2018-03-28 09:38:00

Dumisheni neema ya Kipindi cha Kwaresima ili kukuza utakatifu!


Kwaresima ni kipindi cha kujitathimini iwapo mwanadamu anashirikiana na Mwenyezi Mungu katika mpango huu wa kuijenga Jumuiya ya mwanadamu yenye upendo, haki na amani kwa kushirikishana kila mmoja mapaji na ukarimu ambao Mwenyezi kamjalia kwa ajili ya mafao ya wengi: “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana (…) ili kusiwe na mgawanyiko katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe” (Rej. IWakorintho 12: 7;25). Inawezekana wapo wanaowanyanyasa na kuwatendea vibaya sana wanyonge kama vile kwenye biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mauaji, nyanyaso za ngono, dhuluma ya rasilimali na hazina kubwa kubwa na kadhalika. Lakini kila mmoja, kwa kila tendo dogo la uovu; na kwa kila tendo linalojikunyata na kurudi nyuma badala ya kutenda ukarimu, tunakuwa tunaendeleza kazi ile ile ya shetani. Kwa sababu hata mtu akiwa na mali nyingi kiasi gani, utajiri, maarifa, taaluma, vipaji na karama hata za kiroho, lakini kama hana upendo, basi yote ni bure, hayafai kitu (Rej., I Kor. 13:1-13).

Haidhuru ni tendo dogo kiasi gani, lakini kama ni tendo la chuki, kisilani, dhuluma, uchochezi, uchoyo na mambo kama hayo, bado tunaendelea kushiriki katika kuutesa mwili wa Kristo, na kubaki kwenye himaya ya shetani: “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wezi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi” (IWakorintho 6:9-10). Safari ya kipindi cha kwaresima, ni hija ya kiroho kwa lengo la kujitathimini ni namna gani kila mmoja anaendelea kushiriki akipelekea mateso ya mwili mmoja wa Kristo, ambao sisi tu sehemu, sisi wenyewe ni viungo vya mwili huo, lakini wakati huo huo tunasababisha mateso kati yetu.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 4 Februari aliagiza kutenga tarehe 23 Februari 2018, Ijumaa katika kipindi cha kwaresima iwe siku ya kufunga na kusali ili kuombea Amani duniani, na kwa namna ya pekee nchini Sudani ya kusini na Jamhuri ya Watu wa Congo, DRC. Nchi hizi ni kwa namna ya pekee tumeziwekea nia hiyo, lakini Amani inahitajika duniani kote, sababu mbali ya nyanyaso na dhuluma kubwa zinazowatesa watu katika nchi hizo, kuna sehemu nyingi tu ambapo wanyonge wananyanyaswa, wanadhulumiwa kwa mateso mengi katika Nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kidini, kimaadili na kadhalika.

Mfungo waweza kuwa ni chakula, kinywaji, muda au kitu kingine kinachoendana na tunu za kikristo. Kufunga kuna malengo maalumu. Kufunga ni kwa ajili ya kujinyima, ili kile ambacho mwamini angekitumia, akitoe kwa ajili ya wahitaji. Hivyo mfungo ambao haufikii lengo la kutumia kile tulichojinyima kwa kuwahudumia wahitaji tunakuwa hatujaupatia matunda stahiki mfungo huo.  Pili ni kuacha kujibovusha kwa anasa zinazoendekeza tamaa za kimwili na kupelekea mwanadamu kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa miili yetu ni hekalu la Mungu, tunapoibofusha miili yetu kwa tamaa na anasa tunamfukuza Roho wa Mungu ndani yetu, kwa sababu Roho wa Bwana anaishi katika roho, dhamiri na nafsi iliyo katika hali ya neema ya utakaso (Rej., I Kor. 6:12-20). Mwenyezi Mungu hategemi mwanadamu kuwa mkamilifu bila doa, lakini anategemea ule utakatifu katika hali ya kibinadamu, yaani uwezo wa kuchanganua na kufanya mang’amazui hiari ya kuikimbia dhambi.

Tatu, mfungo unamwezesha mwanadamu kuunganika kwa ukaribu na Mwenyezi Mungu, unamsaidia mwanadamu kujitathimini binafsi ni kwa namna gani anachangia mateso na mahangaiko ya wengine, na kupelekea kujitenga na utukufu wa Mungu. Hii inamsaidia kudhamiria kuachana na tabia hizo na kubadilika. Mwenyezi asema “sikufurahii kufa kwake mtu mwovu, bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya akaishi. Ghairini, ghairini mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa?” (Ezekieli 33:11.) Hatua ya nne sasa, ndio inakuwa kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sala ya rohoni na ya kweli. Hii ndiyo ibada halisi ambayo Mwenyezi Mungu anaihitaji kutoka kwa mwanadamu: “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu” (Yohane 4:23). Hii ni hatua inayomrudisha mwanadamu katika muunganiko wa kina na Muumba wake ili kuishi katika uwepo wa Mungu na kufaidika na Neema na utukufu wa Mungu.

Tunasali kwa malengo pia. Lengo la kwanza, ni kuwaombea wahanga wa mateso na dhuluma hizo wasivunjike moyo, bali wasimame imara katika Imani, wawe kweli mashuhuda wa Kristo kwa wadhalimu na watesi wao, kiasi cha wao kukiri na kuongoka. Yule jemedari alipoona uvumilivu na uaminifu wa Kristo; moyo ule wa msamaha, moyo wa kujitumainisha na kujiaminisha kikamilifu kwa mikononi mwa Mungu Baba: “Yule jemedari alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki” (Luka 23:47). Kukiri imani namna hii ni hatua ya kuongoka kwa watesi. Mungu amekuwa na subira ili wao pia wapate kuongoka, lakini iwapo hawatafanya hivyo, hukumu ya Jehanamu itawakumba: “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyodhani anakawia, bali huwavumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikie toba” (II Petro 3:9).

