2018-03-17 09:21:00

Vijana pia ni wahanga wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika vijana kumsikiliza Roho Mtakatifu anayezungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu. Anawataka kupaaza sauti zao ili ziweze kusikika katika jamii na Kanisa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu ametangaza kwamba, kuanzia tarehe 19 Machi 2018 Sherehe ya Mtakatifu Yosefu mchumba wake Bikira Maria hadi tarehe 24 Machi 2018, kutaadhimishwa “Utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu” kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii ni safari ya maisha ya Kanisa katika kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana, kuwajali, kuimarisha imani pamoja na kusikiliza changamoto zinazotolewa na vijana wa kizazi kipya. Hitimisho la maadhimisho haya litawasilishwa kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa rasmi mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican. Vijana wanategemewa kuwa ni wahusika wakuu katika maadhimisho haya!

Hivi karibuni, kijana Maria Magdalene Savini kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, alimwelezea Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana ni kati ya waathirika wakubwa wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Kutokana na hali ngumu ya maisha, vijana wengi wamejikuta wakiwa pembezoni mwa jamii, hali inayowakatisha tamaa ya maisha. Matokeo yake vijana wengi hasa walioko pembezoni mwa jamii: wamegeuzwa kuwa ni wahanga wa biashara haramu ya viungo vya binadamu, ukahaba na utalii wa ngono, kazi suluba pamoja na kutengwa na jamii. Kutokana na umaskini wa familia wanamotoka, idadi kubwa ya vijana hawana fursa ya kupata elimu bora inayotolewa ndani na nje ya nchi zao. Vijana ni wahanga wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kiasi hata cha kutumiwa kwenye mashambulizi na vitendo vya kigaidi, hali inayowafanya vijana kushindwa kuheshimiana na kuthaminiana na matokeo yake ni uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, amani na mafungamano ya kijamii. Kimsingi vijana wengi hawana uhakika wa usalama wa maisha yao kwa siku za usoni, ndiyo maana hata wakati mwingine, wanashindwa kufanya maamuzi mazito na machungu katika maisha kwa kukosa msingi thabiti wa imani, matumaini na mapendo! Maria Magdalene Savini kwa uchungu mkubwa, amemwomba Baba Mtakatifu Francisko kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu pamoja na kuendelea kujizatiti kupambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Viongozi wa kisiasa, kidini pamoja na watunga sera, wawe mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu na mahitaji yake msingi na kwamba, haki, amani na maridhiano kati ya watu ni mambo msingi katika ujenzi wa jamii inayoheshimiana na kuthaminiana; jamii inayosimikwa katika ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati. Amemwomba Baba Mtakatifu Francisko kuwapatia vijana ushauri wa kina wa jinsi ya kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko amejibu kwa kufafanua kwamba: umaskini, vita, rushwa na ufisadi pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya kutosha katika utekelezaji wa huduma msingi kwa jamii ni chachu inayoshamirisha: biashara ya binadamu na utumwa mamboleo; kukua na kukomaa kwa magenge ya kihalifu kitaifa na kimataifa. Huo ni mwanzo wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na matokeo yake vitu vinapewa kipaumbele cha kwanza kuliko utu na heshima ya binadamu! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana ambao ni mashuhuda wa dhuluma, nyanyaso na uhalifu huu dhidi ya ubinadamu watapata fursa ya kushirikisha mang’amuzi yao wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Sinodi iwe ni jukwaa la kuibua mbinu mkakati wa kupambana na changamoto hizi zinazowasibu vijana wa kizazi kipya, ili kwa Serikali, Kanisa pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali waweze kuwa ni msaada mkubwa kwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo: kwa kuwalinda na kuwasaidia.

Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda kwa vijana wenzao katika mapambano dhidi ya matukio haya yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Sinodi kiwe ni chombo cha matumaini mapya kwa Makanisa mahalia kushirikiana na kushikamana kwa kufanya kazi kwa pamoja ili hatimaye, kuunda mtandao wa njia ya wokovu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Mtakatifu Josephine Bakhita kusali, kuwaombea na kuwanusuru waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu unaogusa hata “Madonda ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Watu wa Mungu wajenge na kudumisha utamawaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali! Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anafafanua kwamba, jumla ya vijana 350 wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Vijana kwa mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.