2018-03-26 07:19:00

Tafakari ya Mateso ya Kristo Yesu kwa jicho la wanawake!


Ndugu msikilizaji, kwa kawaida hata kama kijana mwizi anakimbizwa, na kuzomewa na umati wa watu: “mwiziii! piga huyo! uulia mbali!” lakini utawaona wamama wanaficha nyuso zao na wanalia: “Jamani mwacheni msimpige! jamani tafadhali msimwue!” Hii ndiyo huluka ya akinamama karibu wote, ya upendo na ya kuonea huruma. Wanawake wa Kiyahudi kadhalika, walikuwa na kawaida ya kuwaonea huruma na kuwalilia wahalifu waliokuwa wanasindikizwa na askari kuelekea sehemu ya kutundikwa msalabani hadi kufa. Ndivyo hivyo ilivyokuwa Yerusalemu wakati askari wa kirumi walipomburuta Yesu aliyebeba msalaba kuelekea kusulubishwa kwenye kilima cha Golgota. Kulikuwa na wamama wengi kuanzia wale walikuwa wanamfuata wakati anafundisha, na wengine walijitokeza hapohapo kushuhudia wahalifu wanaopelekwa kusulibiwa. Wamama wengine walilia, wengine waliinamisha tu vichwa chini, wengine walishangaa wasijue kinachoendelea. Katika ibada ya njia ya msalaba tunawakuta akina mama katika vituo vitatu tofauti: Mama mzazi; Veronica na mabinti wa Yerusalemu. Hebu tuwaone kwa karibu akinamama hawa wote walichokifanya katika msafara ule wa kuteswa Yesu.

MABINTI WA YERUSALEMU: Kituo cha nane: Rej. Luka 23: 28-31.

Kadiri ya mwinjili Luka kikundi kimoja alichokutana nacho Yesu ni cha “Mabinti wa Yerusalemu”. Wanaitwa hivyo kwa vile walikuwa ni wazawa na wakazi wa Yerusalemu. Waliweza pia kuwa wahaji wanaouhusudu mji wa Yerusalemu. Kama kawaida yao wamama hawa, walivutwa na huruma wakaanza kumlilia Yesu kama vile angekuwa mtoto wao wa kuzaa. Ama kweli,“uchungu wa mwana anaujua mama.” Baada ya Yesu kuwaona akina mama hawa jinsi wanavyomlilia, tunategemea alitulizika katika mateso yake na kunyamaa. Lakini kinyume chake, anakusanya nguvu kidogo alizokuwa nazo, “akawageukia (wamama wale)”. Nadhani wamama walishtuka sana na kushangaa, “huyu kijana amepata wapi nguvu za kuweza hata kutugeukia sisi.” Aidha akaanza kuwawafundisha kama anavyotuandikia mwinjili Luka: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”” (Lk 23:28…). Makubwa hayo!

Ndugu zangu, lugha hii aliyotoa Yesu katika mazingira haya ya kwenda kufa ni nzito na ngumu kuielewa. Sidhani kama wamama wale walimwelewa Yesu anataka kusema nini. Hivi Yesu alitaka kuwaambia nini hawa wamama wanaomlilia kabla ya msiba? Ni dhahiri kwamba, Yesu hakutaka kuonewa huruma. Kumbuka alipokuwa na miaka kumi na miwili, alibaki hekaluni bila kumjulisha yeyote. Mama na baba yake walimtafuta siku tatu usiku na mchana. Walipofaulu kumkuta hekaluni kati ya majalimu, mama yake mzazi kwa uchungu alimwuliza mwanae: “Mwanangu ulikuwa wapi, baba yako na mimi tumekutafuta sana.” Lakini jinsi Yesu alivyojibu, hata mama yake hakuelewa. Nafasi nyingine ni pale Yesu alipokuwa Kafarnaumu anafundisha katika Sinagogi, mama yake alisikia kuwa yawezekana mtoto wake amerukwa na akili. Hapo mama akaondoka Nazareti na kutembea hadi Kafarnaumu ili kumjulia hali au hata kumchukua. Lakini Yesu akawaambiwa wale walioagizwa na mama yake kuja kumwita:“mama yangu na ndugu zangu ni nani?”.

