2018-03-15 09:43:00

Ukuu wa Fumbo la Msalaba katika maisha na utume wa Makanisa!


Utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo kama shuhuda wa upendo wa Mungu kwa waja wake; ni utume unaofumbatwa hata katika dhuluma na nyanyaso kama ushuhuda wa uekumene wa damu pamoja na changamoto ya kuendelea kubeba Msalaba na kumfuasa Kristo Yesu kama sehemu ya uinjilishaji wa kina! Hii ni changamoto ya kujizatiti kikamilifu katika mapambano ya kuubeba Msalaba wa “umaskini” kati ya watu wengi duniani, kama vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa walimwengu! Haya ni kati ya mawazo mazito yaliyoibuliwa mwishoni mwa mkutano mkuu wa uinjilishaji ulimwenguni uliokuwa unaratibiwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., lenye wanachama 348 sehemu mbali mbali za dunia, kwenye kilima cha Ngurdoto, Jijini Arusha, Tanzania kuanzia tarehe 8-13 Machi 2018. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”.

Katika hotuba yake, Patriaki Mor Ignatius Aphrem II wa Kanisa zima la Kiorthodox nchini Siria amekazia dhana kwamba, utume wa Kanisa unajikita kwa namna ya pekee kabisa, katika wokovu wa roho za watu, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo ili watu wamfahamu Yesu na nguvu yake inayookoa. Hii, ni dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili na utamaduni wa upendo kwa Mungu na jirani kama unavyobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Wakristo wanaitwa kubeba vyema Misalaba ya maisha yao na kumfuasa Kristo Yesu kwa uaminifu, ari na moyo mkuu. 

Upendo wa Kristo Yesu, ni ushuhuda wa sadaka iliyomwezesha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni upendo unaofumbatwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kristo Yesu ni mfano na kielelezo cha huduma hii, aliyoifanya Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake; Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu akathubutu kufanya kazi ya watumwa, changamoto na mwaliko kwa Mama Kanisa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho; umoja na mshikamano wa dhati, kama ushuhuda wa utume wake!

Patriaki Mor Ignatius Aphrem II anaendelea kufafanua kwamba, kama wafuasi amini wa Kristo Yesu, waamini wanahamasishwa kumfahamu vyema Bwana na Mwalimu wao, kwa kuambata Fumbo la Msalaba, tayari kumfuasa katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, njiani watakumbana na mateso, nyanyaso na dhuluma kwa jina lake. Msalaba ni kielelezo cha hekima, nguvu, huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Msalaba ni hekima ya Mungu, lakini kwa wale wanaopotea ni upuuzi.

Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaendelea kuteswa na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni kundi linalonyimwa haki msingi ya kuabudu na kushuhudia imani yake na matokeo yake ni mauaji ya Wakristo kama Jumuiya ya Kimataifa inavyoshuhudia huko Mashariki ya Kati ambako kwa muda wa miaka mia moja iliyopita, Wakristo wameteswa na kukumbana na mkono wa chuma kutoka kwa watawala mbali mbali. Vita ya hivi karibuni huko Mashariki ya Kati vimepelekea Makanisa mengi na nyumba za Ibada kuharibiwa na kunajisiwa vibaya.

Hata katika mateso na mahangaiko kama haya, Kanisa bado limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa! Mama Kanisa anahimizwa kuendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa: upendo, haki na amani duniani, kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Wakristo wanapaswa kuendelea kuwepo katika maeneo yao ya asili ili kukoleza na kudumisha ari na moyo wa haki, amani na upatanisho kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; katika ukweli na uwazi.

Kanisa huko Mashariki ya Kati linahitaji upendo na mshikamano kutoka kwa Wakristo na watu wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia, sanjari na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, yanayofumbatwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mshikamano miongoni mwa wakristo usaidie kuragisha: mateso, mahangaiko na matumaini ya waamini huko Masharki ya Kati pamoja na kuwa na sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa isaidie kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, utawala wa sharia, utu na heshima ya binadamu. Patriaki Mor Ignatius Aphrem II wa Kanisa zima la Kiorthodox nchini Siria anahitimisha hotuba yake kwa kusema, umefika wakati kwa Kanisa kutoa ushuhuda unaomwilishwa uekumene wa huduma na damu kwa kumshuhudia Kristo Yesu. Wakristo wawe tayari kukumbatia na kuumbata Msalaba, tayari kufuata Njia ya Msalaba kwa kutambua kwamba, Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko ni mwanzo wa maisha mapya!

Kwa upande wake, Mchungaji, Dr. Roberto E. Zwetch wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Brazil, IECLB, anasema, Kanisa halina budi kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa kusimama kidete kupambana na: umaskini, magonjwa na ujinga; maadui wakuu watatu wanaomnyanyasa binadamu. Uinjilishaji hauna budi kufumbatwa katika tamaduni, mila na desturi za watu mahalia. Hii ni dhamana na wajibu wa kuendeleza kazi ya: kuganga na kutibu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Wakristo wajifunze kubeba Msalaba wa Kristo Mteswa, ili, kupambana fika dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi binadamu, utu na heshima yake. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, imani, matumaini na huduma ili kupambana na changamoto mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.