Lengo la pili ni kuwaombea watesi na wadhulumaji, na wote wanaotendea wengine ubaya wa aina yeyote wapate kuongoka. Iwapo sisi wenyewe tunakuwa tumefanya mfungo wa kweli, tunakuwa tumejitathimini na kubadili mwenendo wetu mbaya na kuifuata njia ya haki ya Mwenyezi Mungu, sala zetu zitakuwa na uwezo hata wa kupelekea wongofu wa waouvu, kwa sababu “sala yake mtu mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi” (Yakobo 5:16).  Tatu tunasali kwa namna ya pekee kuombea Amani. Lakini ni muhimu kufahamu kiini cha Amani tunayoiombea. Amani tunayoiombea ni Amani ya Kristo. Kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, angali akijua kwamba wanafunzi wake watateseka pia mbeleni, Kristo anawaambia: “Amani nawaachieni, Amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sio kama ulimwengu utoavyo” (Yohane 14:27).

Ulimwengu ukiongozwa na Ibilisi unaonesha amani kana kwamba inapatikana kwenye kumiliki mali nyingi, kuwa na madaraka makubwa, kufahamika sana duniani, kuendekeza kila aina ya tamaa. Fikra za namna hii ndizo zinazomfanya mwanadamu awe tayari kuua, kudhulumu, kunyanyasa kijinsia, kunyima watu haki, kutoheshimu utu, kutojali, kuchonganisha, kusemea vibaya, kusariti, kudanganya, rushwa, na kila aina ya uovu ili tu yeye atendaye hayo apate anachokitaka. Kwa sababu anadhani hayo yatampatia amani ya kweli. Ni kwa namna hii mwanadamu anavyoendelea kusambaza uovu duniani na kuvuruga Amani ya kweli.

Amani ya kweli ambayo Kristo anawapa wanadamu, ni kumtegemea Mwenyezi Mungu na kujiaminisha kwakwe kwa kufuata mapenzi yake. Mungu ndiye aliyeumba vitu vyote, na ni mapenzi yake kwamba mwanadamu avitunze, avitumie lakini kwa heshima na kujali wengine ili kila mmoja apate riziki yake na viumbe vyote viwe ni kwa manufaa ya wote (Rej., Mwanzo 1:28-30; Laudato sì 89-95). Lakini tamaa ya kutaka zaidi kuliko wengine na hofu ya kutokuwa na kitu fulani au hofu ya kutoridhika ndivyo vinapelekea mwanadamu kuipoteza Amani nafsini mwake na kuanza ghasia zinazoonekana kila siku. Mwanadamu amepoteza Amani ya Kristo. Bwana aseme “msisumbuke basi mkisema tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? Kwa maana hayo yote mataifa huyatafuta; Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6: 31-33). Hamaanishi watu wasifanye kazi, au wasitafute riziki; la hasha! anamaanisha mwanadamu aridhike na kile ambacho anakipata kwa halali. Kumbe tuombee Amani ya ndani, Amani katika nafsi ili kila mwanadamu aridhike na kilicho haki na halali kwa kila mmoja na sio kuendekeza tamaa.

Kwa wahanga wa mateso na dhuluma, tunawaombea kupokea yote kwa imani bila kukata tamaa na pengine wao kujiingiza katika uovu fulani, bali wasimame imara kwa kuutazama utukufu mkuu zaidi: “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu, kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu” (Warumi 8:18-19). Kwa kuwa Bwana anawatia moyo wanafunzi wake wabaki waaminifu “msiogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika Jehanamu” (Mathayo 10:28). Tuwaombee watesi na wote wenye kutenda aina yeyote ya ubaya ili wapate kuitambua Amani ya kweli ndani ya Kristo, wasivutwe na tamaa ya mwili, mali, mamlaka nk, bali waridhike na kile kilicho cha haki na halali kwao na kwa kila mmoja.

Mfungo wa tarehe 23 Februari 2018, ulikuwa na malengo hayo. Lakini Kanisa limetenga siku arobaini za kipindi cha kwaresima, kipindi cha mfungo na sala kwa namna ya pekee. Tupo huru kuchagua kila siku iwe ni mfungo na sala kwa ajili ya nia fulani. Na zaidi sana, haya yote yasiishie kipindi cha kwaresima, bali tuishi na kudumu katika sala ya rohoni na ya kweli; na kuepuka kuchangia mateso na dhuluma kwa wengine. Iwapo tunajitambua kuwa hekalu la Mungu, na iwapo tutaishi kweli kwa kuendana na roho na sio kwa tamaa za mwili, matunda yataonekana. Kwani ni kwa matendo ndipo tunafahamiana kama ni wema ama la!, kama vile mti hujulikana kwa matunda yake (Rej., Luka 6:43-45). Wale waishio kwa amani ya dunia, kwa kufuata udanganyifu wa Ibilisi huzaa matunda ya namna hiyo hiyo: “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mafarakano, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu” (Wagalatia 5:19-21). Wale wanaomwabudu Mungu katika roho na kweli, wataishi kwa kuongozwa na Roho wa Bwana, nao watazaa matunda ya roho. Na tunda la roho ni “upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi” (Wagalatia 5:22-23).

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.