Kumbe, hapa Yesu anataka kutuonesha kuwa ameshatoa uamuzi wa kumfuata Mungu Baba yake. Hatua aliyofikia sasa ni ya kwenda mbele siyo kurudi nyuma. Hata kama amehukumiwa kufa, yeye anao uhakika kwamba, yuko mikononi mwa Mungu. Aidha kwa mtindo huu wa majibu tunaweza kusema Yesu anataka kupiga selfi na mabinti hawa. Anawaalika wasimame pamoja naye kila mmoja aangalie kamera, yaani ayaangalie maisha yake binafsi na ulimwengu huu. Kwamba, inabidi wajichukulie mkononi hatima ya maisha yao. “Kila mtu atauchukua, mzigo wake mwenyewe.” Anawaita: “Enyi binti za Yerusalemu”. Anapoutamka mji huo, na wao ndiyo mabinti wa mji huo, waangalie hatima ya mji wao mpendwa wa Yerusalemu. Kwamba, mji huo wa Yerusalemu utakuja kushughulikiwa na Warumi, watauangamiza na halitasalia jiwe juu ya jiwe, yaani kutakuwa na maangamizi kwa Taifa zima la Waisraeli. Yesu analinganisha mateso na kifo chake msalabani na anguko la mji wa Yerusalemu na watu wake. Ukweli huo unadhihirika zaidi anaposema: “Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” (Lk 23:31). Yesu aliye bado ni kijana mbichi wa miaka thelathini na mitatu anajilinganisha na mti mbichi. Lakini anaulinganisha mji mkongwe wa Yerusalemu na mti mkavu unaoungua kirahisi zaidi kuliko mti mbichi. Kwa hiyo mabinti hawa wanapomwangalia Yesu, hawana budi wajifikirie na kujililia wenyewe kutokana na kivumbi kinachowasubiria wao wenyewe. Hii ndiyo selfi ambayo Yesu anawakaribisha kupiga nao na kuwahimiza wasimame sawasawa:“Mwenzako akinyolewa wewe tia maji.”

Maana hii ya maneno ya Yesu ni ya kihistoria. Lakini tunaweza pia kuyatafakari maneno hayo na kuyafsiri hata bila ya kupata mwongozo wa kihistoria. Maana yake tunaalikwa hata sisi tujipige selfi wenyewe pamoja na Yesu. Inatubidi tujiulize maneno hayo kwa mabinti hawa yana maana gani kwetu sisi, hasahasa kwangu mimi binafsi. Ninapoyatafakari mateso ya Kristu, hasa Juma kuu, ninapoadhimisha Misa takatifu au hata ninaposali kituo hiki cha njia ya msalaba maneno haya yana maana gani kwangu?

Suala la msingi hapa siyo la kumwonea huruma Yesu. Kwa sababu inafahamika wazi kama asemavyo Mwinjili Luka, kwamba: kwa kufa kwake Yesu, alijitoa kujikabidhi mzima mzima mikononi mwa Baba na akafufuka kutoka wafu. Lakini kifo cha Yesu kwangu mimi ni fundisho linaloweza kuniongoa. Kwamba inabidi nijililie mwenyewe na kujionea uchungu na kujutia dhambi zangu. Inabidi nichukulie kuteswa kwa Yesu hadi kufa kuwa kutanitukia mimi. Kama siwezi kutubu na kuongoka maisha yangu yatakosa maana na hayatakuwa na mwisho mzuri. Hapo ndipo nitakapokuwa kama mtu anayetafuta baiskeli ndani ya mifuko ya suruali. Yaani nitakapochanganyikiwa hadi kuiambia milima: “Niangukieni.” (Lk. 23:30). Kwangu mimi kifo cha Yesu ni fundisho linalonifungua macho na kunifanya nijiulize mwenyewe:  Maisha yangu yako sawa kweli? Itanitokea hata mimi kwamba kila kitu kitaniangukia? Basi nisitishike na lugha hii ya Yesu, bali nitaadharishwe kuwa mwangalifu. Kumbe kile maaskari wanachomfanyia Yesu, inabidi nijifanyie mwenyewe. Nijitese mwenyewe, nijiweke mwenyewe kiti moto, nijidharau mwenyewe, nijitemee mate mwenyewe, mimi ni askari kwa mimi mwenyewe.

Aidha kwa vile Mwinjili Luka alikuwa pia msanii, katika maana ya mchoraji. Umahiri wake unaonekana hapa anapotuchorea picha ya mateso ya Yesu unayoweza kuyafanyia tafakari na kujifikiria mwenyewe. Luka amemchora Yesu anayemwalika kila mmoja wetu binafsi kupiga naye selfi. Haya pata picha nzuri ya Yesu, mtu wa haki kweli ambaye inabidi nimfikirie na kumpigia taswira. Lakini katika picha hii ya pamoja ya safari ya Njia ya Msalaba yabidi nami niitambue pia njia yangu ya Msalaba katika maisha. Njia ya Yesu ya msalaba inanialika hata mimi kuamua kupita njia inayotakiwa. Kwa hiyo, ninaamua kumfuata Yesu katika njia yake ya Msalaba. Ama kweli njia yake ni ya upendo na ya mateso, ya imani na ya uhakika. Ukiliangalia kwa harakahara neno lile la Yesu kwa wale wamama linatia giza kweli, lakini pia linaweza kunionesha njia hii. Ee Mungu, uliyeweka mioyoni mwa akinamama wa Yerusalemu moyo wa ibada kwa Mwanao msulibiwa na ukawafanya wamfuate katika safari yake ya msalaba, utie ndani mwetu nia thabiti ya kumtumikia Mwanao kwa njia ya matendo ya huruma bila malipo.

