2018-04-01 10:58:00

Wakristo ni wakati wenu kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka!


Kesha la Pasaka ni Mama wa makesha yote ya Liturujia ya Kanisa kwani humo ndimo Mama Kanisa anaadhimisha Fumbo la Pasaka, kiini cha imani yake. Kesha la Pasaka limegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ni: Kubariki Moto wa Pasaka, kielelezo cha ufufuko wa Kristo, mwaliko kwa watoto wa Kanisa kukesha katika: Sala, Neno la Mungu na adhimisho la Sakramenti za Kanisa ili kudumisha imani, matumaini katika ushindi wa Kristo Mfufuka. Ni ushindi unaoshuhudiwa kwa kubariki Mshumaa wa Pasaka na hatimaye, Mbiu ya Pasaka huimbwa ili kutangaza sifa za Mshumaa wa Pasaka, ambaye ni Kristo Yesu mwenyewe! Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno, ambamo waamini wanatafakari historia nzima ya ukombozi inayofumbatwa katika Agano la Kale linalopata utimilifu wake katika Agano Jipya kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Sehemu ya tatu ni Liturujia ya Ubatizo, ambamo waamini wanarudia tena ahadi zao za ubatizo na wakatekumeni walioandaliwa wanapokea Sakramenti za Kanisa.

Katika Kesha la Pasaka, Jumamosi, tarehe 31 Machi 2018 Baba Mtakatifu Francisko amewasha Mshumaa wa Pasaka kwa moto mpya ambao pole pole umelifukuza giza na kuwaangaza waamini waliokuwa wamehudhuria kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Mkesha wa Pasaka Mwanga wa Kristo Mfufuka katika utukufu unafukuzia mbali giza la moyo na roho, ili wote waweze kuishi katika mang’amuzi ya wanafunzi wa Emau: kwa kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa kwa Ekaristi Takatifu itakayoiwezesha mioyo yao kuweza kuwaka tena moto wa imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu ametoa Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu kwa wakatekumeni 8 kutoka: Albania, Italia, Perù, Nigeria na Marekani. John Francesco Ogah, kutoka Nigeria ni kati ya wale waliobahatika kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia ukimya mkuu uliojikita tangu mwanzo wa Kesha la Pasaka kama ilivyokuwa kwa Mitume, walipopigwa bumbuwazi na kukosa maneno mbele ya Fumbo la Msalaba. Ni ukimya uliotawala kwa kuangalia ukweli wa mambo, kiasi kwamba, kila Mtume alikuwa anasutwa na dhamiri yake kuhusu ukosefu wa haki uliopelekea hata Kristo Yesu, akahukumiwa, akateswa na hata kufa Msalabani. Walisutwa na dhamiri kwani walishindwa kumtetea Kristo Yesu pale aliposhutumiwa kwa uwongo; walipomwona akikamatwa na kuteswa Msalabani, wakamgeuzia kisogo, wakamkana na wengine kutimua mbio ili kusalimisha maisha yao!

Ni Kesha la Pasaka ambalo liliwachanganya Mitume wa Yesu hata wasijue ni nini cha kutenda kutokana na hatari kubwa iliyokuwa inawazunguka. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kushinda woga na hofu kwa kujizatiti kupigania haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya mazoea yanayozimisha Injili ya matumaini kiasi cha kuhalalisha mateso na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kama ambavyo Kayafa aliyekuwa Kuhani mkuu kwa wakati ule aliposema “Yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika kimya hiki kikuu, mawe yalianza kupiga kelele, Hayupo hapa! Amefufuka!” Mawe yakashangilia mwanzo wa maisha mapya na furaha ya Injili ikachipuka na kushika kasi, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki katika Injili ya matumaini kwa kuondokana na woga pamoja na hofu isiyokuwa na mashiko kwani Kristo Yesu, amefufuka kweli kweli!

Kaburi tupu anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko kwa waamini kuangalia changamoto za maisha, kujihoji na kuchukua hatua madhubuti, kwa kuamini na kujiaminisha mbele ya Mungu kwamba, daima yuko pamoja na watu wake katika hali mbali mbali za maisha yao na kwamba, mwanga angavu unaweza kupenya katika hali zote za maisha. Ufufuko wa Kristo Yesu ni tukio linalowashirikisha Wakristo wote katika kazi ya ukombozi, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayong’aa, nguvu na akili zinazopania kuamsha ari ya kusimama kidete katika kudumisha utu wa binadamu.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni mbiu inayo enzi matumaini yanayomwilishwa katika Injili ya upendo, ili, mang’amuzi haya yaweze kugusa udhaifu wa binadamu na kupyaisha imani ili kuwa na upeo mpana zaidi katika maisha! Ufufuko wa Kristo Yesu ni upyaisho wa matumaini yanayosimikwa katika ugunduzi ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko daima pamoja na kati ya watu wake! Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ni ushuhuda endelevu wa uwepo wa Mungu katika historia ya watu wake; kwa kumwachia Kristo Yesu kuamsha tena Injili ya matumaini yaliyokuwa yamefifia. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatekeleza dhamana na wajibu wake! Mawe yalipiga kelele, wanawake wakashuhudia na sasa ni wakati kwa waamini kuondokana na mazoea kwa kupyaisha maisha na vipaumbele vyao, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kweli kweli na amewatangulia Galilaya, kule ambako aliwaonjesha Mitume wake, pendo lake la kwanza na sasa anataka kuwaambia: “Usiogope! Nifuate!” Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyokamilisha mahubiri yake wakati wa Kesha la Pasaka, Mama wa Mikesha yote ya Liturujia ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.