2018-03-12 10:54:00

Askofu mkuu Josè A. Bettencourt ateuliwa kuwa Balozi wa Georgia


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Josè Avelino Bettencourt kuwa ni Balozi mpya wa Vatican  nchini Georgia. Ataendelea pia kuwa ni mwakilishi wa Vatican nchini Armenia  pamoja na kuwa Mkuu wa Itifaki ya Vatican. Askofu mkuu Bettencourt alizaliwa tarehe 23 Mei 1962 huko Azzorre, nchini Ureno. Baada ya majiundo na malezi yake ya Kikasisi, kunako tarehe 29 Juni 1993 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo kuu la Ottawa, Canada. Ana shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.

Alianza utume wake katika masuala ya kidiplomasia mjini Vatican kunako tarehe 1 Julai 1999. Katika maisha na utume wake tangu wakati huo, ametoa huduma kwenye Ubalozi wa Vatican nchini DRC na baadaye, kwenye Idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Baadaye Papa Mstaafu Benedikto XVI aliteuliwa kuwa mkuu wa Itifaki ya Vatican, hapo tarehe 14 Novemba 2012. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Armenia mwaka 2018 na kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.