VERONIKA: Kituo cha sita.

Katika wamama wengi sana waliokuwa katika msafara ule wa Yesu Injili inatuletea akinamama wale tu waliokuwa wanamlilia Yesu. Akina mama hao hawatajwi majina kwa hiyo mabinti wa Yerusalemu wanawawakilisha akinamama wote ulimwenguni. Lakini mapokeo yanatuambia kwamba kulikuwa pia na mwanamke mmoja aitwaye Veronika. Aliyemwonea huruma Yesu jinsi anavyoteseka, hasa hasa anavyotiririka jasho na damu usoni. Akavutwa kutaka kupiga naye selfi. Bila kuogopa askari wala macho ya watu katika msongamano ule yeye akaamua kujitoa mhanga, akajituma, akalipasua lile kundi “potelea mbali, la kuwa na liwe.” Akamkaribia Yesu na kumfuta damu na jasho lililokuwa linamtiririka usoni na kumpepea hewa baridi kidogo usoni kwa kitambaa chake.

Hapa tunaweza kufanya fikara zaidi juu ya ujasiri wa mwanamke huyu na juu ya kitendo hiki cha kumfuta Yesu jasho la damu na kumpepea. Kitendo hicho cha nje kinaweza kuonekana kama ni kidogo. Kumbe, ni kama kiyoyozi kidogo tu cha hewa lakini kinapenya majeraha ya kila siku, na kuturidhisha, ni nguvu na heshima na ibada. Ndiyo maana mapokeo yanasema, kuwa Veronika aliporudi kwenye kundi la wenzake alipokichungulia kitambaa alichotumia kumfutia Yesu jasho, akashtuka na kuona kuwa kina picha ya Yesu. Kumbe Yesu alijipiga selfi katika kitambaa cha Veronika. Akabaki na ukumbusho wa kudumu. Mungu anataka kutuamsha, kutujaza roho hiyo ya majitoleo binafsi, roho ya kuthubutu binafsi bila kuogopa kadamnasi kutenda mema na kumkiri Mungu. Kujasiri huku binafsi na kufanya matendo madogo ndiko kunaleta nguvu na pumzi inayoweza kutuvuta kwenda juu zaidi.

MAMA MZAZI: BIKIRA MARIA: MAMA WA MATESO: Kituo cha nne

Katika Mapokeo tunaambiwa kwamba kati ya wamama waliokuwa katika msafara wa Yesu kwenda Golgota kulikuwa pia na Bikira Maria mama yake mzazi. Katika matukio mengi yaliyomsibu Yesu, Mama Maria amekuwa karibu sana mtoto wake. Tukianza na Yesu akiwa bado mtoto, anampeleka kutahiriwa, akaishia kutabiriwa mambo yaliyomshtua moyo. Halafu tena Yesu akiwa na miaka miwili, alipotafutwa kuuawa na Herode. Maria na Yosefu wakamtorosha na kukimbia hadi Misri. Kisha Yesu alipobaki hekaluni siku tatu. Maria na mumewe Yosefu walisumbuka usiku na mchana kumtafuta. Kadhalika pale Maria alipomfungia safari kutoka Nazareti hadi Kafarnaumu ili kwenda kumwona. Kwa vyovyote katika mazingira haya nyeti ya kukamatwa mtoto wake mama yake mzazi asingekosekana. Aidha kwa vile mwisho wa wiki ile ni Pasaka ya Wayahudi, kwa vyovyote Maria alikuwa katika mazingira yale yale, kwa vile ilikuwa ni kawaida yake kufika Yerusalemu. Lakini tutamkuta Mama Maria anatajwa waziwazi na Wainjili akiwa chini ya msalaba.  Maria kamwe hakumwacha mwanae katika mazingira yote, ya furaha, ya kutatanisha na hasa ya kutia uchungu sana. Katika mazingira haya Mama Maria anatufundisha kutokukata tamaa na matumaini katika mazingira magumu. Wazazi wanaalikwa kuiga mfano wa Mama Maria wa kutowakatia tamaa watoto wao waliopeuka kimaadili na kuonekana hawawezekaniki. Wamwombe Mama Maria awaombee kwa Mwanae.

Tumwombe: “Ee Mama wa matumaini, umwombe mwanao atuhurumie, na ufike kututafuta mitaani na vichochoroni tulikojificha tukichanganya mambo. Wewe mama mvumilivu, utufundishe kusubiri fursa, nafasi ya Mungu na kutegemea alama zake zitakapojitokeza, yaani kusoma ishara za nyakati.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.