2018-03-06 14:30:00

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulinda utu na haki msingi za watoto


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulinda na kudumisha haki msingi za watoto, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wanapata elimu bora na huduma msingi ya afya hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2017 kumekuwepo na watoto zaidi ya milioni 535 walioathirika kutokana na: vita, kinzani na athari za mabadiliko ya tabianchi. Watoto hawa wamejikuta wakitumbukia na kutumbukizwa katika wimbi la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Matokeo yake ni kwamba, baadhi yao wana nyanyaswa, wanadhulumiwa na kutumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo!

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa Vatican katika mkutano wa haki msingi za binadamu, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipotolewa na Umoja wa Mataifa. Ujumbe wa Vatican pamoja na mambo mengine, unapenda kukazia kwa namna ya pekee, utu na heshima ya watoto wanaojikuta katika mazingira magumu na hatarishi kwani, vitendo hivi vina madhara makubwa katika: akili, maisha yao ya kijamii na ukuaji wao kwa sasa na kwa siku za usoni! Elimu bora na huduma msingi za afya ni sehemu ya haki msingi ambazo watoto wanapaswa kupatiwa, ili kuwajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali haina budi kuhakikisha kwamba, watoto wanalindwa, wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama kielelezo cha ushuhuda wa mshikamano kwa kutambua kwamba, watoto ni matumaini na jeuri ya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao. Watu waong’oe ndani mwao ndago za: ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; wasimame kidete kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na kulinda mazingira nyumba ya wote. Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu wa kuwalinda, kuwatetea na kuwatunza watoto kwa kuwapatia mahitaji yao msingi, ili kuwajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.