2018-03-19 09:54:00

Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha: huruma, upendo na maisha mapya!


Injili ya Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima ni simulizi la maadhimisho ya Siku kuu ya Wayahudi, iliyowakusanya waamini wakiwemo Wayunani waliotaka pia kumwona Yesu baada ya kusikia maneno yake ya kinabii na matendo makuu aliyokuwa akitenda katika maisha yake. Wayunani walitaka kumwona Yesu na hapa Mwinjili Yohane anasema, kumwona Yesu ni kumwamini, kiasi hata cha kuweza kugusa undani wa mtu! Jibu linalotolewa na Kristo Yesu linawashangaza wengi, kwani anaanza kuzungumzia kuhusu “Saa yake” iliyokuwa imewadia, ili atukuzwe Mwana wa Adamu.

Yesu anawaambia kwamba, mtu anayetaka kumwona, yaani kumwamini kwa dhati kabisa hana budi kumwangalia ndani kabisa ya Fumbo la Msalaba, ambalo linafunua utukufu na ukuu wake kama Mwana wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuyainua macho yao juu ya Msalaba wa Kristo ili kumtafakari na hatimaye, kumfahamu Kristo Yesu. Kwa bahati mbaya, Msalaba umekuwa ukitumiwa na baadhi ya watu kama mapambo tu, lakini kwa waamini, Msalaba ni ufunuo wa Fumbo la Mateso na Kifo cha Mwana wa Mungu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo, chemchemi ya maisha mapya na wokovu kwa binadamu wa nyakati zote! Kwa njia ya Madonda yake Matakatifu, watu wote wamepata kuponywa!

Hii ni tafakati iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 18 Machi 2018 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulitafakari Fumbo la Msalaba linaloonesha sadaka na majitoleo ya Kristo Yesu hadi kifo cha aibu! Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia undani wa Fumbo la Msalaba. Ibada kwa Madonda Mtakatifu ya Yesu, iwawezeshe waamini kuzama katika Moyo wake Mtakatifu, ili kujifunza na hatimaye, kutambua Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu; Ukuu na Hekima ya Msalaba.

Yesu alitumia nafasi hii anasema Baba Mtakatifu, ili kudadavua kuhusu maana ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu kwa mfano wa chembe ya mbegu inayoanguka ardhini, ikafa na hatimaye, kutoa mazao mengi. Kumbe, Fumbo la Msalaba ni chemchemi ya maisha mapya. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu ameweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo na hivyo, kumkirimia maisha mapya yanayopatanishwa katika upendo. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amelipa fidia ya wengi, hiki ndicho kiini cha Fumbo la maisha ya Yesu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujizatiti kikamilifu katika kumwilisha sheria hii ya Pasaka katika maisha yao, kwa kujisadaka ili kuondokana na ubinafsi, tayari kuona, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na jirani wanaohitaji msaada zaidi. Ni mwaliko wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Injili. Lengo ni kujenga na kudumisha udugu na ukarimu; kwa kuona, kutafakari na hatimaye, kuguswa na upendo na huruma inayobubujika kutoka katika Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria alibarikiwa kuelekeza moyo wake kwa Mwanaye wa pekee, tangu alipozaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama kule mjini Bethlehemu hadi alipomwona akiinama kichwa na kukata roho pale Mlima Kalvari, awasaidie waamini kukutana na kumtambua Kristo Yesu, jinsi kama alivyo, ili waweze kuangaziwa na hatimaye, kupeleka matunda ya haki na amani ulimwenguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.