2018-03-07 07:10:00

Kanisa linataka kuwa karibu zaidi na maskini na wale wanaoteseka!


Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ni sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Sekretarieti kuu ya Vatican ili kuboresha huduma ya Kanisa, kwa kuliwezesha Kanisa kuwa karibu na watu wanaotafuta matumaini na ukamilifu wa maisha yao. Kanisa linataka kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia, mipasuko ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Kanisa linatambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; binadamu anayependwa sana na Mungu kwani amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Mwanadamu katika hija ya maisha yake, daima anatafuta mambo msingi yanayosimikwa katika matumaini. Kumbe, ni wajibu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu kuwasaidia watu kutimiza ndoto hii njema kadiri ya uwezo na nafasi iliyopo.

Haya yamesemwa hvi karibuni na Monsinyo Segundo Tejado Munoz, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano. Anasema katika maisha na utume wake, daima amekutana na maskini na watu waliokata tamaa ya maisha kutokana na changamoto mbali mbali walizokutana nazo katika safari yao. Hawa ndio ambao Mwenyezi Mungu anataka awahudumie katika maisha na utume wake kama Padre, kwa kutambua kwamba, maskini ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa; wao ndio walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko

Monsinyo Segundo Tejado Munoz anasema, katika maisha na utume wake amewahi kutumwa na Askofu wake kutoka Hispania kwenda nchini Albania ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Kanisa baada ya kuanguka na kuporomoka utawala wa Kikomunisti nchini humo, ulioacha majeraha na machungu makubwa kwa familia ya Mungu nchini Albania. Kunako mwaka 1993 akaanza utume wake wa kimissionari huko Tirana, nchini Albania, muda mfupi tu, baada ya kuporomoka Ukuta wa Berlin. Huko akakutana na watu walioweza kufurahia maisha, hata kwa kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu aliwakirimia katika maisha.

Akateuliwa kuwa mkurugenzi wa Caritas, Albania na huko akapambana na changamoto za kijamii, athari za vita ya Kosovo ya Mwaka 1999 pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, waliokuwa wanatafuta usalama na hifadhi ya maisha. Katika mazingira kama haya, akagundua kiu ya watu wa familia ya Mungu katika maisha yao ya kiroho, kiutu na kimaadili ambayo yalipaswa kusimikwa kwa namna ya pekee katika: Sala, Sakramenti za Kanisa na Neno la Mungu pamoja na kuendelea kuimarisha maisha yao ya Kikristo, ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizokuwa zinaendelea kujitokeza.

Kufumba na kufumbua, Kanisa Katoliki nchini Albania likajikuta likiwa na umati mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji mbele yake: lakini umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ukaliwezesha Kanisa kuweza kuwahudumia watu hawa, kwa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio chao kadiri ya uwezo wake. Waamini wakafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji walikuwa wanapata walau chakula cha kuwawezesha kuishi. Hapa, Kanisa likaonesha na kushuhudia uwezo wake wa kuwa karibu na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Itakumbukwa kwamba, Monsinyo Segundo Tejado Munoz, tangu mwaka 2003 amekuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa lililokuwa linaratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum sanjari na kusimamia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni huduma inayotekelezwa na Vatican kwa kushirikiana na Makanisa mahalia, waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaotamani kuona watu wakiwezeshwa ili kuondokana na umaskini, ujinga na mardhi, maadui wakuu wa maendeleo endelevu ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili kama mwendelezo wa mchakato wa kazi ya ukombozi, iliyoanzishwa na Kristo Yesu, aliyewahudumia watu katika maisha yao ya kiroho: kwa kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwaondolea dhambi zao; kwa kuwaponya magonjwa na mahangaiko yao ya ndani pamoja na kuwalisha walipokuwa na njaa. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia watu walioathirika kwa majanga asilia kama yaliyojitokeza nchini Japan, Ufilippini na Equador, ili kuwarejeshea watu matumaini ya maisha, imani na mapendo, kumwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maeneo na mazingira kama haya ni dhamana nyeti sana inayohitaji unyenyekevu wa hali ya juu, unaoshuhudia uwepo wa huduma ya upendo inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kanisa halina utajiri wala rasilimali fedha na vitu kuweza kuwasaidia watu wote wanaokumbana na majanga asilia katika maisha yao, lakini uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni alama ya matumaini, imani na mapendo thabiti. Katika hali ya utupu na mahitaji makubwa, watu wengi wanapenda kuona uwepo endelevu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa uwepo wa Kanisa, mahali ambapo waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaweza kukusanyika kumshukuru, kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu! Kama  waamini wanataka kwa mara nyingine kusali kwa pamoja, ili kuonja uwepo wa Mungu kati yao katika shida na mahangaiko yao ya ndani!

Hii ndiyo dhamana na changamoto inayofanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu chini ya uongozi wa Kardinali Peter Turkson. Hili ni Baraza ambalo kwa sasa linakabiliana na changamoto katika: shughuli za kichungaji, huduma ya huruma na upendo sanjari na mshikamano wa dhati na watu wa Mungu. Hii ni huduma inayomwilishwa katika sekta ya afya; wakimbizi na wahamiaji; Utume wa Bahari; watu wasiokuwa na makazi maalum; wahudumu wa hospitali na magereza. Dhamana hii inatekelezwa kwa njia ya ushirikiano wa karibu sana na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Kimataifa, “Caritas Internationalis” pamoja na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kitaifa na kimataifa bila kuyasahau Makanisa mahalia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.