2018-03-19 14:48:00

Askofu mkuu Lèon Badikebele ateuliwa kuwa Balozi nchini Argentina


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Lèon Kalenga Badikebele kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Argentina. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Badikebele alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini El Salvador, Belize na Antilles. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Kalenga Badikebele alizaliwa kunako tarehe 17 Julai 1956 huko Kamina, nchini DRC. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 5 Septemba 1982 na kuingizwa Jimboni Luebo, DRC. Alianza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe 27 Februari 1990. Tangu wakati huo, akatumwa kutekeleza dhamana na utume huu huko nchini Haiti, Guatemala, Zambia, Misri, Zimbabwe na Japan kwa nyakati mbali mbali.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe 1 Machi 2008 akamteuwa kuwa Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu Mei Mosi, 2008 na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati ule na kutumwa kwenda nchini Ghana kama Balozi wa Vatican. Tarehe 22 Februari 2013, akateuliwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini El Salvador, Belize na Antilles. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Machi 2018 akatemteua kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Argentina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.