2018-03-23 14:00:00

Tafakari ya Njia ya Msalaba Ijumaa Kuu 2018 imetungwa na vijana


Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kwa mwaka 2018: ni mwaliko kutoka kwa vijana kwa Mababa wa Kanisa kusikiliza kwa makini kilio chao cha imani na mang’amuzi ya miito, na kukijibu kwa kuwaongoza na kuwasindikiza katika maisha yao, kwani, wanataka kumfuasa Kristo Yesu kama Bwana na Mwalimu, lakini bado wanayo hofu na machungu makubwa mioyoni mwao. Wanataka kuonja huruma na upendo wa Mungu ambao kimsingi ni chemchemi ya amani, huruma, msamaha na utu wema!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Ulimwenguni, ambayo kwa mwaka 2018 inaadhimishwa katika ngazi ya kijimbo kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” anawataka vijana kuorodhesha hofu na mashaka “yanayowakoroga” vijana katika maisha yao, tayari kujiaminisha mbele ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Anawataka vijana kuwa na kumbu kumbu ya historia yaok, kuwa na ujasiri wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao hadi kieleweke pamoja na kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko amewadhaminishwa vijana wa kizazi kipya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2018. Vijana wanatafakari maana ya haki, kashfa ya Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu; umuhimu wa kuwa mambo rejea katika maisha ya vijana; changamoto ya majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na mapambano ya maisha yanayowakabili vijana katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo na sayansi. Tafakari ya vijana hawa imeratibiwa na kuhaririwa na Professa Andrea Monda anasema Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Hizi zote ni jitihada za Mama Kanisa kutaka kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi mwezi Oktoba, 2018, lakini utangulizi wake unafanyika kuanzia tarehe 19 Machi 2018 na kuhitimishwa, Jumapili ya Matawi, Kanisa linapoadhimisha Siku ya Vijana Duniani na kwa Mwaka huu katika ngazi ya Kijimbo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kutafakari Fumbo la Pasaka: yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku.

Itakumbukwa kwamba, miaka mitano iliyopita, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa kuguswa sana na mahangaiko ya wananchi walioko huko Mashariki ya Kati, aliwaomba vijana kutoka Lebanon kwa kushirikiana na Patriaki Bèchara Boutros Rai kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, kwa kuonesha shida na magumu wanayokumbana nayo, imani na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake! Kwa upande wake, Professa Andrea Monda, hivi karibuni aliwakutanisha vijana wa kizazi kipya nyumbani mwake, kama ilivyokuwa kwa Mitume wakati ule walipokuwa wana sali na kungoja ujio wa Roho Mtakatifu, ili kupitia Maandiko Matakatifu na hatimaye, waweze kuishirikisha imani na matumaini yao yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Vijana hawa, kila mtu ameguswa kwa namna yake ya pekee kwanza kabisa na wahusika wakuu wanaotajwa katika Njia ya Msalaba, kiasi kwamba, imekuwa rahisi kwa vijana hawa kuweza kugawana Vituo 14 vya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Vijana wameguswa na mateso, mahangaiko na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka na kunyanyasika kiasi kwamba, wanavuliwa utu na heshima yao, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu pake Msalabani! Vijana wameonja ukakasi wa ukosefu wa haki msingi unaofanywa na vyombo vya sheria kama ilivyokuwa kwa Yesu, kuhukumiwa usiku wa manane.

Fumbo la Msalaba, limeendelea kuwa ni kizungumkuti kwa vijana wengi katika safari ya imani yao, lakini hatimaye, baada ya sala na tafakari ya kina wamegundua kwamba, Fumbo la Msalaba ni ufunuo wa hali ya juu kabisa wa huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele! Udhaifu wa mwili wa Yesu kutokana na mateso makali ni changamoto ambayo inawahamasisha vijana kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya, baada ya kuanguka na kutopea katika: matumizi haramu ya dawa za kulevya, fujo na ghasia, ukahaba na mambo yale yote yanayochafua sura na mfano wa Mungu katika maisha yao.

Vijana wanaona kwamba, Fumbo la Ufufuko ni mwanzo wa maisha na matumaini mapya hata katika safari yao ya ujana, ambao ni kazi kweli kweli, kwani huu ni wakati wa kuponda mali, kufa kwaja, na kusahau kwamba, fainali ni uzeeni! Kuna mateso, mahangaiko na changamoto zinazowakumba katika maisha, lakini vijana daima wakumbuke kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wana utu na heshima yao kama binadamu! Vijana wanaogopa kifo! Wasingelipenda kukabiliana mubashara na Fumbo hili katika ujana wao! Lakini huu ni ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho, kumbe, wanapaswa kujiandaa kikamilifu ili kulipokea Fumbo la Kifo kwa imani na matumaini thabiti! Kutokana na hofu ya mateso, magonjwa na kifo, vijana wanawaomba Mababa wa Kanisa kuwasikiliza, kuwaongoza na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, bila ya kuwahukumu wala kuwabeza; kwani maisha ya ujana ni kazi kweli kweli! Kimsingi, Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kwa mwaka 2018 ni muhtasari wa shida, changamoto na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.