2018-04-03 09:28:00

Bw. Abiye Ahmed ameapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia! Matumaini!


Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia Bwana Abiye Ahmed, mwenye umri wa miaka 42 ameapishwa  siku ya Jumatatu, tarehe 2 Aprili 2018 mbele ya Bunge la Ethiopia na sherehe hii kuhudhuriwa pia na wanasiasa kutoka katika vyama vya upinzani. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Ethiopia mwananchi kutoka kabila la Oromo ameteuliwa kuwa Waziri mkuu nchini Ethiopia, ambaye ameahidi kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na kupunguza matatizo ya mvutano wa kikabila usiokuwa na tija,  mvuto wala mashiko katika jimbo la Oromiya anakotoka. Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amempongeza Waziri Mkuu wa Ethiopia, Bwana Abiye Ahmed kwa kuonesha matumaini yake kwamba, Ethiopia sasa itaweza kuvuka matatizo na changamoto za kisiasa zilizokuwa zinahatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Wiki iliyopita muungano wa vyama vilivyo madarakani ulimteua Abiye Ahmed, afisa wa zamani wa ngazi ya juu katika jeshi la Ethiopia, kumrithi Hailemariam Desalegn, “aliyebwaga manyanga” ili kuleta mageuzi yatakayosaidia kukuza, kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa dhidi ya dhana ya ukabila iliyokuwa inaanza kuwapekenya wananchi wa Ethiopia kwa kubaguana na kutengana! Waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia Bwana Hailemariam Desalegn aliongoza tangu mwaka 2012 baada ya kifo cha Waziri mkuu Meles Zenawi.

Mkoa wa Oromiya unaozunguka mji wa Addis Ababa unakabiliwa na machafuko tangu mwaka 2015. Machafuko hayo yamesababishwa kwa kiasi kikubwa na hisia ya kubaguliwa, kutengwa na kubezwa kwa watu wengi kutoka kabila la Oromo, ambayo ina karibu theluthi moja ya wakazi milioni 100 wa Ethiopia. Machafuko katika jimbo la Oromiya yamekua ni tishio kubwa kwa ustawi, maendeleo na ustawi wa wananchi wa Ethiopia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.