2018-03-28 08:35:00

Sikilizeni na kukijibu kilio cha Wakristo Mashariki ya Kati!


Mama Kanisa anawaalika watoto wake walioenea sehemu mbali mbali za dunia, kuhakikisha kwamba, wanaonesha ushuhuda wa imani hai, upendo na mshikamano wa dhati ili kujibu kilio cha mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu katika Nchi Takatifu, kwa kuchangia kwa hali na mali wakati wa maadhimisho ya Ijumaa Kuu, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1974 katika Waraka wake wa Kitume “Nobis in Animo” yaani “Kuhusu Mahitaji ya Kanisa katika Nchi Takatifu” anasema, Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu ni mashuhuda wa mahali patakatifu katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani. Hawa ni watu wenye upendeleo wa pekee machoni pa Mwenyezi Mungu na amana ya maisha ya kiroho kwa Wakristo wote.

Mwenyeheri Paulo VI anayetarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu mwaka huu, anaendelea kudadavua kwa kusema, watu hawa wanateseka sana kutokana na dhuluma, nyanyaso na ukatili wa kila aina; kielelezo hai cha mateso ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni watu wanaopaswa kuungwa mkono kwa sala na sadaka ili kuendelea kuthubutu kuishi katika maeneo haya matakatifu; kwa kupyaisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kumbe, “Mchango wa Ijumaa Kuu” unaotolewa na waamini sehemu mbali mbali za dunia ni ushuhuda wa mshikamano wa imani, mapendo na matumaini unaooneshwa na Wakristo, ili kuwategemeza jirani zao wanaoishi katika Nchi Takatifu.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ndilo limepewa dhamana na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, linaratibu Mchango wa Ijumaa kuu kila mwaka, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu, kielelezo na ushuhuda wa mshikamano wa Kanisa na Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, lakini zaidi wale wanaoishi katika Nchi Takatifu. Mchango huu unatumika kwa ajili ya kutunza maeneo matakatifu, malezi na majiundo makini ya wakleri, watawa na mihimili ya uinjilishaji katika ujumla wake bila kusahau huduma katika sekta ya elimu, afya, ustawi wa jamii na mendeleo endelevu. Fedha iliyokusanywa kwa mwaka 2017 ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 5, 531, 899, 22 pamoja na Euro 1, 423,251, 78.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki linasema, fedha hii imesaidia sana katika malezi na majiundo ya majandokasisi; mapadre, watawa na waamini walei kutoka Makanisa ya Mashariki wanaohudumiwa kadiri ya Sheria za Kanisa na Baraza hili. Fedha hii imetumika kwa ajili ya maboresho ya sekta ya elimu huko Mashariki ya Kati, ili kuwajengea watoto na vijana uwezo wa kupambana na hali yao ikikumbukwa kwamba, wengi wao ni wale wanaotoka katika maeneo ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini.

Baraza limetoa fedha kwa ajili ya huduma na utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji huko Mashariki ya Kati pamoja na Nchi za Misri, Ethiopia na Eritrea. Mchango huu, umeliwezesha Kanisa kuonesha mshikamano wa upendo na huruma kwa waathirika wa vita huko Iraq na Siria. Mchango huu, umekuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, kiasi hata cha kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa safari zisizokuwa na uhakika wa usalama. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 bado unaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowakirimia hifadhi wanapokuwa ughaibuni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.