2018-03-23 14:52:00

Ratiba elekezi ya Papa Francisko katika maadhimisho ya Juma kuu, Roma


Baba Mtakatifu Francisko, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya Matawi, tarehe 24 Machi 2018 sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” Lk. 1:30. Ibada itaadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:00 kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu atabariki matawi na baadaye kuongoza maandamano kuelekea katika maadhimisho ya Misa ya Mateso ya Bwana.

Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu ambao utakamilishwa kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Juma Takatifu.

Tarehe 29 Machi 2018, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu. Ibada hii itaadhimshwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu atabariki Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa na pamoja na Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapoweka wakfu kama mapadre na maaskofu. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekarissti Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbu kumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai!

Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu inayoadhimishwa na Mama Kanisa hadi Kristo Yesu atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti Pacha na Daraja Takatifu ya Upadre. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakitenda kwa nafsi ya Kristo, wakitangaza fumbo lake pamoja na kuyaunganisha maombi ya waamini pamoja na sadaka ya Kristo Msalabani inayoadhimishwa katika Ibada ya Misa Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, na kadiri ya utaratibu wake, tarehe 29 Machi 2018, majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Karamu ya Bwana, kwenye Gereza kuu la “Regina Coeli” lililopo mjini Roma. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na kusalimiana na wafungwa wagonjwa na baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwaosha miguu wafungwa 12, kielelezo cha upendo wa Kristo unaomwilishwa katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baadaye, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na wafungwa katika eneo la VIII la Gereza kuu la “Regina Coeli”.

Tarehe 30 Machi 2018 Mama Kanisa anaadhimisha Ijumaa kuu, yaani kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuanzia saa 11:00 jioni majira ya Ulaya kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kuanzia saa 3:15 Usiku kwa saa za Ulaya, baba Mtakatifu Francisko ataongoza Njia ya Msalaba, mwishoni atatoa neno na kuwappatia waamini baraka yake ya kitume. Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kwa mwaka 2018: ni mwaliko kutoka kwa vijana kwa Mababa wa Kanisa kusikiliza kwa makini kilio chao cha imani na mang’amuzi ya miito, na kukijibu kwa kuwaongoza na kuwasindikiza katika maisha yao, kwani, wanataka kumfuasa Kristo Yesu kama Bwana na Mwalimu, lakini bado wanayo hofu na machungu makubwa mioyoni mwao. Wanataka kuonja huruma na upendo wa Mungu ambao kimsingi ni chemchemi ya amani, huruma, msamaha na utu wema!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Ulimwenguni, ambayo kwa mwaka 2018 inaadhimishwa katika ngazi ya kijimbo kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” anawataka vijana kuorodhesha hofu na mashaka “yanayowakoroga “vijana katika maisha yao, tayari kujiaminisha mbele ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na kumbu kumbu ya historia yao, ujasiri wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao hadi kieleweke pamoja na kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko amewadhaminishwa vijana wa kizazi kipya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2018.

Jumamosi Kuu tarehe 31 Machi 2018 majira ya saa 2:30 Usiku kwa Saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza “Kesha la Pasaka” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Atabariki moto wa Pasaka na kuongoza maandamano kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na baadaye itaimbwa “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Jumapili ya Pasaka ya Bwana, tarehe 1 Aprili 2018 saa 4:00 asubuhi majira ya saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye atatoa baraka zake za kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini Urbi et Oribi”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.