2018-04-03 13:19:00

Ulimwengu unaomboleza kifo cha Mama Winnie Madikizela Mandela!


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limesikitishwa sana na taarifa ya kifo cha Mama Madikizela Mandela, aliyefariki dunia, tarehe 2 Aprili 2018 akiwa na umri wa miaka 81. Kwa muda wa miaka 50 alikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya siasa na sera za ubaguzi wa rangi; ustawi, maendeleo na demokrasia ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini. Katika harakati za mapambano haya akajikuta anatengwa na familia, watoto, ndugu na jamaa zake, kiasi cha kuangaliwa kama mtu hatari sana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.

Askofu William Slattery, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini katika salam zake za rambi rambi kwa familia ya Mzee Nelson Mandela anasema, Mama Madikizela licha ya kuwa ni mke wa Mzee Madiba, lakini pia alikuwa kweli ni mwanamke wa shoka, aliyekataa nyanyaso na dhuluma; akata kusimamia haki, amani na demokrasia ya kweli. Aliwahamasisha waafrika wengi kusimamia haki zao msingi, utu na heshima yao. Kama binadamu, historia ya maisha yake, iliandikwa pia kwa mapungufu yake ya kibinadamu, kiasi hata cha kunyanyasika mbele ya watu wake aliowapenda upeo, akatengana na mumewe Mzee Madiba waliokuwa wameshibana kwa dhati!

Mama Madikizela alitaka kuona haki sawa katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi nchini Afrika ya Kusini! Askofu William Slattery anasema Ijumaa Kuu, siku mbili kabla ya kifo chake, alipata nafasi ya masaa matano kukaa kimya Kanisani huku akitafakari maisha yake. Sasa apumzike kwenye usingi wa amani na abahatike kukutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye haki, huruma na mapendo, ili aweze kumkaribisha katika maisha ya uzima wa milele!

Kwa upande wake Rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa amekiri kwamba, kifo cha Mama Winnie Madikizela ni pigo kubwa kwa Afrika ya Kusini, kwani alikuwa ni kiungo kikubwa kwa wapigania haki, usawa na maendeleo ya wengi. Alikuwa ni sauti ya wanyonge na maskini. Umoja wa Afrika unaungana pia Afrika ya Kusini kuomboleza kifo cha Winnie Mandela. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres anasema, kwa hakika Winnie Mandela alikuwa ni mwanamke wa shoka dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, aliyesimamia haki msingi za binadamu. Ataendelea kukumbukwa kuwa ni Mama wa Taifa la Afrika ya Kusini. Alizalia tarehe 26 Oktoba 1936. Kunako mwaka 1990 akatalakiana na Mzee Madiba. Tarehe 11 Aprili, kutakuwa na Ibada ya Kitaifa na mazishi yake kwa heshima zote za kitaifa yatafanyika tarehe 14 Aprili 2018. Mama Winnie Madikizela Mandela, Apumzike kwa Amani, Amina.

Na Pauline Mkondya,

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.