2018-04-03 11:50:00

Makanisa Sudan ya Kusini yataendelea kuwa ni sauti ya kinabii!


Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini, SSCC., katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka kwa Mwaka 2018 linawataka viongozi wa Makanisa kushikamana kwa dhati kabisa na wananchi wanaoteseka kutokana na vita, njaa na kinzani za kijamii, ili hatimaye, waweze kuona mwanga wa Kristo Mfufuka katika maisha yao! Viongozi wa Kanisa waendelee kuwa ni vyombo vya imani, matumaini, upendo na mshikamano kwa watu waliokata tamaa ya maisha kutokana na vita, njaa na majanga mbali mbali ya maisha wanayokutana nayo kila kukicha!

Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini linakaza kusema, litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Viongozi wa Makanisa wanataka kuwa ni sauti ya kinabii kwa watu wanaoteseka kwa vita, mauaji na baa la njaa huko Sudan ya Kusini. Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini Mchungaji Peter Gai Lual Marro na Katibu wake Padre James Oyet Latansio kutoka Kanisa Katoliki, hivi karibuni walimtembelea na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Papa Francisko amewaambia kwamba, licha ya vikwazo vilivyojitokeza kiasi cha kushindwa kutembelea Sudan ya Kusini kama walivyokuwa wamepanga, lakini bado anayo nia thabiti moyoni mwake, kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu akipenda, atatembelea Sudan ya Kusini kama kielelezo cha mshikamano wake na familia ya Mungu Sudan ya Kusini inayoteseka sana kutokana na vita, baa la njaa na ukame wa kutisha! Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini, linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa kwa namna ya pekee na mahangiko ya familia ya Mungu Sudan ya Kusini!

Sudan ya Kusini iliyojipatia uhuru wake kwa “jasho la damu” kunako mwaka 2011, imeendelea kuogelea katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayofumbatwa katika uchu wa mali na madaraka kwa gharama ya raia wasiokuwa na hatia! Mateso yote haya ni sehemu ya Njia ya Msalaba kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini! Hii ni vita ya watu kujitakia wenyewe na kwamba, kunahitaji jibu makini ili kuondokana na mateso dhidi ya watu wasiokuwa na hatia! Viongozi wa Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini wanasema, vita hii ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu ambao umejitokeza kwa namna ya pekee kunako mwaka 2014. Vita na baa la njaa linakwamisha mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 5.5 wanaokabiliwa na baa la njaa na kwamba, wanahitaji msaada wa dharura. Zaidi ya wananchi milioni 7. 5 waliotawanyika sehemu mbali mbali za Sudan ya Kusini wanahitaji msaada wa kiutu!

Viongozi wa Makanisa wanakaza kusema, haki, amani na maridhiano ni njia pekee itakayoweza kukomesha majanga yanayowaandama wananchi wa Sudan ya Kusini. Watu wanatamani kuona amani inatawala, lakini wapi! Badala yake, mtutu wa bunduki unaendelea kuangamiza maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Baraza la Makanisa linapongeza juhudi za Serikali na wapinzani kutaka kukutanishwa pamoja nchini ya mwamvuli wa Makanisa kujadiliana, ili hatimaye, kuweza kufikia muafaka na amani kutawala! Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini linakaza kusema, litaendelea kusali, lakini hata wao wanapaswa kusikiliza na kujibu kilio cha amani kwa vitendo. Baraza la Makanisa litaendelea kuimarisha kanuni maadili na utu wema kwa kujikita zaidi katika maisha ya kiroho kama sehemu ya mchakato wa toba, wongofu wa ndani, msamaha na hatimaye, upatanisho wa kitaifa! Amani ni chachu na kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.