2018-03-24 13:30:00

Askofu Banshimiyubusa ateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Bujumbura!


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Evariste Ngoyagoye wa Jimbo kuu la Bujumbura, Burundi la kung'atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Gervais Banshimiyubusa, kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bujumbura. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Gervais Banshimiyubusa alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Ngozi, nchini Burundi.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Gervais Banshimiyubusa alizaliwa tarehe 9 Septemba 1952 huko Gisuru, Burundi. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, kunako tarehe 4 Julai 1981 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tarehe 10 Mei 2000, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mwandamizi wenye haki ya kurithi Jimbo Katoliki la Ngozi na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 16 Septemba 2000. Kunako tarehe 14 Desemba 2000, akarithishwa Jimbo Katoliki la Ngozi na sasa Baba Mtakatifu Francisko amemteua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bujumbura.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.