2018-03-22 08:56:00

Papa Francisko kushiriki maadhimisho ya Siku IX ya Familia, Dublin


Mama Kanisa kuanzia tarehe 21 hadi 26 Agosti, 2018 ataadhimisha Siku ya IX ya Familia Duniani, Jimbo kuu la Dublin nchini Ireland, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu”. Siku hii inapania kuwa ni maadhimisho ya chemchemi ya furaha ya Injili ya familia kwa walimwengu, kwa kumshukuru Mungu kwa kuwajalia wanadamu uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaofumbatwa katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo! Huu ni upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku, bila kusahau changamoto na mapungufu yanayomwandama mwanadamu! Bila upendo huu, si rahisi sana kuweza kuishi kama watoto wa Mungu, watu wa ndoa, wazazi na kama ndugu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake Jumatano tarehe 21 Machi 2018 ametangaza nia yake ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani na kwamba, atakuwa na hija ya kitume Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland kuanzia tarehe 25-26 Agosti 2018. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa na Serikali wanaoendelea kujibidisha katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani. Baba Mtakatifu amepata pia fursa ya kubariki na kusali mbele ya Sanamu ya Familia Takatifu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuhimiza umuhimu wa familia kuishi kwa kujikita katika upendo kwa ajili ya upendo na ndani ya upendo wenyewe.

Hii ina maana kwamba, wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana. Anawaalika wanafamilia kumwilisha ndani mwao maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga tabia ya unyenyekevu uliopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua, kuwaingiza na kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho na ushuhuda wa mradi mkubwa wa upendo wa Mungu kwa binadamu unaofumbatwa katika Injili ya familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.