2018-03-28 14:29:00

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa!


Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba.

Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Fumbo hili kwa muda wa Siku tatu kuu muhimu yaani: Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na hatimaye, Pasaka yenyewe! Jumatatu ya Pasaka ni mwendelezo wa sherehe ya Pasaka ya Bwana, hii ni siku ya familia na jamii katika kujenga umoja, mshikamano na mafungamano! Mama Kanisa anawahamasisha waamini kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha Sherehe hizi kama msingi wa maisha yao ya imani pamoja na kutambua dhamana na utume wao ulimwenguni. Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano kuu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kusherehea Siku kuu tatu muhimu katika maisha na utume wa Kristo Yesu unaoshuhudiwa katika historia.

Jumapili ya Pasaka, Kanisa linamshangilia Kristo Mfufuka kwa “Sekwensia ya Pasaka” yaani “Kristo Pasaka yetu aliyechinjwa sadaka, tumaini la watu wake amefufuka na amewatangulia mjini Galilaya. Kadiri ya Mapokeo, wakati wa Pasaka, watu wanasalimiana kwa maneno “Kristo Amefufuka”, ili kulitukuza Fumbo la imani ambalo ni chemchemi ya furaha na matumaini yanayowawajibisha waamini ili kushiriki kikamilifu katika utume wao ulimwenguni. Sherehe na mashangilio ya Pasaka ndani ya familia hayana budi kujikita katika hija, utume kwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka. Kwa njia ya Kerigma, Kanisa linainjilishwa, ili kuendelea kuinjilisha.

Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, anatoa muhtasari wa Fumbo kuu la Pasaka kwa kuwataka waamini kujisafisha kwa kutoa ile chachu ya kale, ili wapate kuwa donge jipya, kama vile hawakutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wao amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika Kesha la Pasaka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anatarajia kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa Wakatekumeni nane, watakao zawaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu, mwanzo wa maisha mapya ya Kikristo!

Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, wote wamehesabiwa haki, kwa vile wamefufuka katika Kristo Yesu, wanapaswa kuyatafuta na kuyaambata yale ya mbinguni, ushuhuda wa imani tendaji. Kwa wale waliozaliwa upya kwa kuuvua utu wao wa kale, wataweza kuhesabiwa haki mbele ya Kristo. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuondokana na unafiki katika maisha yao kwa kuishi na kutenda mema na pale wanapotumbukia dhambini, wawe na ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili hatimaye, wao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wale wanaoteseka na kudhalilishwa kwa utupu; wanaokosa mahitaji yao msingi, watu wanaoishi katika upweke na uvuli wa mauti. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa upya wa maisha ndani ya Kristo Yesu, Wakristo wanaweza kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini, alama ya maisha mapya na ufufuo. Wakristo wawe na ujasiri wa kumwachia Kristo Yesu, aweze kuosha na kutakasa macho ya imani, ili kuona na kutenda vyema, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Mfufuka.

Kwa kuishi vyema Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha ya Bikira Maria aliyefuatana na Mwanaye Mpendwa katika Njia yake ya Msalaba, akateseka sana pamoja naye hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba bila kumwonea aibu! Ni Mama ambaye, moyo wake ulisheheni furaha isiyokuwa na kipimo, kwa Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka wafu. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yawawezeshe waamini kushiriki kikamilifu ili waweze kupyaisha maisha yao! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote maandalizi na hatimaye, maadhimisho mema ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana! Wazazi wawasaidie watoto wao kumwona Kristo Mfufuka kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.