2018-03-29 13:27:00

Papa: Ukaribu wa Mungu unafumbatwa katika: Neno, Sakramenti na Huduma


Mama Kanisa Siku ya Alhamisi Kuu anaadhimisha Karamu ya Mwisho, Kristo Yesu, usiku ule alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili na Damu yake Azizi, kama Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, Karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa na roho hujazwa neema, na ambamo waamini wanapewa amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani ya Kanisa katika kufikiri na kutenda! Alhamisi kuu Mama Kanisa anakumbuka pia siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja ambayo ina ngazi tatu: uaskofu, upadre na ushemasi. Huu ni ukuhani wa huduma ambao hutofautiana kiasili na ukuhani wa waamini wote.

Wahudumu wenye Daraja hutekeleza wajibu wao mbele ya watu wa Mungu kwa kufundisha, kwa ibada takatifu na kwa utawala wa kichungaji. Alhamisi kuu, Mama Kanisa pia anakumbuka pia siku ambayo Kristo Yesu aliweka amri ya upendo unaomwilishwa katika huduma, hasa kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Haya ndiyo Mafumbo makuu ya Kanisa yanayoadhimishwa, Alhamisi Kuu. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi Kuu asubuhi, tarehe 29 Machi 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameadhimisha Ibada ya Misa ya Krisma ya Wokovu kwa kubariki mafuta matakatifu ya Krisma, wagonjwa na ya wakatekumeni pamoja na wakleri kurudia tena ahadi zao kwa Kristo mbele ya Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa ukaribu wa Mwenyezi Mungu unaofumbatwa katika utume, kwani huu ndio ufunguo wa uinjilishaji, upendo wa Mungu kwa binadamu; majadiliano ya maisha ya kiroho; katika mahakama ya huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho na kwamba, ukaribu wa Mungu unafumbatwa pia katika mahubiri.

Baba Mtakatifu anasema, Kitabu cha Kumbu kumbu ya Torati kinaonesha ukaribu wa Mungu kwa watu wake. Alimpaka mafuta Daudi mtumishi wake, ili kuonesha ukaribu wake kama ambavyo umeshuhudiwa na Kristo Yesu aliposema, Roho wa Bwana yu juu yake kwa maana amemtia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema na kwamba, sehemu hii ya Maandiko Matakatifu imetimia ndani mwao! Yesu ni mjumbe na kiini cha Habari Njema ya Wokovu, kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa watu wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ndiyo elimu inayofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho, Utamadunisho pamoja na majadiliano kati ya vijana wa kizazi kipya! Ukaribu wa Mungu ni mwelekeo wa maisha ya mtu mzima unaonesha uwepo na utayari wa kusikiliza na kuwahudimia watu kama ilivyokuwa kwa Filipo aliyejisadaka kuwahubiria watu wa Uyahudi na Samaria na wote waliosikia Habari Njema wakajawa furaha kubwa! Filipo akajitoa bila ya kujibakiza kutangaza na kuwabatiza watu waliokuwa tayari kumwongokea Kristo Yesu katika maisha yao.

Ukaribu ni kiini cha uinjilishaji unaofumbatwa katika huruma ya Mungu kama ilivyoshuhudiwa na Msamaria mwema katika ukweli, uwazi na uaminifu wa kuwataja watu kwa majina na hali zao halisi bila kukwepesha macho! Ukweli wa Kiinjili uguse undani wa maisha ya watu ili kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, Kristo Yesu aweze kuwagusa, kuwaganga na kuwaponya. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Bikira Maria, Mama wa Mapadre, anaweza pia kuitwa kuwa ni Mama wa ujirani mwema anayeshuhudia ukaribu wa upendo wa Mungu kwa watu wake unaomwilishwa katika huduma makini kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana. Kanisa liwe makini kusoma alama za nyakati, ili kugundua mahali panapokosekana divai katika familia na tamaduni, ili kuweza kuzima kiu na matamanio halisi ya watu hawa!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wakleri kutafakari ukaribu wa Makuhani katika majadiliano ya maisha ya kiroho, katika Sakramenti ya Upatanisho na katika Mahubiri! Wakleri wawasaidie waamini wao kumwabudu Mungu katika Roho na kweli kama ilivyokuwa kwa yule Mwanamke Msamaria. Wawasaidie waamini kutambua dhambi na udhaifu wao, ili waweze kuguswa na ari na mwamko wa kimisionari, tayari waamini hao kuongoka na kuwa ni vyombo vya uinjilishaji. Yesu alimwezesha Mwanamke Msamaria kuendelea kuwa na ibada na wala hakumwekea kizingiti katika utume wake kama mmisionari.

Ukaribu wa Mungu unafumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, pale ambapo mwamini anapata nafasi ya kuzungumza ana kwa ana na Padre muungamishaji, bila kumhukumu mdhambi bali kumpatia nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu ili asitende dhambi tena, bali ajitahidi kuambata upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake. Kimsingi huruma na msamaha wa Mungu hauna kipimo kwa wote! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wakleri kutoa mahubiri yanayogusa sakafu ya maisha ya watu, kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro siku ile ya Pentekoste, kiasi kwamba, watu waliguswa na Neno la Mungu wakatubu na kumwongokea Mungu. Mahubiri ni kipimo madhubuti cha kuweza kutambua ni kwa kiasi gani mchungaji yupo karibu na watu wake na kwa kiwango gani anaweza kuwasiliana nao! Ni kielelezo na ushuhuda wa mhubiri kuwa karibu na Mungu katika sala na uhalisia wa maisha ya watu.

Wakleri wawe na unyenyekevu kama watoto wadogo, ili kumkimbilia na kumwambata Kristo Yesu katika maisha yao, ili kuwa na nguvu ya kimaadili wanapofundisha na kuwahudumia watu wao sanjari na kuwaonjesha upendo ule ambao umemfanya Yesu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya wokovu wa wengi. Ukaribu wa Mungu kwa waja wake unamwilishwa kwa Njia ya Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa kwa watu. Wakleri wawe karibu, pamoja na kati ya watu, kwa kutembea pamoja nao ili kuonja uwepo wa Mungu katika uhalisia wa maisha na wala si kwa njia ya mazoea. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaomba wakleri katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, kumkimbilia Bikira Maria Mama wa ujirani mwema, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo vya Yesu vinavyojenga na kudumisha umoja katika utofauti, ili hata katika utofauti wa mawazo, Bikira Maria aendelee kushuhudia uwepo wake wa kimama, kama alivyomkaribia daima Kristo Yesu katika maisha yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.