2018-03-26 12:33:00

Kongamano la Vijana Jimbo Katoliki Musoma, 2018


Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na "Vatican News" anabainisha umuhimu wa maadhimisho ya Kongamano la Vijana Jimbo Katoliki Musoma, linalofanyika wakati wa Juma kuu, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Huu ni muda muafaka wa kuwakumbusha vijana, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa kwani vijana: ni rasilimali ya nchi, imani, amani na kwamba, wao ni askari wa taifa. Mama Kanisa anawahamasisha vijana kulinda na kutunza ujana wao kwa kuuboresha kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kiimani.

Ujana mwema, utawawezesha huko mbeleni kufurahia uzee wao! Askofu Msonganzila anaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Kongamano la Vijana Jimbo Katoliki Musoma, ni muda muafaka kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kunadi: historia, maisha, utume na karama zao kwa vijana wa kizazi kipya wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani, bila kusahau kwamba, maisha ya ndoa na familia ni wito maalum, lakini kwa pamoja wanahamasishwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama wito wa wote! Ni muhimu sana ikiwa vijana wataendelea kubaki kuwa ni vyombo patanishi na shikamanishi katika mchakato mzima wa ujenzi na udumishaji wa Kanisa mahalia!

Askofu Msonganzila anaendelea kufafanua kwamba, Juma kuu, Mama Kanisa anapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ni muda muafaka pia wa kuwafunda vijana kutoka katika dini, madhehenu, mila na tamaduni mbali mbali Jimboni Musoma tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Vijana Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, miaka 33 iliyopita. Maadhimisho ya Mwaka 2018 katika ngazi ya Kijimbo yameongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito.”

Baba Mtakatifu Francisko analita Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kuwasilikiza vijana wa kizazi kipya, ndiyo maana hata Jimbo Katoliki Musoma linaendelea kuboresha sera na mikakati ya utume wa Kanisa kwa vijana kama ilivyobainishwa kwenye Programu ya Vijana Jimbo Katoliki Musoma. Kongamano la Vijana Jimbo Katoliki Musoma kwa mwaka 2018 linawashirikisha vijana kutoka: Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Tanzania, TYCS, na Umoja wa Vijana Wafanyakazi Tanzania, VIWAWA. Kanisa linajishughulisha zaidi na kanuni maadili, utu wema pamoja na maisha ya kiroho!

Jimbo Katoliki Musoma limewaalika wadau kutoka vikosi vya ulinzi na usalama kusaidia kuwafunda vijana ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa Amani, upendo, mshikamano na maridhiano katika jamii. Askofu Michael Msonganzila anakaza kusema, Jimbo Katoliki la Musoma, liko mpakani kati ya Tanzania na Kenya na mara nyingi vijana ndio wanahusika na ghasia na vurugu mpakani, kumbe, wanapaswa kufundwa ili kuheshimu utawala wa sheria, amani, utulivu na udugu kwa kutambua kwamba, dhana nzima ya ulinzi na usalama iko mikononi mwa raia wote! Kongamano katika ngazi ya Kijimbo ni majumuisho ya semina na warsha za vijana zilizofanywa kwenye ngazi ya Parokia na Dekania kwa kuwahusisha Mapadre walezi pamoja na viongozi wa vijana. Kongamano la Vijana Jimbo Katoliki Musoma linafanyika kwenye Kituo cha Matumaini ya Vijana Jimbo la Musoma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.