2018-03-20 16:04:00

Patriaki Daniel wa Romania: Bebeni Msalaba wa maisha yenu kwa imani


Mfanyeni Kristo Yesu kuwa ni kitovu cha maisha yenu; ndiyo ujumbe kutoka katika mahubiri ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima yaliyotolewa na Patriaki wa Kiorthodox Daniele wa nchini Romania. Patriaki Daniele akijikita kutazama juu ya ishara ya mateso ya Kristo na jinsi gani ya kuwa na  uaminifu mwema, amefafanua  juu ya utofauti ya sikukuu ya “kutukuka kwa msalaba”, inayoadhimishwa tarehe 14 Septemba ya kila mwaka   na  Injili inayosomwa katika Domenika ya tatu ya kwaresima, kwamba haitazami kusulibiwa kwa Yesu tu,  bali  kwa namna ya pekee kwa kila mkristo, anapaswa kuubeba msalaba na kuuona mwanga huo katika matendo matakatifu ya msalaba kwa maisha ya kiroho binafsi.

Ili kuwa mkristo mwema ni lazima kubeba majukumu na kujikana binafsi, kuuchukua msalaba na kuiga mfano ya Kristo. Lakini kujikana binafsi haina maana ya kujiharibu, bali kuwa huru na kuondokana na kuishi maisha ya  ubinafsi. Mara nyingi tunaishi ubinafsi,kwa kufikiria kulimiki  mali zaidi, kutaka utukufu, kutaka kuwa na uwezo na kutaka kuishi maisha ya anasa. Lakini Yesu anasema, ni lazima kujikana kila siku ikiwa na maana ya kuacha matakwa yako binafsi ya kutaka kujitosheleza binafsi  ili kuweza kufikia hatua ya kumweka Kristo awe kitovu cha maisha yetu.

Patriaki Daniele akiendeleana tafakari lake anasisitiza kuwa, kujikana binafsi maana yake ni kujikabidhi moja kwa moja na kuacha kujifikiria binafsi, ukidharau Mungu na watu ambao wanahitaji msaada wetu na kwa maana nyingine kujikana binafsi ni tabia ya kujifungua  wazi ili uweze kuwa na  muungano na Mungu na jirani, kuishi maisha ya  upendo mnyenyekevu kwa Mungu na upendo wa huruma kwa ajili ya wengine. Ili uweze kuubeba msalaba lakini ni mapambano anasisitiza, ili uweze kushinda mateso yako kwa matumaini.

Ni mapambano kwa ajili ya kushinda matatizo tuliyo nayo na kukaribia zaidi Mungu, kugeuza changamoto za maisha ili kufikia ngazi ya  juu kiroho. Lakini yote hayo yawezekana  kwa msaada wa Mungu. Ni kwa njia ya neema yake tu, tunaweza kuishi na kujifungua hadi kuhisi furaha ya kweli  na si kuona kama vile mzigo; na tunaweza kutambua kuwa na umoja na Kristo kwa njia ya sala, hasa zaidi katika Ekaristi ambayo inatupatia nguvu ya kubeba msalaba tuweze kufurahia ufufuko wake. Patriaki ametoa mfano kuwa: kama ilivyo kawaida ya mfalme aliye shinda vita  hutuma kwanza bendera yake katika mji alio ukomboa, na  ndiyo  hiyo ishara ya ushindi wa  Kristo dhidi ya dhambi, mauti na giza anayo watumia wale wote waliofunga ili waionapo ishara hiyo wapate nguvu zaidi.

 Anahitimisha Patriaki wa Kiorthodox Daniele kwamba, sisi sote tunao jitahidi kushinda dhambi za ubinafsi, mapambano dhidi ya uchu, kiburi na ya kumkana Mungu, hatuna budi kutazama kwa dhati ishara hiyo ya ushindi wa Kristo.  Vilevile na kutazama Msalaba Mtakatifu unaotupatia nguvu katika mapambano ya kiroho na kulainisha mahitaji yetu, unatoa utamu dhidi ya uchungu na kutupatia faraja!

Sr Angela Rwezaula 
Vatican News

 








All the contents on this site are copyrighted ©.