2018-03-30 16:32:00

Ushauri wa bureee kwa wakleri kutoka kwa Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa ya Krisma ya Wokovu kwa kukazia umuhimu wa Mapadre kuwa ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu kwa watu wake kwa njia: majadiliano ya maisha ya kiroho, Sakramenti ya Upatanisho, mahubiri lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kielelezo makini cha uinjilishaji mpya, aliwagawia wakleri kitabu kilichoandikwa na Padre Diego Fares: Mambo kumi ambayo Papa Francisko anashauri kwa Mapadre. Baba Mtakatifu alipata chakula cha mchana na Maparoko kumi kutoka katika Jimbo kuu la Roma kwenye makazi ya Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwasikiliza wote waliomshirikisha maisha na utume wao kati pamoja na watu wa Mungu Jimbo Kuu la Roma. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka Maparoko hawa kuonesha ukaribu wa Mungu kwa watu wao pamoja na kuhakikisha kwamba, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanajisikia nyumbani wanapokuwa Kanisani!

Kitabu cha “Mambo kumi ambayo Papa Francisko anashauri kwa Mapadre” ni muhtasari wa mashauri makuu ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa kwa wakleri katika utume na maisha yao ya kiroho. Anawaalika wakleri kujishikamanisha na Kristo Yesu katika maisha yao, ili waweze kuwa na uwezo wa kuwahubiria na kuwashuhudia watu Habari Njema ya Wokovu inayogusa undani wa maisha yao. Wakleri wajitaabishe kuwafahamu watu wao kwa undani ili waweze kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu!

Baba Mtakatifu Francisko katika barua ya shukrani aliyomwandikia Padre Diego Fares anamshukuru kwa ujasiri aliouonesha kwa kuwahamasisha wakleri kutoka kifua mbele kwa ujasiri ili kuwahudumia watu wa Mungu. Haya ni maneno ambayo yanabubujika kutoka katika undani wa maisha na utume wake, kama vile Askofu anapozungumza na mapadre wake. Kitabu hiki ni ushuhuda wa mawazo makubwa ya Baba Mtakatifu wakati wa maisha na utume wake nchini Argentina na kwa sasa hapa Roma. Ni matunda ya utamaduni na sanaa ya kusikiliza, msaada na mang’amuzi ya miito, ili kuwawezesha wakleri kutokata tamaa na matatizo na changamoto za maisha wanazokutana nazo, bali kuendelea kuwa na ari na mwamko mpya katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha wakleri kutoka huko walikojificha kwenye Sakristia, tayari kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu walioko pembezoni mwa jamii. Hawa ndio watu wanaohitaji kuonjeshwa Injili ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwani Mwenyezi Mungu anataka kila mtu aweze kuokoka na kupata maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka Padre Diego katika maisha na utume wake ili kuwasaidia watu kugundua Uso wa Yesu katika uhalisia wa maisha ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kitabu hiki kitasaidia kuhamasisha miito ya kipadre na kitawa, pamoja na kuendelea kuwafunda walezi watakaojisadaka kwa ajili ya kuwasindikiza na kuwahudumia majandokasisi katika safari ya wito wao! Walezi hawa wasaidie kuganga, kuponya na kuwaongoza vijana katika njia ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.