2018-04-04 08:19:00

Askofu mkuu Auza: Haki msingi za watoto wahamiaji zizingatiwe!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018, anakazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii. Baba Mtakatifu anasema, Kuwalinda maana yake ni kuhakikisha kwamba haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu zinalindwa na kudumishwa, kwa kupatiwa huduma ya faraja; kwa kulinda na kutunza nyaraka na utambulisho wao; kwa kupatia fursa za haki, nafasi ya kuweka kufungua akaunti ya fedha benki pamoja na huduma makini ya maisha; kwani kwa hakika, wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni hazina na amana kwa jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi.

Kumbe, utu na heshima yao, uhuru wa kutembea, uwezekano wa kupata fursa za ajira na mawasiliano ni mambo ambayo wanapaswa kupewa. Kwa wale wanaotaka kurejea makwao, basi, kuwepo na huduma itakayowawezesha kuingizwa katika mfumo wa kazi na jamii katika ujumla wake. Itifaki za kimataifa kuhusu haki za watoto wakimbizi na wahamiaji hazina budi kufuatwa na kuzingatiwa kikamilifu, kwa kupewa elimu ya msingi na sekondari na kamwe wasiwekwe vizuizini. Watoto wasio ongozana na wazazi na walezi wao, wapewe ulinzi na usalama wa kutosha; wahakikishiwe haki zao msingi kwa kuzingatia sheria za kimataifa. Wakimbizi na wahamiaji wapewe nafasi ya kupata huduma ya afya ya jamii, waingizwe kwenye mfumo wa pensheni na uwezekano wa kuhamisha mafao yao pale wanaporejea makwao.

Hivi karibuni, Askofu Mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican  kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia mada kwenye mjadala maendeleo na mafao ya watoto wanaojikuta wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za uso wa dunia anasema, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Hii ni kazi inayotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Majimbo pamoja na Parokia. Kunako mwaka 2016, Jumuiya ya Kimataifa iliridhia mchakato wa kusitisha uwekwaji wa watoto wakimbizi na wahamiaji kwenye vizuizi, ili kulinda na kudumisha haki zao msingi pamoja na uhuru.

Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji, maarufu kama "Global Compact" ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuondokana na kisingizio cha usalama wa taifa, sera na mikakati ya kisiasa isiyopenda kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, ambao ni rasilimani inayopaswa kutumiwa vyema kwa kuheshimu haki zao, utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kwa namna ya pekee, watoto wanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia: Sheria, kanuni na sera zinazoshughulia haki msingi za watoto kimataifa. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, watoto wanaowekwa kizuizini wanapata madhara makubwa katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni. Kuna baadhi ya nchi ambazo zimefanikiwa kutoa suluhu mbadala kwa kutowaweka watoto wakimbizi  na wahamiaji vizuizini. Njia hii inapaswa kufuatwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wadogo.

Kwa upande wake, Monsinyo Robert J. Vitillo, Katibu mkuu wa Tume ya Kikatoliki ya Wahamiaji Kimataifa, “International Catholic Migration Commision” anakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa: kulinda na kudumisha haki msingi za watoto sanjari na kuhakikisha kwamba, maamuzi yanayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa yanasaidia ustawi wa watoto wenyewe. Huu ni ushauri pia ambao unatolewa na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR.

Sheria ya watoto wakimbizi na wahamiaji iliyopitishwa nchini Italia kunako mwaka 2017 baada ya kuona wimbi kubwa la watoto wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanatembea peke yao bila ya ulinzi na usalama wa wazazi wao, liliamua kwamba, watoto hawa wasirudishwe makwao katika nchi ambamo kuna vita, kinzani na migogoro kwani wanaweza kuteseka zaidi. Muda wa watoto kuishi vizuizini upunguzwe na kwamba, watoto hawa wapewe ulinzi na malezi na wataalam waliobobea sanjari na kuzishirikisha familia ambazo zinaweza kutoa hifadhi kwa watoto kama hawa!

Mahitaji ya watoto na vijana yapembuliwe kwa kina na mapana na kupewa majibu muafaka. Kuandaa miundo mbinu itakayokuwa rafiki kwa ajili ya kuwahudumia watoto hawa, sanjari na kuboresha bajeti kwa ajili ya Manispaa zinazotoa hifadhi, ulinzi na usalama kwa watoto hawa pamoja na kuanza mchakato wa kuweza kuwaunganisha watoto hao na familia zao asilia. Huu ni mfano wa sheria rafiki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wakimbizi na wahamiaji! Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa Nchini Ubelgiji, “Caritas International Belgium” linalofanya utume wake katika nchi 200 duniani, limefanikiwa pia katika mchakato wa kuwaunganisha watoto wakimbizi na wahamiaji pamoja na familia zao.

 Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.