2018-03-19 08:39:00

Papa Francisko: Wazazi igeni mfano bora wa Mtakatifu Yosefu


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, tarehe 19 Machi 2018, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu, sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitano tangu aanze rasmi utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anapenda, wanaume wote, siku kuu njema. Anawataka wawe mfano bora wa kuigwa kwa watoto wao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu. Wajizatiti katika mchakato mzima wa ukuaji wao katika kimo, hekima na neema, daima wakimpendeza Mungu.

Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria inapata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu. Yosefu ni mtu wa mwisho kuzungumza na Mwenyezi Mungu kwa njia ya maono na ndoto katika Agano Jipya. Yosefu ni mtu mwaminifu na mwenye haki ambaye ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi na msimamizi wa nyumba yake. Yosefu ni kiungo muhimu sana kati ya Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa dunia, kwani amezaliwa kutoka katika ukoo wa Yakobo na Daudi mtumishi wa Mungu.

Yosefu, mtu mwaminifu na mwenye haki, ndiye Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Yesu. Mwenyezi Mungu alimpatia dhamana na wajibu wa kuitunza na kuilinda Familia Takatifu; akamwokoa Mtoto Yesu dhidi ya upanga wa Mfalme Herode kwa kumkimbiza na kumpatia hifadhi nchini Misri na hatimaye, akamrejesha tena kutoka uhamishoni Misri na kutua nanga mjini Nazareti. Papa Pio IX akamtangaza kuwa msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Yohane XXIII akaingiza jina la Mtakatifu Yosefu katika Kanuni ya Kirumi. Hii pia inajulikana kama Siku kuu ya wanaume, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko amewatumia salam na matashi mema, wanapoadhimisha siku yao, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watoto wao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.