2018-04-03 08:22:00

Papa Francisko: Tangazeni Fumbo la Pasaka kwa haraka na mshangao!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka, tarehe 1 Aprili 2018 amekazia mambo makuu matatu: Mbiu ya Ufufuko wa Kristo Yesu kama kiini cha imani ya Kanisa; Mariamu Magdalene akaenda mbio kwa haraka kutoa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo Yesu na tatu ni mshangao uliowakuta Mitume wa Kristo baada ya kushuhudia kwamba, kwa hakika Kristo Yesu alikuwa amefufuka kweli kweli! Hii ni tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu papo kwa hapo baada ya kuguswa na Liturujia ya Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, wazo la kwanza, ni mbiu ya ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni ushuhuda ambao Wakristo wa mwanzo wamerithishana kwa njia ya simulizi. Mwenyezi Mungu alipenda kuwashangaza waja wake kwa kuwajalia wanawake neema ya kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko, jambo ambalo linaonesha kwamba, kwa hakika, Mwenyezi Mungu anayo mambo mengi yanayowashangaza na kuwagusa watu kutoka katika undani wa maisha yao. Mbiu ya ufufuko wa Kristo imewashangaza walimwengu anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Wazo la pili, kadiri ya simulizi la Ufufuko wa Kristo kwa wafu, linaonesha jinsi ambavyo wanawake waliokuwa wamejihimu asubuhi na mapema kwenda makaburini, walivyoshuhudia kaburi wazi, wakaenda mbio kuwajulisha Mitume wa Yesu! Petro na Yohane wakatoka mbio kwenda kushuhudia tukio hili la ajabu, kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni, walipoambiwa na Malaika kuhusu Habari Njema ya kuzaliwa kwa Kristo, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu, wakaondoka na kuelekea Bethlehemu kwenda kushuhudia jambo kuu lililokuwa limetendeka!

Huu ndio mshangao uliomkuta yule Mwanamke Msamaria pale kisimani, alipotoka “nduki” kwenda kuwajulisha wananchi wa Samaria kuhusu ushuhuda uliotolewa na Kristo Yesu mintarafu maisha yake! Watu wakaacha shughuli zao, wakaondoka kwenda kushangaa kuhusu mbiu ya Habari Njema ya Wokovu. Haya ndiyo yanayotendeka hata leo hii kunapotokea matukio yasiyokuwa ya kawaida, watu wanavutika kwenda kushuhudia! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu unatolewa kwa haraka, ndiyo alivyofanya Andrea alipokwenda kumshirikisha Petro kwamba, wamekutana na kuonana na Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi!

Yesu ni mwema na anawatambua kwa undani sana Mitume wake, anawapatia nafasi ya kuweza kuonja huruma na upendo wake wa daima kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma, ambaye hakuamini katu katu, hadi alipoweka mkono wake kwenye Madonda Mtakatifu ya Yesu na kwa mshangao mkubwa akapiga kelele ya imani, “Bwana wangu na Mungu wangu.” Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu ni mwingi wa huruma na uvumilivu hata kwa wale wanaokwenda pole pole kwa mwendo wa “Kinyonga”! Hawa ni watu wa Mungu wasiokuwa na haraka katika maisha!

Wazo la tatu anasema Baba Mtakatifu ni: “Mbiu ya Pasaka” inayoleta mshangao mkubwa katika maisha ya watu wa Mungu! Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwauliza Wakristo ikiwa kama bado wanaguswa na mshangao wa Mungu katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Mitume Petro na Yohane waliotoka mbio kwenda kaburini, wakaona na kuamini! Petro Mtume, aliamini kwanza kwa shingo upande kutokana na kuchomwa sana na dhamiri kwamba, licha ya urafiki na uaminifu aliokuwa wamekirimiwa na Kristo Yesu, lakini akamsaliti na kumkana mara tatu kwamba, hamjui! Baba Mtakatifu anawauliza waamini Pasaka ya Mwaka 2018 wanafanya nini? Hii ni tafakari ambayo inaweza kuwaongoza waamini katika Kipindi hiki cha Pasaka!

Katika ujumbe wake wa Pasaka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” amekazia kwamba, Kristo Yesu Mfufuka ni tumaini la ulimwengu! Wakristo wanamwomba Mwenyezi Mungu ajalie amani duniani; upatanisho, matumaini, majadiliano, faraja kwa watu waliokata tamaa na wale wote wanaoteseka, kudhulumiwa na kunyanyaswa katika utu na heshima yao kama binadamu!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Pasaka amesema kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ni sawa na chembe ya ngano ambayo imekufa ili kutoa mazao mengi. Alisulubiwa, akafa na kuzikwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, kielelezo cha upendo wa Mungu unaomwilishwa hadi katika hatua ya chini kabisa, ili kuweza kuupyaisha ulimwengu, ili matunda yake yaweze kuonekana hata katika historia mamboleo inayogubikwa na ukosefu mkubwa wa haki msingi za binadamu, vita, kinzani na mipasuko. Kristo Mfufuka awakirimie walimwengu matumaini, utu na heshima mahali ambapo kuna umaskini na ubaguzi; mahali pale ambapo watu wanateseka na kufa kutokana na baa la njaa na ukosefu wa fursa za ajira. Kristo Mfufuka awe kati ya wakimbizi na wahamiaji wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kiasi hata cha kukataliwa, ili uwepo wa Kristo uwe ni faraja kwao! Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Kristo Mfufuka awe ni faraja na nguvu kwa waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.