na rangi ya bluu hafifu iliyokwajuka au samawati ambayo iliwakilisha maji ya ubatizo yaliyozistahilisha tena roho za wanadamu mbele ya Mungu. Kwa hiyo adhimisho la huruma ya Mungu huufunua ukarimu, msamaha na upendo wa Mungu ambao kwa ujumla wake huadhimishwa katika fumbo la Pasaka.

Injili ya Dominika hii hutupatia simulizi la Tomaso, mtume ambaye kwanza aliona shaka lakini alifunuliwa ubavu na Kristo mwenyewe na kuona aliishia katika kuamini. Ubavu wake Kristo uliofunuliwa unatufungulia hazina za ufalme wa Mungu na hayo ndiyo maziwa yasiyoghoshiwa tunayoalikwa kujishibisha nayo kwa ajili ya wokovu wetu. Tunapoelekeza macho yetu na kumtazama Yeye waliyemchoma ndipo tunapouona urefu na upana wa upendo wa Mungu na hivyo kukiri kama Mtume Tomaso “Bwana wangu na Mungu wangu” na kisha kwenda kushuhudia kwa matendo yetu. Ni maelekezo kwenda kwake kama kisima chenye maji ya uzima. Imani yetu juu ya ufufuko wake inatupatia nguvu ya kumsikiliza na kufuata mafundisho yake kama kielelezo kwa maisha yetu ya kila siku. Ni onyo kwamba tusijaribu kuchanganya mambo mengine na uzima huu tuupatao kwa Kristo. Tunaelekezwa kuutunza na kuufanya hai daima kwa ajili ya wokovu wetu.

Pasaka inatupatia maisha mapya yanayochipuka katika Kristo mfufuka. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidhihirisha upya huu wa maisha katika maisha yao ya kindugu. Kwanza walikuwa na moyo mmoja na roho moja; hakuna ambaye alimiliki sana au kukosa kabisa. Wote waliishi katika hali ya umoja, “wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao aliyekuwa na mahitaji”. Furaha ya Kristo mfufuka inamsukuma kila mmoja kujiona anaungana na ndugu yake. Waliokuwa navyo wanajitoa na kuwagawia wengine. Hapa tunaona moja ya tunda muhimu linaloletwa na Kristo mfufuka, yaani kuwaunganisha wanadamu wote katika nafsi yake. Sote tunakuwa ni kaka na dada kwani kwa kuungana na Kristo tunafanywa kuwa mwili mmoja na roho moja. Muungano wetu huu katika Kristo unastawisha na neema zake Kristo mwenyewe zinazobubujika kutoka ubavuni mwake. Ni baraka za kimbingu ambazo zinatuhakikishia wokovu kwani tunakua na kukomaa katika yeye Kristo mfufuka.

Hili ni jawabu kwa jamii ya wanadamu inayopambwa na misukosuko mbalimbali; jamii ambayo imejitenga; jamii ambayo kila mmoja anatafuta kupata zaidi hata kama atapitia mgongo wa mwenzake. Tunashuhudia leo hii utamaduni wa kifo unatawala, utamaduni wa kutupa vitu bila kuwajali wahitaji, vita na magomvi na dhuluma nyingi ambazo zinaukandamiza ubinadamu. Uko wapi ushuhuda wetu kama wakristo? Neema za Kristo zinazotumiminikia kutoka katika ubavu wake zinatuwezesha kupingana na hayo. Neema za Kristo zinazotububujikia kutoka ubavuni mwake ndizo zinazotuwezesha katika karama mbalimbali ambazo kwazo tunapaswa kuzidhihirisha kama ilivyokuwa kwa jamii ya wakristo wa kwanza, yaani, kwa ajili ya watu wote. Tumshuhudie Kristo kwa kufanya juhudi ya kuupyaisha ubinadamu ulichakazwa. Hiyo ndiyo inapaswa kuwa alama ya jamii ya kikristo ambayo inapambwa na upendo.

Mtume anatuambia katika somo la pili kutekeleza ushuhuda huo kwa kuzishika amri za Mungu. Amri zake ni maagizo yake ya namna tunavyopaswa kuenenda katika ulimwengu huu. Amri hizo zinadhihirika katika kumpenda Kristo aliye ufunuo wa amri zake. Mwanadamu anakabiliana na maswahibu mbalimbali kwa sababu tu ya kuacha kuzishika amri za Mungu. Mwanadamu anapomwacha Mungu anajikuta anaingia katika uhuria wa kimaadili na kila mmoja kujiamulia mambo yake na mwisho wake ni mgongano katika kutetea maslahi binafsi. Maisha ya kipasaka yanatuwezesha kuungana na Mwana wa Mungu na hivyo kuweza kuzitimiza amri zake. Ushuhuda wetu wa maisha ya kipasaka uonekane katika umoja wetu wa kindugu; umoja ambao unamfanya kila mmoja kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya wengine. Tukiwa tumepokea upya huu wa maisha ya kipasaka tuiadhimishe Pasaka hiyo katika maisha yetu huku tukichagizwa na baraka za kimbingu zinazotububujikia kutoka ubavuni mwa Kristo. Hizo ndizo neema mbalimbali zipatikanazo kwa njia ya huduma ya kanisa; ndiyo maziwa yasiyoghoshiwa ambayo kwayo tutaufikia wokovu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.