2018-03-19 10:24:00

Kardinali Baldisseri asema, inapendeza sana kuwasikiliza vijana!


Wazazi wanayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili kwa watoto wao, kwa kutambua kwamba, wao, ni waalimu na makatekista wa kwanza wa imani, maadili na utu wema, mambo msingi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazazi na walezi wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na malezi makini kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kujenga mshikamano na mahusiano ya karibu zaidi na watoto pamoja na vijana wao. Familia ni mahali pa kwanza kabisa pa kutakatifuza maisha, kwani, wazazi na walezi wanashiriki kwa namna ya pekee, katika kazi ya uumbaji na malezi ili kukoleza mchakato wa ujenzi na ukomavu wa utu wema, uaminifu, uzuri, moyo wa huduma na sadaka; upendo na mshikamano wa dhati; mambo muhimu sana katika maisha na utume na vijana wa kizazi kipya!

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, hivi karibuni, amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wazazi,walezi na vijana huko Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, nchini Italia. Mkutano huu uliandaliwa na Jumuiya ya Papa Yohane XXIII. Hii sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 3-28 Oktoba, 2018, lakini kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko, utangulizi wa Sinodi hii inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito” unaanza rasmi, tarehe 19 Machi 2018 na kuhitimishwa na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2018 katika ngazi ya kijimbo.

Kardinali Baldisseri anasema kwamba, utamaduni wa kukutana, kuwasikiliza, kuwajali, kuwasindikiza na kuwaimarisha vijana katika imani, matumaini na mapendo ni utamaduni na sanaa ya hali ya juu kabisa inayopania kupyaisha uso wa Kanisa la Kristo ili liweze kupambwa na kung’ara kwa tunu za ujana. Ni mchakato unaopania pamoja na mambo mengine, kuendelea kuibua sera, mbinu na mikakati ya maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Anakaza kusema, inapendeza kuwasikiliza vijana wakishirikisha: furaha, matumaini, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika uhalisia wa maisha yao.

Huu ndio wakati uliokubaliwa kwa Mama Kanisa kujizatiti zaidi katika utamaduni wa kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao, tayari kuwajengea uwezo wa kufanya hata maamuzi magumu katika wito na maisha yao, tayari kumfuasa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Vijana wanawahitaji watu watakaowasikiliza, watakaowathamini na kuwapatia ushauri wa kina wakati wa shida na mahangaiko yao ya ndani; wanapokumbana utupu katika maisha ili hatimaye, waweze kusindikizwa na hatimaye, kuuona mwanga katika njia ya maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anakazia mambo makuu matatu kama sehemu ya mang’amuzi ya maisha ya mtu binafsi: kwanza kabisa ni: kujitambua, kutoa tafsiri na kuamua. Haya pia ni mambo msingi yanayoweza kuwasindikiza vijana katika safari yao ya maisha hapa duniani. Vijana wanapaswa kusaidiwa ili kuuona mwanga katika maisha yao, kwa kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na matukio mbali mbali ya maisha. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, hawana na kamwe hawataweza kuwa na majibu yote katika matatizo na changamoto za maisha ya ujana wao. Kutokana na ukweli huu, vijana wanapaswa kupewa ufunguo sahihi wa kuweza kutafsiri matukio na changamoto hizi katika maisha ili hatimaye, kufanya uamuzi sahihi na makini katika maisha. Kardinali Baldisseri anawataka wazazi na walezi wa vijana kuwasaidia vijana kuwa na mang’amuzi sahihi ya maisha na wito unaobubujika kutoka katika undani wao, kwa kuzingatia dhamiri nyofu na hai, ili kutambua chanzo cha wito huu na matokeo yake katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.