2018-04-03 08:42:00

Kanisa Katoliki Huko Mashariki kuanzia Mwaka 1917-2017


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake (1917-2017) limechapisha Kitabu kijulikanacho kama “Oriente Cattolico” yaani “Kanisa Katoliki huko Mashariki” ambacho kimegawanyika katika vitabu vikuu vitatu. Kardinali Leonardo Sandri, tarehe 24 Machi 2018 amemzawadia Baba Mtakatifu Francisko nakala yake. Toleo hili jipya linakuja baada ya miaka 43 tangu toleo la kwanza lilipochapishwa. Hii ni kazi kubwa ya kisayansi iliyotekelezwa na “Commissione Scientifica” yaani “Tume ya Sayansi Kimataifa” iliyokutana kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2017.

Kwa hakika anasema Kardinali Sandri haya ni matunda ya ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki na Kiwanda cha Uchapaji cha “Valore Italiano Editore”. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa taarifa muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki huko Mashariki. Hizi ni taarifa ambazo zimeboreshwa zaidi ikilinganishwa na toleo la kwanza lililochapishwa kunako mwaka 1974. Kitabu kinaonesha mabadiliko makubwa yaliyokwisha kutokea kwa Kanisa Katoliki huko Mashariki mintarafu uelewa na historia ya Kanisa.

Kitabu kimesheheni vitabu vya rejea vinavyoweza kutumiwa kwa ajili ya kufanya tafiti za kisayansi pamoja na kuonesha uwepo, maisha na utume wa Kanisa Katoliki katika Makanisa ya Mashariki, sehemu mbali mbali za dunia! Hiki ni chombo kinachotoa mwanga zaidi wa uwepo wa Ukristo katika Makanisa ya Mashariki sehemu mbali mbali za dunia, pamoja na changamoto mamboleo zinazopaswa kuvaliwa njuga ili kukuza na kudumisha maisha na utume wa Kanisa huko Mashariki. Kitabu hiki kinaweza pia kupatikana kwenye mitandao ya kijamii kwa anuani ufuatayo: www.orientecattolico.com.

Ni matumaini ya Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kwamba, kitabu hiki kitaweza kuzima kiu ya Makanisa mahalia, Parokia, Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu juu ya utajiri wa imani na tamaduni; furaha, mateso, mahangaiko na ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa njia hii wataweza kufahamika na kuthaminiwa zaidi katika maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia. Baada ya Pasaka, Kitabu hiki cha “Oriente Cattolico” kimeanza kupatikana madukani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.